Polisi nchini Kenya wamepiga marufuku maandamano yaliyopangwa kufanyika Jumatatu jijini Nairobi. Maandamano yaliyopendekezwa na kiongozi wa upinzani Raila Odinga ni kinyume cha sheria, kulingana na Inspekta Mkuu wa Polisi Japhet Koome. Kile ambacho serikali iliita maandamano yasiyoidhinishwa katika miji kadhaa ya Kenya Jumatatu iliyopita yaligeuka kuwa ghasia, na kuua mwanafunzi mmoja wa chuo kikuu na kujeruhi wengine kadhaa. Waandamanaji waliwarushia mawe polisi wa kutuliza ghasia nje ya ofisi za serikali katika mji mkuu na kuchoma matairi barabarani. Polisi walitumia gesi ya kutoa machozi na kuwakamata viongozi watatu wa upinzani na zaidi ya waandamanaji 200.