SPD imemchagua mwanamke kwa mara ya kwanza katika historia yake ya miaka 155 kuwa mwenyekiti. Mivutano iliyopo ndani ya chama hicho ni mzigo mkubwa unaomsubiri kiongozi mpya Kwa mara ya kwanza katika historia ya miaka 155 ya chama cha Social Democratic SPD nchini Ujerumani kimemchagua mwanamke kukiongoza chama hicho. Katika mkutano maalum wa chama uliofanyika leo Jumapili(22.04.2018) katika mji wa Magharibi mwa Ujerumani wa Wiesbaden wanachama wa SPD wamepiga kura kuchagua kati ya wagombea wawili -Andrea Nahles ambaye ni kiongozi wa chama hicho bungeni au meya wa jiji la Flensburg Simone Lange. Mshindi wa nafasi ya mwenyekiti wa SPD ana majukumu ya kutuliza mivutano ya ndani ya chama wakati ambapo chama hicho kinapambana kujiweka katika nafasi nzuri baada ya kupata kipigo na kuporomoka kufuatia matokeo mabaya ya uchaguzi mkuu uliofanyika mnamo mwezi Septemba mwaka 2017 sambamba na kujengeka upinzani wa wanachama wanaopinga chama hicho kuingia katika serikali ya mseto...