Kama Uingereza itashindwa kufafanua kuhusu ni nani anayeongoza utaratibu na kutoa maamuzi muhimu kuhusu Brexit, Umoja wa Ulaya utalazimika kuendelea kusubiri tu. Kwanza, Waziri anayehusika na masuala ya Brexit David Davis alijiuzulu, kisha Waziri wa Mambo ya Nchi za Kigeni na aliyeongoza kampeni za kuitaka Uingereza kujiondoa Ulaya Boris Johnson akafuata. Wanalivuruga jaribio la Waziri Mkuu Theresa May la kuishawishi serikali yake kukubali Uingereza kuendeleza mahusiano ya karibu na Umoja wa Ulaya baada ya Brexit. Kujiuzulu huko kulikoratibiwa kwa mawaziri hao wenye misimamo mikali kuhusu Brexit kunaitumbukiza serikali ya May katika mgogoro na kuvuruga matumaini ya Umoja wa Ulaya ya kuweza hatimaye kuanza, katika wiki chache zijazo, mazungumzo muhimu kuhusu makubaliano ya kutengana na mahusiano ya usoni kati ya Uingereza na umoja huo. Ni Ijumaa iliyopita tu ambapo May alijaribu, kulazimisha kuliunganisha baraza lake la mawaziri linalozozana. Lakini kama mambo yanavyokwend...