Kama Uingereza itashindwa kufafanua kuhusu ni nani anayeongoza utaratibu na kutoa maamuzi muhimu kuhusu Brexit, Umoja wa Ulaya utalazimika kuendelea kusubiri tu.
Kwanza, Waziri anayehusika na masuala ya Brexit David Davis alijiuzulu, kisha Waziri wa Mambo ya Nchi za Kigeni na aliyeongoza kampeni za kuitaka Uingereza kujiondoa Ulaya Boris Johnson akafuata. Wanalivuruga jaribio la Waziri Mkuu Theresa May la kuishawishi serikali yake kukubali Uingereza kuendeleza mahusiano ya karibu na Umoja wa Ulaya baada ya Brexit.
Kujiuzulu huko kulikoratibiwa kwa mawaziri hao wenye misimamo mikali kuhusu Brexit kunaitumbukiza serikali ya May katika mgogoro na kuvuruga matumaini ya Umoja wa Ulaya ya kuweza hatimaye kuanza, katika wiki chache zijazo, mazungumzo muhimu kuhusu makubaliano ya kutengana na mahusiano ya usoni kati ya Uingereza na umoja huo.
Ni Ijumaa iliyopita tu ambapo May alijaribu, kulazimisha kuliunganisha baraza lake la mawaziri linalozozana. Lakini kama mambo yanavyokwenda sasa, jaribio hilo lilishindwa kabisa. Wahafidhina wa Uingereza wamegawika kabisa kuhusu namna ya kushirikiana na Umoja wa Ulaya baada ya Brexit.
Boris Johnson (Kushoto) na Jeremy Hunt
Kwa upande mmoja, wenye msimamo mkali hawako tayari kulegeza msimamo. Katika upande mwingine, wabunge wa msimamo wa wastani wanaamini kuwa aina ya Brexit ambayo wapinzani wao wanataka ni uwendawazimu mtupu
Brexit inaichana katika vipande Uingereza na chama chake cha Conservative na kuharibu mjadala wa kisiasa. Umoja wa Ulaya uliitaka serikali ya Uingereza kutofanya mashauriano kivyake, bali na umoja huo – sasa, mambo yanaonekana kuwa mabaya Zaidi badala ya kuwa bora Zaidi.
Mapendekezo ya May yatakuwa mwanzo tu
Licha ya yote hayo, May anadai kuwa mapendekezo yake ya kuendeleza mahusiano na Umoja wa Ulaya yanaleta suluhisho. Hata hivyo, mapendekezo yaliyowekwa mezani katika mkutano wake na mawaziri, yanatekeleza maslahi ya Uingereza pekee. Hivyo yanaweza, kutumiwa kama chanzo cha kufanya mazungumzo zaidi.
Mapendekezo haya ya chama cha forodha na suala la soko huria kwa mujibu wa maslahi ya Uingereza, katika hali yake ya sasa hayakubaliki na Umoja wa Ulaya. Inabidi wafanye makubaliano zaidi ili kufikia suluhisho ambalo litakubalika pia katika upande wa Umoja wa Ulaya.
Hata kama May atanusurika makabiliano ya sasa na wahafidhina wake wenye msimamo mkali, anaweza bado, hapo baadaye, akaanguka kwa sababu Umoja wa Ulaya hauwezi kumpa tu chochote anachotaka.
Mwandishi wa DW Barbara Wesel
Kuelekea ukingoni
Kwa Umoja wa Ulaya, misukosuko inayoendelea katika serikali ya Uingereza ni kitu kinachobadilisha mkondo ambacho sio cha kawaida na hakikubaliki. Kwa sasa kuna masuala muhimu zaidi ya kushughulikiwa kuliko kukabiliana na kelele na kilio kutoka makundi mbalimbali ya Brexit.
Mkutano wa kilele unaokaribia wa jumuiya ya Kujihami ya NATO na Rais Donald Trump wa Marekani, mkutano wake na Rais wa Urusi Vladmir Putin, mgogoro kuhusu sera ya uhamiaji na ongezeko la siasa kali za kizalendo nchini Poland, Italia na Austria ni mambo yanayoangaziwa kwa sasa na mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya.
Badala yake, mazungumzo ya Brexit ambayo yanaendelea kufanya mizunguko ya mduara yanamaliza nguvu na muda. Inaonekana kuwa viongozi wa Uingereza ambao ni wapinzani wakali wa Umoja wa Ulaya wanapuuza hali ya ulimwengu, au wanaamini kuwa wanaweza kupambana na changamoto hizo peke yao.
Lakini kama serikali ya Uingereza haitaeleza wazi ni nani anayefanya maamuzi linapokuja suala la Brexit na nani anayewakilisha maoni ya wengi katika Umoja wa Ulaya, haitawezakana kuendeleza mazungumzo. Wanadiplomasia wa Umoja wa Ulaya watalazimika kusubiri hadi mapambano ya madaraka nchini Uingereza yatakapomalizika.
Maoni