SHERIA 17 ZA SOKA
=======================
Mchezo wa soka ni moja ya michezo maarufu sana duniani na ni biashara kubwa sana katika ulimwengu wa michezo na ukitaka kuamini hili angalia makampuni yaliyowekeza katika kudhamini soka – ni makampuni makubwa makubwa yenye hadhi ya kitaifa na kimataifa. Kwa kuzingatia aina hii ya wadhamini, waendeshaji wa mchezo wa soka, wameweka kanuni na miongozo ya kufuatwa ili kuhakikisha kuwa wale wanaowekeza pesa zao wanaona thamani ya uwekezaji wao. Kwa hiyo soka kama ilivyo katika michezo mingine inazo kanuni na tutajadili kanuni moja baada ya nyingine kama zilivobainishwa katika muongozo wa FIFA unaojulikana kwa jina la Law of the Game.
Sheria Namba 1: Dimba
==============
NYASI - Dimba la soka litakuwa la nyasi asilia au bandia kulingana na kanuni za masindano na nyasi hizo lazima ziwe za rangi ya kijani. Kwa dimba la nyasi bandia na kama mchezo unaochezwa utakuwa wa kutambuliwa na FIFA, basi nyasi hizo bandia lazima zikidhi viwango maalumu vya FIFA.
ALAMA MBALIMBALI – Dimba la soka litakuwa la umbo la mstatili na michoro mbalimbali ya mistari. Mistari hii ni kwa ajili ya maeneo husika ambamo imechorwa. Kuna mistari miwili mirefu inayojulikana kama mistari ya pembeni na mingine miwili mifupi inayoitwa mistari ya goli. Kiwanja kimegawanywa katika pande sawa mbili kwa mstari unaoitwa Mstari wa Katikati – mstari huu hugawa mistari ya pembeni katika pande mbili zilizo sawa. Pia kipo kitovu cha uwanja ambayo ni sehemu ya katikati kabisa ya uwanja. Kitovu hiki kimezungukwa na duara la kipenyo cha mita 9.15.
VIPIMO
urefu wa mstari wa pembeni lazima uwe mkubwa kuliko urefu wa mastari wa goli.
Urefu wa mstari wa pembeni ni mita 90 (yadi 100) au 120 (yadi 130).
Urefu wa mstari wa goli ni mita 45 (yadi 50) au 90 (yadi 100)
Mistari yote itakuwa na upana ulio sawa usiozidi sentimeta 12.
Kwa mechi za kimataifa, upana na urefu wa dimba utakuwa kama ifuatavyo:
Urefu: mita 100 (yadi 110) mpaka 110 (yadi 120)
Upana : mita 64 (yadi 70) mpaka 75 (yadi 80)
ENEO LA GOLI
Eneo la goli litaundwa na mistari miwili iliyochorwa pembe-mraba na na mstari wa goli umbali mita 5.5 (yadi 6) kutoka kila mlingoti wa goli. Mistari hii itaingia ndani ya eleo la uwanja kiasi mita 5.5 (yadi 6) kisha mistari hii itaunganishwa na mstari uliochorwa sambamba na mstari wa goli.
ENEO LA PENATI
Eneo la penati litaundwa na mistari miwili iliyochorwa pembe-mraba na mstari wa goli kiasi mita 16.5 (yadi 18) kuelekea ndani ya uwanja na itaunganishwa na mstari uliochorwa sambamba na mstari wa goli. Kwa kila eneo la penati, kutakuwa na kitovu cha kupigia penati ambayo itakuwa ndiyo alama ya kuweka mpira kwa ajili ya kupiga tuta – alama hii itachorwa eneo usawa wa kitovu cha goli na itakuwa umbali wa mita 11 (yadi 12). Mstari wa upinde wa duara la mita 9.15 (yadi 10) utachorwa kutoka kitovu cha kupigia penati kuelekea upande wa nje ya eneo la penati.
VIBENDERA VYA KONA
Kutakuwa na vibendera vya kona vyenye kimo cha takribani mita 1.5 (futi 5) visivyo na ncha-kali sehemu ya juu na lazima vitawekwa katika kila kona ya uwanja. Vibendera hivi vinaweza kuwekwa pia katika mstari wa katikati kiasi umbali wa mita moja kutoka usawa wa matari wa pembeni.
KIROBO-DUARA CHA KONA
Kutakuwa na virobo-duara vya nusu-kipenyo cha mita 1 (yadi 1) katika kila kibendera cha kona, ndani ya eneo la uwanja.
MAGOLI
katikati ya kila mstari wa goli litasimikwa goli. Lango hili litakuwa na milingoti miwili iliyosimikwa umbali sawa kutoka kila upande wa kibendera cha kona. Milingoti hii itaunganishwa na mtambaa-panya sehemu ya juu. Nguzo na mtambaa panya vinaweza kuwa katika mfumo wa miti, chuma au aina nyingine ya matirio iliyothibitishwa. Vinaweza pia kuwa na maumbo ya mraba, mstatili, mduara au umbile la yai na hayatakuwa hatarishi kwa wachezaji. Umbali kati ya milingoti ni mita 7.32 (yadi 8) na umbali kutoka mtambaa-panya kuja chini katika mstari wa goli itakuwa ni mita 2.44 (futi 8).
Milingoti na mtambaa-panya vitakuwa na upana unaolingana usiozidi sentimeta 12 (inchi 5). Mstari wa goli nao pia utakuwa na upana sawa na milingoti pamoja na mtambaa-panya wa goli. Nyavu zinaweza kufungwa katika magoli na sakafu iliyo nyumba ya goli alimradi tu zitapashwa kufungwa vyema kiasi cha kutokuleta bughudha kwa mlinda mlango.
Nguzo za goli (yaani milingoti miwili na mtambaa-panya) lazima zitakuwa na rangi nyeupe.
USALAMA
Malango lazima yasimikwe imara ardhini. Magoli ya kuhamisha yanaweza kutumika tu ikiwa kama yatakuwa yanakidhi sharti hili.
MUONGOZO WA KAMATI MAALUMU YA FIFA
MUONGOZO 1:
Ikiwa kama kutakuwa na eneo maalumu kwa ajili ya kusimama makocha wa timu zinazopambana, lazima eneo hilo litakidhi matakwa yaliyothibitishwa na Bodi ya Vyama vya Soka Kimataifa kama tutakavyoona hapo baadae katika kipengele cha Eneo la Ufundi.
MUONGOZO 2:
Pale itakapotakiwa kutumika teknolojia maalumu ya goli (goal-line technology), marekebisho ya muundo wa goli yanaweza kufanyika . marekebisho haya lazima yatakidhi matakwa ya program maalumu ya FiFa.
++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
SHERIA NAMBA 2: MPIRA
Kwa wasomaji wapya. Jana tulitizama Sheria Namba 1 inayoelezea kuhusu Dimba la Soka. Leo tutatizama sheria namba 2. Sheria hii inazungumzia kwa muhtasari kuhusu mpira. Wengine wanaita boli. Wengine gozi la ng’ombe. Mimi hupenda kuita jabulani nikitiwa hamasa na mpira wa Nike uliotumika katika Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010, huko Bondeni kwa Madiba. Kama na wewe una jina unalopendelea utatuambia unaitwa je?
UMBILE NA VIPIMO:
Mpira wa soka utakuwa na sifa zifuatazo:
Umbo la tufe
Utatengenezwa kwa matirio ya ngozi au matirio nyingine itakayokuwa inafaa
Mduara usiozidi sentimeta 70 (inchi 20) na usiopungua sentimeta 68 (inchi 27)
Usiozidi gramu 450 na usiopungua gramu 410
Mgandamizo (presha) kati ya 600-1100g/cm2 kutoka usawa wa bahari.
KUBADILISHA MPIRA MBOVU
Ikiwa kama mpira utapasuka ama utapata kasoro wakati wa mchezo yafuatayo yatafanyika:
Mchezo utasimama
Mchezo utaanza tena kwa mwamuzi kudondosha mpira eneo ambapo mpira wa awali ulipata kasoro, isipokuwa tu kama mchezo ulisimamishwa ndani ya eneo la goli ambapo katika hali kama hiyo mwamuzi ataudondosha mpira mpya eneo la goli sambamba na mstari wa goli katika pahala karibu na ulipokuwa mpira ulioharibika kabla ya mchezo kusimama.
Ikiwa kama mpira utapasuka ama utapata kasoro wakati wa kupiga mkwaju wa penati au penati ikiwa imeshapigwa tayari, na haukumgusa mchezaji yeyote ama milingoti ya goli ama mtambaa-panya wa goli, penati itarudiwa.
Ikiwa kama mpira utapasuka ama utapata kasoro sekunde chache kabla ya mchezo kuanza, au wakati wa golikiki, au wakati wa konakiki au wakati wa frikiki au wakati penati au wakati wa kurusha, zoezi litarudiwa.
Ieleweke katika kanuni hii kwamba mpira hautabadilishwa isipokuwa kwa idhini ya mwamuzi.
NYONGEZA
Mipira itakayokubalika katika michezo mbali mbali inayotabuliwa na FIFA itatakiwa kuwa na alama zifuatazo:
FIFA Quality Pro
FIFA Quality
IMS – International Match Standard
Alama hizi zitaashiria kwamba mpira husika unakidhi viwango vya ubora vilivyobainishwa na FIFA na kwamba mashirika au makampuni yatakayofanya kazi ya kupima ubora wa mipira lazima yatapata kibali cha FIFA. Vyama wanachama wa FIFA wataruhusiwa kutumia mipira yenye alama hizo tatu zilizobainishwa hapo juu.
habari wadau. tunaendelea. na leo tutatizama Sheria Namba 3. Hii inahusu idadi ya wachezaji. karibuni...
+++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
SHERIA NAMBA 3: IDADI YA WACHEZAJI
Mchezo wa soka utachezwa baina ya timu mbili, kila moja ikiwa na wachezaji wasiozidi 11, miongoni mwao mmoja atakuwa mlindamlango. Mchezo unaweza usichezwe ikiwa moja kati ya timu zinazopambana itakuwa na wachezaji chini ya 7.
Mabadiliko:- kwa michezo maalum inayotambuliwa au kutii miongozo ya FIFA, idadi ya wachezaji kwa ajili ya kufanya mabadiliko itakuwa isiyozidi wa 3. Hata hivyo kanuni za mashindano husika zinaweza kubainisha idadi ya wachezaji wa mabadiliko kuanzia wa 3 lakini wasiozidi 12. Lakini, kwa mechi za timu ya taifa idadi ya juu kabisa ya wachezaji wa mabadiliko itakayokubalika itakuwa ni 6.
Kwa michezo mingine isiyosimamiwa wala kufuata kanuni za FIFA, idadi kubwa ya mabadiliko inaweza kufanyika kwa kuzingatia yafuatayo:
Timu zinazoshiriki zitakubaliana idadi ya wachezaji wa mabadiliko
Mwamuzi apewe taarifa kabla ya mchezo
Ikiwa kama mwamuzi hakutaarifiwa, au kama hakuna makubaliano yaliyofikiwa baina ya timu kabla ya mchezo, basi idadi ya mabadiliko yanayokubalika haitazidi wachezaji 6.
Kurejerea mabadiliko:- mchezaji aliyekwisha kufanyiwa mabadiliko na kutoka kwa kadiri ya kanuni za FIFA hatoruhusiwa tena kuingia uwanjani kucheza katika mchezo uleule. Mabadiliko ya namna hii yatakubalika katika michezo ya ndondo tu kwa kadiri ya makubaliano ya waandaaji wa hizo ndondo.
Utaratibu wa Kufanya mabadiliko
Katika kila mchezo, majina ya wachezaji watakaofanyiwa mabadiliko yatakabidhiwa kwa mwamuzi kabla ya mchezo kuanza. Mchezaji yeyote ambaye jina lake halitakuwa miongoni mwa majina aliyokabidhiwa mwamuzi hatopaswa kucheza katika mchezo husika.
Taratibu za kufuata wakati wa kufanya mabadiliko:
Mwamuzi lazima ataarifiwe kabla ya kufanya mabadiliko
Mchezaji anayetarajiwa kuingia hatoruhusiwa kuingia dimbani mpaka yule anayetoka awe ametoka kwelikweli uwanjani na kwamba mwamuzi atamuashiria yule anayeingia kwamba ‘sasa unaweza kuingia bwana mkubwa’
Mchezaji anayeingia atapitia mstari wa katikati ya dimba na kwamba atafanya hivyo wakati ambapo mchezo utakuwa umesimama.
Mabadiliko yatakamilika pale mchezaji anayeingia atakuwa ameingia dimbani
Mchezaji aliyetoka hatoruhusiwa tena kucheza katika mchezo husika isipokuwa tu kama kanuni za ndondo zitatumika.
Mwamuzi atakuwa mwenye mamlaka ya mwisho kama mchezaji aingie au asiingie.
Kubadili mlindamlango:- mchezaji yeyote anaweza kubadilishana nafasi na mlindamlango ikiwa tu mwamuzi atataarifiwa kabla mabadiliko kufanyika na kwamba mabadiliko hayo yafanyike wakati mchezo umesimama.
UKIUKWAJI WA SHERIA HII NA ADHABU ZAKE
Ikiwa kama mchezaji wa mabadiliko ataingia dimbani bila ruksa ya mwamuzi yafuatayo yatatokea:
Mwamuzi atasimamisha mchezo (japo si muda uleule ambao mchezaji atakuwa ameingi ama mchezaji huyo hataingilia mchezo)
Mwamuzi atamuonesha kadi ya njano kwa kufanya kitendo kisicho cha uanamichezo na kwamba atamuamuru atoke nje
Ikiwa kama mwamuzi atakuwa alisimamisha mchezo, itabidi auanzishe kwa kupigwa mpira wa adhabu usio wa moja kwa moja dhidi ya timu ya mchezaji aliyeingia uwanjani kienyeji.
Ikiwa kama yatafanyika mabadiliko kwa kutumia mchezaji ambaye hakutajwa katika orodha ya wachezaji wa mabadiliko aliyokabidhiwa mwamuzi na kwamba mwamuzi hakujulishwa juu ya mabadiliko hayo:
Mwamuzi atamruhusu yule mchezaji aingie
Mchezaji aliyeingia hatapewa adhabu yoyote
Idadi ya wachezaji wanaopashwa kufanya mabadiliko katika orodha aliyopewa mwamuzi haitapunguzwa
Mwamuzi atatoa ripoti ya tukio hili kwa mamlaka husika.
Ikiwa kama mlinda mlango na mchezaji watabadilishana nafasi bila ufahamu wa mwamuzi, mwamuzi ataruhusu mchezo uendelee mpaka pale mpira utakapotoka nje na ni hapo mwamuzi atawalima kadi za njano wachezaji waliohusika.
Ikiwa kama kutafanyika ukiukwaji mwingine wa kanunu hii tofauti na zilizotajwa, mchezaji atakayehusika ataoneshwa kadi ya njano na mchezo utarejelewa tena kwa mpira wa adhabu isiyo wa moja kwa moja dhidi ya timu ya mchezaji aliyevunja kanuni.
Kadi nyekundu
Mchezaji atakayeoneshwa kadi nyekundu kabla ya mchezo kuanza anaweza kubadilishwa na mmoja wa wachezaji walio katika orodha ya mwamuzi ya wachezaji wa mabadiliko.
Mchezaji wa mabadiliko aliyeoneshwa kadi nyekundu kabla au baada ya kuanza kwa mechi hatoruhusiwa kufanyiwa mabadiliko tena.
+++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
SHERIA NAMBA 4: VIFAA VYA WACHEZAJI
Usalama :- mchezaji hatakiwi kuvaa kifaa au kitu chochote hatarishi kwake au kwa mchezaji mwenzake. Hii ni pamoja na vito vya thamani kama pete, mikufu n.k.
Vifaa muhimu :- vifaa muhimu kwa ajili ya mchezaji vitakuwa ni pamoja na vifuatavyo:
Jezi yenye mikono – kama mchezaji atakuwa amevaa nguo nyingine ndani, rangi ya mikono ya hiyo nguo ya ndani itapaswa kuwa sawasawa na rangi ya mikono ya jezi.
Bukta – kama mchezaji atakuwa amevaa nguo ya ndani kama vile taiti au , rangi ya hiyo taiti lazima iwe sawa na rangi kuu ya bukta. Mfano kama rangi ya bukta ni nyekundu yenye michirizi mieupe, basi rangi ya taiti itatakiwa kuwa na rangi nyekundu.
Soksi
Vikinga-ugoko (shinguargds)
Viatu – njumu
Maelezo kuhusu vikinga-ugoko:
Lazima vifunikwe gubigubi na soksi
Vitatengenezwa ka mipira, plastiki, au matirio yoyote inayofaa ya kufanana na hayo
Vitatakiwa kuwa kinga kwa miguu ya mchezaji kwa kiwango fulani.
Rangi
timu zinazopambana zitavaa rangi tofauti tofauti na rangi za timu zote mbili zitakuwa tofauti na rangi za wamuzi.
Kila mlindamlango atavaa rangi tofauti na wachezaji wenzake pamoja na waamuzi.
UKIUKWAJI WA SHARIA HII NA ADHABU ZAKE
ikiwa kama sharia hii itakiukwa, mchezo hautasimama, ila mwamuzi atamuru mchezaji aliyefanya makosa kutoka nje ya uwanja kusahihisha makosa yake ya kiuvaaji. Mchezaji atatoka nje ya uwanja pale mpira utakapokuwa umesimama kwa sababu ya kutoka nje au sababu nyingine.
Mchezaji yoyote atakayepaswa kutoka nje ya uwanja kwenda kurekebisha uvaaji wake hatorudi ndani ya uwanja isipokuwa kwa kuruhusiwa na mwamuzi. Mwamuzi atajiridhisha kwanza ikiwa kama mchezaji amerekebisha uvaaji wake kabla ya kumruhusu kurejea uwanjani.
Mwamuzi atamruhusu mchezaji kuingia pale tu mpira utakapokuwa umetoka nje ya uwanja.
Mchezaji aliyeamuriwa kutoka kwenda kurekebisha uvaaji wake akirejea bila ruksa ya mwamuzi atalimwa kadi ya njano.
Kurejelewa kwa mchezo:- ikiwa kama mwamuzi atasimamisha mchezo kwa ajili ya kutoa adhabu ya kadi ya njano, mchezo utarejelewa kwa kupigwa kwa mpira wa adhabu ndogo dhidi ya timu ya mchezaji aliyepigwa kadi ya njano.
MSIMAMO WA FIFA JUU YA SHERIA HII:
Kuhusu vifaa muhimu vya michezo:
Vifaa muhimu vya michezo havitakuwa na maneno au misemo au vijembe vya kisiasa, au kiimani, au hata misemo binafsi, au picha zenye ujumbe fulani usioendana na maudhui ya mchezo wa mpira wa miguu. Adhabu itatolewa dhidi ya timu ya mchezaji atakaekiuka sheria hii.
Mavazi ya ndani:
Wachezaji hawataruhusiwa kuonesha maandishi yaliyo katika nguo za ndani yenye maudhui ya itikadi za kisiasa au imani za kidini isipokuwa kwa nembo ya makampuni yaliyotengeneza hilo wazi. Mchezaji au timu ya mchezaji itakayokiuka sheria hii itakumbana na rungu la FIFA.
++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
Sheria Namba 5: Mwamuzi
Mamlaka ya Mwamuzi
Kila mchezo utaendeshwa na mwamuzi ambaye atakuwa na mamlaka kamili ya kuhakikisha sheria za soka zinafuatwa katika mchezo atakaokuwa amepangiwa kuchezesha.
Nguvu na Majukumu
Mwamuzi atahakikisha:
Sheria za soka zinafuatwa
Ataongoza mchezo kwa msaada wa waamuzi wasaidizi na itakapobidi atasaidiwa pia na kamisaa
Atahakikisha kuwa mpira utakaotumika unakidhi viwango vilivyobainishwa katika Sheria Namba 2
Atahakikisha kuwa vifaa vya wachezaji vinakidhi Sheria Namba 4
Atadhibiti muda na kuweka kumbukumbu ya matukio katika mchezo
Atasimamisha, kusubirisha au kuahirisha mchezo kwa utashi wake ikiwa kama kuna sheria itakiukwa.
Atasimamisha, kusubirisha, au kuahirisha mchezo ikiwa kutatokea sintofahamu ya aina yoyote kutoka nje ya uwanja
Atasimamisha mchezo ikiwa kwa maoni yake atajiridhisha kuwa kuna mchezaji ameumia sana na atahakikisha mchezaji yule anaondolewa uwanjani. Mchezaji aliyeumia atarejea tu uwanjani baada ya mchezo kuwa umeanza tena.
Ataruhusu mchezo uendelee mpaka pale mpira utakapotoka nje ikiwa kwa maoni yake atajiridhisha kuwa kuna mchezaji ameumia na kwamba mchezaji huyo hakuumia sana.
Atahakikisha kuwa mchezaji anayetokwa na damu ametoka nje ya uwanja na kwamba mchezaji huyo atarudi tu uwanjani ikiwa damu zitakuwa zimekoma kumtoka na kwamba hawezi kurudi kienyeji mpaka pale mwamuzi atakapomuonesha ishara ya kumruhusu kurudi.
Ataruhusu mchezo uendelee ikiwa kama timu iliyofanyiwa madhambi watanufaika na kuendelea kwa mchezo na kama hawatanufaika mwamuzi atarejerea madhambi ya awali na kuruhusu kupigwa kwa mpira wa adhabu.
Atamuadhibu mchezaji atakayefanya madhambi mfululizo katika muda uleule mfupi
Atamchukulia hatua za kinidhamu chezaji atakaefanya makosa ya kustahili kadi ya njano au kadi nyekundu lakini atafanya hivyo tu mpaka pale mpira utakapokuwa umetoka nje.
Atachukua hatua dhidi ya maofisa wa timu watakaoonesha utovu wa nidhamu na kwa utashi wake anaweza kuwaamuru kutoka uwanjani.
Atachukua hatua kutokana na ushauri wa mwamuzi msaidizi kwa matukio ambayo kwa bahati mbaya hakuona
Atahakikisha kuwa mtu asiyehusika haruhusiwi kuingia uwanjani
Ataashiria kuanza kwa mchezo baada ya kuwa umesimama
Atawakabidhi mamlaka ripoti ya mchezo ambayo itaambatana na taarifa juu ya hatua za kinidhamu alizochukua dhidi ya wachezaji au viongozi wa timu na matukio mengine ambayo yatatokea kabla, wakati na baada ya mchezo.
Maamuzi ya Mwamuzi
Maamuzi ya mwamuzi yatakuwa ya mwisho. Hii ni pamoja na ikiwa kama goli limefungwa ama halikufungwa na matokeo ya jumla ya mchezo.
Mwamuzi atabadili maamuzi ikiwa tu kwa akili zake atagundua kuwa amekosea au kama atashauriwa na mwamuzi msaidizi au kamisaa – lakini kwa sharti kwamba asijekuwa ameshaanzisha mchezo au amemaliza mchezo.
++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
Sheria Namba 6: Waaamuzi Wasaidizi
Majukumu:- watateuliwa waamuzi wasaidizi wawili ambao majukumu yao yatakuwa kama ifuatavyo:
Wataashiria mpira wote umetoka nje ya uwanja
Wataashiria ni timu gani inapaswa kupiga kona, goal kick, au kurusha mpira
Wataashiria ikiwa kama mchezaji ameotea
Wataashiria kufanyika kwa mabadiliko
Wataashiria juu ya matukio yoyote ambayo mwamuzi wa kati atakuwa hakuona.
Wataashiria juu ya madhambi yanayoweza kufanyika na wao kuona vema zaidi kuliko mwamuzi wa kati. Hii ni pamoja na madhambi yanayofanyika katika eneo la penati.
Wataashiria ikiwa wakati wa upigaji wa mkwaju wa penati, mlinda-mlango alihama kutoka mstari wa goli kabla ya penati kupigwa na pia wataashiria kama mpira umevuka mstari au laa.
++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
SHERIA NAMBA 7: MUDA WA MCHEZO
Vipindi:- Mpambano wa soka utakuwa na vipindi viwili vya dakika 45 kila kimoja, isipokuwa kama itakubaliwa vinginevyo kati ya mwamuzi wa kati na timu zinazopambana. Makubaliano yoyote ya kubadili muda wa vipindi vya mchezo mfano kupunguza muda na kuwa dakika 40 kutokana na kutokuwa na mwanga wa kutosha uwanjani lazima yafanyike kabla ya kuanza kwa mchezo na yakidhi kanuni za mashindano husika.
Mapumziko:- wachezaji wanastahili kupata mapumziko ambayo hayatazidi dakika 15. Hata hivyo kanuni za mashindano zitatakiwa kubainisha muda halisi wa mapumziko na mabadiliko yoyote juu ya urefu wa muda wa kupumzika lazima yapate idhini ya mwamuzi wa kati.
Muda wa nyongeza:- kutakuwa na muda wa dakika za nyongeza kwa vipindi vyote viwili utakaotokana na kupotea kwa muda kutokana na yafuatayo:
Kufanyika kwa mabadiliko
Kuhudumia mchezaji aliyeumia
Kumuondoa uwanjani mchezaji aliyeumia
Upotezaji wa muda makusudi
Sababu nyingine yoyote
Ieleweke katika sharia hii kwamba dakika za nyongeza zitatolewa kwa hiari ya mwamuzi wa kati.
Kupigwa kwa penati:- ikiwa kama kutatakiwa kupigwa kwa mkwaju wa penati, muda wa kipindi husika utaongezwa mpaka pale mkwaju huo wa penati utakapopigwa – zege halilali.
Mchezo uliokatishwa:- huu utarudiwa isipokuwa tu kama kanuni za mashindano husika zitabainisha vinginevyo.
+++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
SHARIA NAMBA 8: KUANZA KWA MCHEZO
Mwamuzi ataanzisha mchezo ikiwa:-
Itakuwa mwanzo kabisa wa mpambano
Baada ya goli kuwa limefungwa
Mwanzoni mwa kipindi cha pili au dakika za nyongeza (extra time) pale inapobidi
Utaratibu
Kabla ya kuanza kwa mchezo au kuanza kwa kipindi cha dakika za nyongeza yafuatayo yatafanyika:-
mwamuzi atarusha sarafu na timu inayopatia (kama ni mkia au kichwa) itachagua goli la kushambulia katika dakika 45 za kwanza za mchezo.
Timu iliyokosea jibu katika zoezi la urushaji wa sarafu itaanzisha mchezo
Timu iliyopatia jibu katika zoezi ka kurusha sarafu itaanzisha mchezo wakati wa kuanza kwa kipindi cha pili
Wakati wa kipindi cha pili timu zitabadilishana magoli
Kuanza kwa mchezo baada ya goli kuwa limefungwa:-
Baada ya kufungwa kwa goli, timu iliyofungwa itaanzisha mchezo
Wachezaji wa kila timu watakuwa upande wao wa uwanja wakitenganishwa na mstari wa kati
Wachezaji wa timu pinzani ya ile inayoanzisha mchezo watakuwa umbali wa mita 9.15 (yadi 10) kutoka ulipo mpira mpaka pale mchezo utakapokuwa umeanza
Mpira lazima uwe katikati ya uwanja na ukiwa umetulia
Mwamuzi atatoa ishara ya kuanza kwa mchezo
Mpira utakuwa tayari kuchezwa ikiwa utapigwa na kuanza kutembea
Mchezaji alieanzisha mchezo hatakiwi kuugusa tena mpira ule mpaka pale utakapokuwa umeguswa na mchezaji mwingine
Ukiukaji wa sheria hii
Ikiwa kama mchezaji anayeanzisha mchezo ataugusa tena mpira kabla haujaguswa na mchezaji mwingine:
Mpira wa adhabu ndogo utapigwa dhidi ya timu ya mchezaji huyo
Ikiwa kama kutatokea ukiukwaji mwingine tofauti:
Mwamuzi ataamuru mchezo uanzishwe tena
Kudundisha mpira :- ni namna ya mwamuzi kuanzisha mchezo upya na hii itatokea wakati mchezo ukiwa unaendelea na mwamuzi atalazimika kusimamisha mchezo kwa sababu yoyote ambayo hata isiyo andikwa kwenye sharia 17 za soka.
Utaratibu wa kudundisha mpira
Mwamuzi ataudundisha mpira pahala ulipokuwa wakati akisimamisha mchezo isipokuwa tu kama mchezo ulisimama mpira ukiwa eneo la goli ambapo katika hali kama hii mwamuzi ataudundisha mpira katika mstari uliosambamba na mstari wa goli pahala ulipokuwa mpira kipindi mwamuzi anasimamisha mchezo. Mpira utakuwa tayari kuchezwa pale tu utakapogusa chini.
Mwamuzi atadundisha mpira tena:
Kama utaguswa na mchezaji kabla haujagusa chini
Kama mpira utatoka baada ya kugusa chini
Kama mpira wa kudundisha utatinga nyavuni?
Kama mpira wa kundundisha utapigwa na kuingia nyavuni kwa goli la timu pinzani, mpira wa goal kiki utapigwa
Kama mpira wa kudundisha utaingia nyavuni na kuzaa goli la kujifunga, timu pinzani watapewa kona.
+++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
SHERIA NAMNA 9: MPIRA UMETOKA AU HAUJATOKA?
MPIRA UMETOKA NJE
Mpira utakuwa umetoka nje ya dimba ikiwa:
Mpira wote utakuwa umevuka mstari wa goli au mstari wa pembeni iwe ni ikiwa upo chini au hewani. ‘wote’ maana yeka kusiwe na sehemu ya mpira inabaki juu ya mstari.
Mwamuzi atakuwa amesimamisha mchezo (kumbuka wakati wa mapumziko na baada ya mechi mwamuzi hubeba mpira na kuondoka nao)
MPIRA HAUJATOKA NJE
Mpira utakuwa ndani ya dimba muda wote ikiwa ni pamoja na:
Utakapogonga mlingoti wa goli au mtambaa-panya au mlingoti wa kibendera cha kona na kurudi dimbani
Utakapomgonga mwamuzi wa kati au msaidizi wake lakini sharti wawe dimbani
+++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
SHERIA NAMBA 10: NAMNA YA KUFUNGA GOLI
NI GOLI AU SIYO GOLI?
Itahesabika kuwa limefungwa goli ikiwa mpira wote utavuka mstari wa goli ulio kati ya milingoti miwili ya goli na chini ya mtambaa-panya. Hata hivyo timu inayofunga goli isiwe imekiuka kanuni wakati wa harakati za kufunga hilo goli.
NANI KASHINDA?
Timu itakayofunga magoli mengi kuliko mwenzake wakati wa mchezo itatangazwa mshindi wa mchezo husika. Ikiwa kama timu zinazopambana zitafunga idadi sawa ya magoli au ikiwa kama hakutakuwa kumefungwa goli lolote, mchezo utaamuliwa kuwa sare au suluhu.
KANUNI ZA MASHINDANO
Ikiwa kama kanuni za mashindano zinataka lazima apatikane mshindi baada ya mpambano au baada ya mechi za nyumbani na ugenini, utaratibu pekee unaokubalika kumpata mshindi ni:
Goli la ugenini
Muda wa nyongeza
Mikwaju ya penati
TEKNOLOJIA YA GOLI
Teknolojia ya goli au kwa kimombo goal-line technology (GLT) inaweza kutumika kwa kusudi la kuthibitisha ikiwa kama goli limefungwa au laa. Kutumika au kutokutumika kwa GLT lazima kuwe kumebainishwa katika kanuni za mashindano husika.
+++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
SHERIA NAMBA 11: KUOTEA
Angalizo: siyo kosa kisheria kwa mchezaji kuotea. Kwa hiyo mchezaji hatapewa kadi ya njano wala nyekundu eti kisa kaotea. Wala hataonywa kwa maneno na mwamuzi. Yeye aotee tu anavyotaka hata mara mia atajujuwa mwenyewe.
Hata hivyo mchezaji atakuwa ameotea ikiwa:
Atakuwa karibu na mstari wa goli la timu pinzani kuliko mpira wenyewe na mlinzi wa mwisho
Mchezaji atahesabika hakuotea ikiwa:
Atakuwa upande wa nusu ya uwanja inayohusu timu yake
Atakuwa katika mstari sambamba na mlinzi wa mwisho wa timu pinzani
Atakuwa sambamba na walinzi wawili wa mwisho wa timu pinzani
Makosa
Mwamuzi atapuliza kipyenga cha kuotea ikiwa mchezaji anayedhani kuwa yupo katika nafasi ya kuotea ataingilia mchezo. Mfano mchezaji amezidi/ameotea halafu mara ghafla anarudi ndani haraka-haraka kutaka kupokea pasi hapo mwamuzi lazima apulize kipyenga cha kuashiria kuwa mchezaji huyo ameotea.
Hakuna Makosa
Ikiwa mchezaji aliye katika nafasi ya kuotea atapokea mpira wa goal-kick
Ikiwa mchezaji aliya katika nafasi ya kuotea atapokea mpira wa kurusha
Ikiwa mchezaji aliye katika nafasi ya kuotea atapokea mpira wa kona
Ukiukwaji wa sharia hii na adhabu zake
Pale itakapotokea kuwa mchezaji ameotea, mwamuzi ataamuru upigwe mpira wa adhabu ndogo dhidi ya timu pinzani.
++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
SHERIA NAMBA 12: MAKOSA MBALI MBALI NA UTOVU WA NIDHAMU
Itakapotokea mchezaji anafanya makosa au utovu wa nidhamu hatua zifuatazo zitachukuliwa:
Mpira wa Adhabu wa Moja kwa Moja :- adhabu hii itatolewa dhidi ya timu pinzani ikiwa kama mchezaji wao atafanya moja kati ya makosa yafuatayo:
Atamkanyaga makusudi au atadhamiria kumkanyaga makusudi mchezaji wa timu pinzani
Atamkwatua au kudhamiria kumkwatua mchezaji wa timu pinzani
Atamrukia mchezaji wa timu pinzani
Atampamia makusudi mchezaji wa timu pinzani
Atampiga au atadhamiria kumpiga mchezaji wa timu pinzani (mfano kupiga kiwiko)
Atamsukuma mchezaji wa timu pinzani
Atakaba vibaya badala ya kucheza mpira ataukosa na kumuumiza mcheza ji wa timu pinzani (tackling)
Vilevile, mpira wa adhabu wa moja kwa moja utaamuriwa upigwe ikiwa yafuatayo yatatendeka:
Mchezaji atamkamata makusudi mchezaji wa timu pinzani
Mchezaji atamtemea mate mchezaji wa timu pinzani
Ataushika mpira makusudi ndani ya eneo la penati (isipokuwa kwa mlindamlango tu)
Penati
Mpira wa penati utapigwa ikiwa lolote kati ya makosa 10 yaliyobainishwa hapo juu yatafanyika na mchezaji ndani ya eneo la penati la timu yake, bila kujali eneo kosa limefanyikia, cha muhimu tu iwe ndani ya eneo la penati la maguu 18.
Mpira wa adhabu ndogo
Mpira wa adhabu ndogo utapigwa dhidi ya timu pinzani ikiwa mlindamlango ndani ya eneo lake la kujidai atafanya lolote kati ya haya yafuatayo:
Atakaa na mpira kwa zaidi ya sekunde 6 bila kuuachia au kuupiga ili mchezo uendelee
Ataudaka mpira. Atauachia. Lakini kabla haujaguswa na mchezaji mwingine ataudaka tena.
Atadaka mpira wa kurusha uliorushwa kwake moja kwa moja na mchezaji wa timu yake
Mwamuzi pia ataamuru upigwe mpira wa adhabu ndogo ikiwa kwa maoni yake atahisi mchezaji:
Amecheza mchezo wa hatari
Amemzuia mchezaji wa timu pinzani kuambaa na mpira
Atamzuia mlindamlango asipige au kuuachia mpira aliodaka
Atafanya lolote tofauti na yaliyotajwa hapo awali ambapo katika hali kama hiyo mwamuzi atasimamisha mchezo na kutoa kadi ya njano au nyekundu kwa muhusika
Hatua za kinidhamu
Kadi ya manjano itatumika kuashiria kuwa mchezaji ameonywa
Kadi nyekundu itatumika kuashiria kuwa mchezaji ametolewa nje.
Anayestahili kupewa kadi ya manjano au nyekundu ni mchezaji tu awe uwanjani au nje ya uwanja
Mwamuzi ana mamlaka ya kutoa adhabu dhidi ya mchezaji kuanzia mchezo unapoanza mpaka unapokamilika
Mchezaji atakaetenda kosa la kustahili kadi ya manjano au nyekundu iwe yupo uwanjani au nje, iwe ni dhidi ya mchezaji wa timu pinzani au mchezaji wa timu yake au mwamuzi au mwamuzi msaidizi ataadhibiwa kutokana na aina ya kosa.
Makosa yanayostahili kadi ya manjano
Tabia zisizo za kiwanamichezo
Utovu wa nidhamu kwa maneno au kwa vitendo
Kukiuka sheria mara kwa mara
Kuchelewesha kuanzisha mchezo makusudi
Kutokutii kukaa umbali unaokubalika wakati wa kupigwa kwa kona, mpira wa adhabu au mpira wa kurusha
Kuingia uwanjani bila ruksa ya mwamuzi
Kutoka uwanjani makusudi bila ruksa ya mwamuzi
Mchezaji aliye katika benchi la ufundi atapewa kadi ya manjano ikiwa:
Ataonesha vitendo visivyo vya kiwanamichezo
Ataonesha utovu wa nishamu kwa maneno au kwa vitendo
Atachelewesha kuanzisha mchezo kwa makusudi
Kadi nyekundu
Mchezaji ataoneshwa kadi nyekundu na kutolewa nje ya uwanja ikiwa atafanya makosa yafuatayo:
Kucheza faulo ya hatari
Kufanya kitendo cha vurugu
Kumtemea mate mchezaji wa timu pinzani au mtu yeyote
Kuzuia timu pinzani wasipate goli kwa kushika mpira makusudi ndani ya eneo la penati (hii lakini haihusiani na mlindamlango akishika mpira ndani ya eneo lake la kujidai)
Kuzuia timu pinzaniw asipate goli la dhahir shahir kwa kumcheza rafu mchezaji anayeambaa kwenda kufunga
Kutumia lugha ya matusi, kashfa au kuonesha ishara mbaya
Kupewa kadi ya pili ya njano katika mchezo huohuo.
Mchezaji aliyepewa kadi nyekundu hatakiwi kuonekana eneo la karibu na dimba na wala asikae katika benchi la ufundi la timu yake.
+++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
Sheria Namba 13: Mpira wa Adhabu
Aina za mpira wa adhabu. Ziko mbili:
Mpira wa adhabu wa moja kwa moja
Mpira wa adhabu ndogo
Mpira wa adhabu wa moja kwa moja:
Ukipigwa na kuzama moja kwa moja golini kwa timu pinzani, goli litahesabika
Ukipigwa na kuzama katika goli la timu inayopiga huo mpira, refa ataamuru kona
Mpira wa adhabu ndogo:
Ishara:-mwamuzi ataashiria adhabu ya mpira wa adhabu ndogo kwa kunyanyua mkono wake juu na ataendelea kuuacha mkono wake wima mpaka pale adhabu itakapochezwa na kwamba baada ya kuwa umepigwa mpira lazima umguse mchezaji mwingine au utoke nje.
Kufunga goli kwa mpira wa adhabu ndogo:
Goli la mpira wa adhabu ndogo litahesabika tu ikiwa baada ya mpira kuwa umepigwa, utamgusa mchezaji mwingine ndiyo uingie golini. Kinyume na hapo:
Kama mpira wa adhabu ndogo utapigwa moja kwa moja na kutinga nyavuni bila kuguswa na mtu yeyote mwamuzi ataamuru goal kiki.
Kama mpira wa adhabu ndogo utapigwa moja kwa moja na kuzaa goli la kujifunga, mwamuzi ataamuru kona.
Kuhusu utaratibu:
Kwa adhabu zote mbili mpira utatakiwa kutulia kwanza kabla ya kupigwa na kwamba mpigaji hatakiwi kuugusa tena mpira ule mpaka uwe umeguswa na mchezaji mwingine.
Pahala pa kupigia mpira wa adhabu:
Kwa mpira wa adhabu ndani ya eneo la penati dhidi ya timu inayoshambulia(hii ni kwa adhabu za aina zote moja kwa moja na adhabu ndogo):
Wachezaji wa timu inayoshambulia watakaa umbali wa yadi 10 kutoka ulipo mpira
Wachezaji wa timu inayoshambulia watakaa nje ya eneo la penati mpaka pale mpira utakapopigwa
Wachezaji wa timu inayoshambulia wataruhusiwa kuucheza mpira pale utakapokuwa umetoka nje ya eneo la penati.
Kama kutafanyika madhambi ndani ya eneo la goli – maguu 12, mpira utatengwa popote
Mpira wa adhabu ndogo dhidi ya timu inayoshambuliwa:
Wachezaji wa timu inayoshambuliwa watakaa umbali wa yadi 10 kutoka ulipotengwa mpira mpaka pale utakapochezwa isipokuwa tu kama watakuwa wamejipanga kwenye mstari wa goli.
Mpira utakuwa tayari kuchezwa pale utakapopigwa na kuanza kutembea
Ikitokea adhabu inaamuliwa ndani ya eneo la goli, mpira utatengwa juu ya mstari ulio sambamba na mstari wa goli.
Ukiukwaji wa sheria hii na adhabu zake:
Kama wakati wa kupiga mpira wa adhabu, mchezaji wa timu pinzani atakaa karibu kuliko vile inavyotakiwa kisheria, muamuzi ataamuru adhabu ipigwe tena.
Kama mpira wa adhabu utapigwa na timu iliyokuwa inashambuliwa kutoka eneo lao la penati ukawa haujatoka nje ya eneo la penati, muamuzi ataamuru adhabu ipigwe tena.
Mpira wa adhabu unaopigwa na mchezaji mwingine tofauti na golikipa:
Kama baada ya kuwa adhabu imepigwa na kisha mchezaji yuleyule aliyepiga adhabu akaugusa tena kabla haujaguswa na mchezaji mwingine, mwamuzi ataamuru upigwe mpira wa adhabu ndogo.
Kama baada ya kuwa adhabu imepigwa na kisha mchezaji yuleyule aliyepiga adhabu akaugusa kwa mkono kabla haujaguswa na mchezaji mwingine:
muamuzi ataamuru mpira wa adhabu wa moja kwa moja
muamuzi ataamuru penati ikiwa makosa haya yatafanyika ndani ya eneo na penati
Mpira wa adhabu unaopigwa na golikipa
Kama baada ya kuwa adhabu imepigwa na kisha golikipa yuleyule aliyepiga adhabu akaugusa tena (siyo na mikono) kabla haujaguswa na mchezaji mwingine muamuzi ataamuru mpira wa adhabu ndogo.
Kama baada ya kuwa adhabu imepigwa na kisha golikipa yuleyule aliyepiga adhabu akaugusa tena na mikono kabla haujaguswa na mchezaji mwingine:
Muamuzi ataamuru ipigwe adhabu ya mpira wa adhabu wa moja kwa moja kama golikipa ameushika mpira nje ya eneo la penati.
Muamuzi ataamuru mpira wa adhabu ndogo ikiwa golikipa kaushika tena mpira ule ndani ya eneo la penati.
++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
Sheris Namba 14: Tuta
Tunaijadili sasa Sheria Namba 14. Lakini kabla ya kuendelea zaidi tukumbushane tena makosa 10 yanayoweza kusababisha mchezaji alimwe kadi ya njano:
1. Kumpiga mchezaji wa timu pinzani
2. Kumpamia kwa makusudi mchezaji wa timu pinzani
3. Kumsukuma mchezaji wa timu pinzani
4. Kumkwatua mchezaji wa timu pinzani
5. Kumrukia mchezaji wa timu pinzani
6. Kupiga tackle na kuukosa mpira na badala yake ukampata mpinzani
7. Kumvuta jezi au kumkamata mchezaji wa timu pinzani
8. Kumtemea mate mchezaji wa timu pinzani
9. Kumkanyaga mchezaji wa timu pinzani
10. Kuunawa mpira kwa makusudi.
Makosa hayo 10 hapo juu yakifanyika ndani ya box la maguu 18 ya timu yako mwamuzi ataamuru upigwe mkwaju wa penati.
Penati lazima ipigwe - haijalishi iwe ni mwisho wa dakika 45 za kwanza au za pili, au dakika za nyongeza. Tuta kama zege. Halilali.
Mpira utatengwa kwenye kiduara cha kupigia tuta na kwamba mpigaji lazima atambuliwe vema na mwamuzi na kwamba golikipa atasimama juu ya mstati wa goli katikati ya milingoti akitizamana uso kwa uso na mpigaji wa tuta.
Ukiacha mpigaji wa tuta, wachezaji wengine wote watasimama nje ya eneo la penati kiasi cha yadi 10 hivi kutoka kilipo kiduara panapotengwa mpira wa tuta.
Ikiwa kila kitu kipo sawia, muamuzi ataamuru tuta lipigwe. Mpigaji lazima aupige mpira uende mbele na kwamba hataruhusiwa kuucheza tena mpaka pale utakapokuwa umeguswa na mchezaji mwingine.
KASORO
Ikiwa mpigaji wa tuta (au mchezaji mwenza wa mpigaji tuta) atakiuka baadhi ya sharia za soka wakati wa kupiga tuta na goli likaingia muamuzi ataamuru tuta lipigwe tena. Kama mpiga tuta atakosa kufunga goli, muamuzi ataamuru adhabu ndogo dhidi ya timu ya mpigaji.
Ikiwa golikipa (au mchezaji mwenza wa golikipa) anayepigiwa tuta atakiuka baadhi ya sharia za soka wakati wa upigaji wa tuta na goli likaingia, goli hilo litasimama lakini kama mpigaji atakosa, muamuzi ataamuru tuta lipigwe tena.
Na ikiwa baada ya tuta kupigwa…
Mpigaji akaugusa (isipokuwa kwa mikono) tena mpira, muamuzi ataamuru mpira wa adhabu ndogo dhidi ya timu ya mpigaji.
Ikiwa mpigaji tuta ataushika kwa makusudi mpira kabla ya kuguswa na mpigaji mwingine muamuzi ataamuru adhabu ya mpira wa moja kwa moja.
Ikiwa mpira utagusa kitu kingine chochote tofauti na mchezaji, muamuzi ataamuru tuta lipigwe tena.
Ikiwa mpira utarudi dimbani baada ya kupanguliwa na kipa au ukagonga nguzo za goli na kurejea dimbani na kisha ukagongana na kitu kingine chochote tofauti na mchezaji, muamuzi atasimamisha mchezo kisha ataundundisha na mchezo kuendelea.
insha-allah, panapo majaaliwa tutaendelea...
MTEULE THE BEST Image caption Waziri wa maswala ya kigeni nchini Urusi Sergei Lavrov na mwenzeka wa Marekani Rex Tillerson Waziri wa maswala ya kigeni nchini Urusi Segei Lavrov amemwambia waziri wa ulinzi nchini Marekani Rex Tillerson kwamba kuiwekea vikwazo zaidi Korea Kaskazini hakutafua dafu. Taarifa iliochapishwa na wizara ya kigeni nchini Urusi inasema kuwa wawili hao walizungumza kwa njia ya simu na kushutumu majaribio ya makombora ya hivi karibuni yaliotekelezwa na Pyongyang . Lakini inasema kuwa bwana Lavrov alisisitiza kwamba diplomasia ndio njia ya pekee ya kumaliza wasiwasi katika rasi ya Korea, na kutaka hatua zozote dhidi ya taifa hilo kusitishwa akionya huenda zikasababisha madhara yasiojulikana. Waziri wa ulinzi nchini Marekani amesisitiza kuwa bado kuna fursa ya kidiplomasia katika kukabiliana na Korea Kaskazini. Mapema rais Trump alichapisha ujumbe katika akaunti yake ya Twitter akisema mazungumzo sio suluhisho.
Maoni