Rais wa Tanzania Dkt John Magufuli Jumapili aliongoza taifa hilo kupokea ndege mpya ya kisasa ambayo imenunuliwa kwa ajili ya kutumiwa na shirika la ndege la taifa hilo.
Ndege hiyo mpya aina ya Boeing 787-8 Dreamliner ilinunuliwa na Serikali ya Tanzania kwa ajili ya kuliimarisha Shirika la Ndege la Taifa (ATCL).
Bei ya ndege hiyo inakadiriwa kuwa $224.6 milioni (Sh512 bilioni za Tanzania) kwa mujibu wa taarifa kwenye tovuti ya kampuni ya Boeing.
Ndege hiyo iliwasili majira ya saa 11:10 jioni katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, kisha kupewa heshima ya kumwagiwa maji na baadaye Rais Magufuli akiwa na viongozi wakuu walioambatana naye akaizindua rasmi.
Aidha, yeye na Makamu wake Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa, waliikagua kwa kuingia ndani ya ndege ili kujionea mandhari ya ndani.
Mataifa ya Afrika yaliyo na Dreamliner
Ethiopia (Ethiopian Airlines )*- 19
Kenya (Kenya Airways) - 8
Morocco (Royal Air Maroc) - 5
*Ethiopia pia wana Boeing B787-9 tatu, ambayo ni ndege kubwa kuliko 787-8 na inaweza kuwabeba abiria 290
Akizungumza kabla ya kuwasili kwa ndege hiyo Rais Magufuli alikuwa amewapongeza Watanzania kwa kuchapa kazi na kulipa kodi.
Rais Magufuli akiwa ndani ya ndege hiyo
Alisema hilo liliiwezesha Serikali kupata fedha za kutekelezea miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ununuzi wa ndege kwa ajili ya kuimarisha ATCL ambayo ilikuwa na hali mbaya.
Hapa, ni mkusanyiko wa nukuu muhimu kutoka kwa hotuba yake, ambapo alizungumzia pia ukosoaji unaoelekezwa kwa mpango wake wa kuangazia kununua ndege.
Rais Magufuli akifurahia jambo na Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania Inmi Petterson
Ndege hiyo imepewa jina 'Kilimanjaro-Hapa kazi tu'.
1.Mradi utakuwa wa faida kwa Air Tanzania
"Shirika letu la ndege lilikuwa na hali mbaya sana, lilikuwa na ndege moja tu tena ilikuwa inafanyiwa matengenezo mara kwa mara, soko la ATCL lilishuka sana hadi kufikia asilimia 2.5, lakini sasa tumenunua ndege 7, hii ni ndege ya 4 na nyingine mbili zitakuja kabla ya mwaka huu kuisha, na nyingine kubwa aina ya Boeing 787-8 Dreamliner itakuja mwaka 2020.
"Tangu tumeongeza ndege 3 mpya aina ya Bombardier Q400 biashara ya ATCL imeongezeka, Shirika letu lilikuwa linasafirisha abiria 4,000 tu kwa mwezi lakini sasa linasafirisha abiria 21,000 na ndege zinatua katika vituo 12."
2. Ndege itaifaa Tanzania kiuchumi
Rais Magufuli anaamini ununuzi wa ndege hiyo utachangia kuimarisha uchumi wa Tanzania, kwa pamoja na miradi mingine mikubwa inayotekelezwa na serikali.
Alisema: "Tumeleta ndege hizi pia ili ziimarishe na kuongeza mapato yetu ya utalii nchini. Asilimia 70 ya watalii wanatumia ndege."
"Tunaboresha usafiri wa reli, majini na barabara. Waliodhani kuwa maboresho ya Bandari hayana tija sasa wameaibika."
3.Ndege zitaijengea Tanzania heshima na hadhi
Rais Magufuli alibainisha kuwa Serikali iliamua kuchukua hatua ya kulinusuru Shirika la Ndege la Taifa ili kujenga heshima na kulinda hadhi ya Taifa, kuimarisha na kuboresha huduma za usafiri wa anga na kukuza utalii.
"Tumefufua ATCL kurejesha heshima ya nchi, ilikuwa aibu kutokuwa na ndege kwa nchi kubwa kama Tanzania," alisema.
4. Wasiofurahia watapata 'taabu sana'
Rais Magufuli pia aliwasuta waliokuwa wanadai kwamba ndege hiyo ni ya gharama ya juu na haitaifaa Tanzania. Alisema ndege hizo zimenunuliwa kwa kutumia kodi na kwamba si kwa kupitia mkopo.
"Ndege zote hizi tumenunua kwa fedha zetu wenyewe, hatujakopa kwa mtu. Ndege hizi ni matokeo ya Watanzania kulipa kodi na kuchapakazi. Nawapongeza wote walioshiriki kikamilifu," alisema.
"Madai kuwa Watanzania wengi hawafaidiki na ndege hayana msingi. Wapo wengi wanaohitaji ndege bei ilikuwa juu."
"Ndege hii imewafurahisha wengi na kama yupo mtu hajafurahia tukio hili basi huyo atapata taabu sana!
5. Hela tunazo
Rais Magufuli alionekana kusisitiza kwamba ndege hizo hazijanunuliwa kwa mkopo na kwamba Tanzania 'ina hela'.
Kaimu waziri wa Marekani nchini humo alihudhuria sherehe hiyo uwanja wa kimataifa wa ndege wa Julius Nyerere Dar es Salaam na Rais Magufulia likuwa na ujumbe kwake.
"Tunataka Balozi wa Marekani utufikishie salam Boeing kuwa ile Dreamliner ya pili waikamilishe haraka, hela tunazo," alisema.
Tanzania inatarajia kupokea 2 aina ya Bombardier Novemba mwaka huu na Januari 2020 wapokee ndege hiyo nyingine aina ya Dreamliner. Ndege za Bombardier huwa zina uwezo wa kuwabeba abiria 132.
Kuanza safari nje ya nchi
Katibu Mkuu Uchukuzi Dkt Leonard Chamriho alisema ndege hiyo yenye uwezo wa kuchukua abiria 262, itaanza kutoa huduma kwa safari za ndani katika vituo vya Dar es Salaam, Kilimanjaro na Mwanza.
Mwezi Septemba itaanza safari zake kwenda Bombay nchini India, Guangzhou nchini China na Bangkok nchini Thailand.
Dkt Chamriho alisema kwamba utaratibu umeanza ili ifanye safari za kwenda Uingereza na miji mingine duniani.
Kando na ndege hizo mbili za Dreamliner ambazo Tanzania inanunua, taifa hilo pia linanunua ndege aina ya Bombardier Q400 ambapo tatu tayari zimepokelewa na zinafanya kazi.
Ndege hizo zinahudumu kati ya Dar es Salaam ,Visiwa vya Comoros, Mwanza, Kigoma na Mtwara.
Boeing 787-8 Dreamliner ni ndege ya aina gani?
Ndege hiyo ya Tanzania ilisafiri kutoka uwanja wa Paine mjini Seattle, Washington safari ya umbali wa saa 22.
Boeing 787-8 Dreamliner ni ndege ya kisasa ambayo hutumia injini ya kisasa zaidi aina ya Trent 1000 TEN. Bei yake inakadiriwa kuwa $224.6 milioni.
Injini hiyo inatumiwa katika ndege zote mpya aina ya Boeing 787 na huhifadhi mafuta, ambapo huwa inachoma mafuta kwa kiwango cha asilimia tatu chini ukilinganisha na ndege za aina hiyo na kuyatumia vyema zaidi.
Hilo huiwezesha kupunguza matumizi ya mafuta ukilinganisha na ndege nyingine za ukubwa kama wake kwa asilimia 20-25, aidha hupunguza utoaji wa gesi chafu kwa kiwango sawa na hicho.
Aidha, huwa haipigi kelele sana. Ni ndege ambayo imechukua uwezo na kasi ya ndege kubwa aina ya 'jet' na kuuweka kwenye ndege ya ukubwa wa wastani.
Ina uwezo wa kubeba abiria 262 ni ya kisasa zaidi kuwahi kumilikiwa na serikali ya Tanzania. Mataifa mengine kama vile Kenya na Ethiopia hata hivyo yamenunua ndege kama hizo kadha.
Ndege hii ina uwezo wa kusafiri kiilomita 13,620 kwa wakati mmoja na urefu wake ni mita 57. Upana wa mabawa yake ni mita 60. Urefu wake kutoka chini hadi juu ni mita 17.
Rais Magufuli aligusia hilo aliposema: "Ndege hii ni ya kisasa na kote walikopita walikuwa wana uwezo wa kunipigia simu na kuongea nao angani."
Ethiopia ilikuwa nchi ya kwanza duniani kando na Japan kuanza kutumia ndege aina ya Boeing 787-8 Agosti
Maoni