Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na mwenzake wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni wameahidi kuimarisha ushirikiano kati ya nchi zao mbili. Wawili hao wamewaagiza Mawaziri wa nchi hizi mbili kujadiliana juu ya namna ya kuongeza biashara kati ya nchi hizo ili kupata manufaa makubwa zaidi ya uhusiano na ushirikiano uliopo. Dkt Magufuli na Bw Museveni walitoa agizo hilo baada ya kufanya mazungumzo rasmi katika Ikulu ndogo ya Masaka nchini Uganda ambako Rais Magufuli ameendelea na ziara yake rasmi ya kiserikali ya siku tatu. Rais Magufuli amesema kwa muda mrefu biashara kati ya Tanzania na Uganda imekuwa ni takribani shilingi Bilioni 200 kwa mwaka kiasi ambacho ni kidogo mno ikilinganishwa na fursa zilizopo, uhusiano na ushirikiano wa kidugu uliojengwa tangu enzi za Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. "Tumewaagiza Mawaziri na wataalamu wakae na waangalie vikwazo vyote vinavyosababisha tufanye biashara kwa kiasi kidogo, wakishajadili watatuambia tufanye nini, tunataka kuona bias...