Mkutano mdogo wa kilele ambao ulioandaliwa Brussels kujadili sera ya uhamiaji na uliofanyika kwa ombi la Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, ambaye alikuwa kwenye shinikizo nchini mwake, haukutoa maamuzi yoyote. Lakini hotuba za viongozi wa nchi 16 waliohudhuria zinaashiria safari inakoelekea. Swali ni iwapo hatua zilizopangwa kuchukuliwa zitamsaidia Merkel katika mzozo na Waziri wake wa mambo ya ndani Horst Seehofer au iwapo mwanasiasa huyo wa chama cha Christian Social Union, CSU, atanufaika zaidi. Seehofer anasisitiza suluhisho la muda mfupi la wanaotafuta hifadhi kukataliwa kuingia Ujerumani wanapofika mpakani. Angela Merkel naye matumaini yake ya suluhisho ni maafikiano yatakayotokana na mazungumzo baina ya nchi kuhusu suala la kuwarudisha wahamiaji hao walikotoka. Mkutano huo wa Brussels ulitoa mapendekezo kadhaa na je mapendekezo haya yatakuwa na athari gani kwa siasa za ndani za Ujerumani? Baadhi ya nchi zinataka kubuniwe vituo vya mapokezi ya wakimbizi Libya ...