Mrundi wa Stand United aliyewapiga Yanga hat trick kwenye Uwanja wa Taifa, Alex Kitenge amekiri kwamba hali yake ni ngumu na anakiona chamoto. Lakini habari ya kushtua ni kwamba tangu awapige Yanga kwenye mechi iliyomalizika kwa ushindi wa mabao 4-3 Jangwani, hajatumbukiza tena nyavuni mpaka leo. Kacheza michezo minne bila kufunga hata bao la kuotea kati ya sita waliyocheza Stand. “Mabeki wengi wamekuwa hawanipi nafasi ya kukaa na mpira nafikiri hii inatokana na kuwafunga Yanga mabao matatu, na kipindi nakuja nilikuwa mgeni wengi walikuwa hawanijui lakini sasa wameshaujua ubora wangu, ila nitajitahidi nirudi kwenye mbio za kuwania ufungaji bora kwa sababu hakuna ligi ambayo nimecheza nikakosa kuwa katika tatu bora ya ufungaji bora,’’ alisema Kitenge