Serikali imesema itaanzisha madawati ya jinsia katika shule za msingi na sekondari, ili wanafunzi waripoti matukio ya kikatili wanayofanyiwa na wazazi na jamii inayowazunguka.
Lengo la hatua hiyo ni kuendelea kupunguza vitendo hivyo vinayoendelea kushamiri nchini.
Mkakati huo, ulitangazwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, wakati akifungua mdahalo wa wahariri wa vyombo vya habari kuhusu ukeketaji, ndoa na mimba za utotoni katika kuelekea Siku ya Mtoto wa Kike Oktoba 11, jana jijini Dar es Salaam.
Dk. Ndugulile alisema sababu ya kuanzisha madawati hayo katika shule ni baada ya kubaini wanaofanya vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa watoto chini ya miaka 18 ni wazazi, walezi, ndugu wa karibu na majirani.
āMatukio ya ukatili wa kijinsia yanaendelea kushamiri ndani ya jamii kwa sababu wanaohusika wapo ndani ya familia. Hivyo hayaripotiwi kwenye vyombo vya sheria na badala yake familia zinamalizana nyumbani tu kwa kupeana vitu kama ng'ombe, fedha na mali nyingine,ā alisema na kuongeza:
āSerikali sasa kwa kushirikiana na maofisa elimu, tumeanzisha madawati ya jinsia kwenye shule ili wanafunzi waweze kuripoti matukio haya wanayofanyiwa kwa walimu wao ambao watakuwa wamepewa mafunzo maalum."
Pia serikali itaboresha madawati ya jinsia zaidi ya 500 yaliyopo katika vituo vya polisi nchini, ili matukio ya kikatili ya kijinsia kwa watoto yanayoripotiwa yapewe kipaumbele ili hatua za kisheria zichukuliwe haraka.
Dk. Ndugulile alisema kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike inayoadhimishwa Oktoba 11 kila mwaka inasema āImarisha uwezo wa mtoto wa kike; tokomeza ukeketaji, mimba na ndoa za utotoniā ina lengo kuhamasisha jamii kushirikiana na serikali kumaliza matukio hayo ndani ya jamii.
Alifafanua kauli mbiu hiyo inahamasisha jamii kushirikiana na serikali kupinga na kukemea vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto walio chini ya miaka 18.
Alisema kwa mujibu wa takwimu za Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS), katika kipindi cha mwaka 2017 matukio 41,000 ya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto yaliripotiwa na kati ya hayo ya watoto peke yake yalikuwa 13,000.
Alisema sababu za kuendelea kushamiri kwa matukio hayo ni mila na desturi potofu na umaskini unaochochea watoto wa kike kuolewa chini ya miaka 18.
Alitaja madhara wanayopata ni ukatili wa kingono, mimba za utotoni, kukatisha ndoto zao na maambukizi ya magonjwa kama Ukimwi.
Alisema mpango wa serikali ni kuhakikisha wanapunguza matukio hayo hadi kufikia asilimia 50 ifikapo mwaka 2022.
Dk. Ndugulile alisema njia watakazotumia kupunguza matukio hayo ni kukusanya takwimu, kuyasemea na kuyatolea taarifa matukio hayo yanayoripotiwa katika madawati ya jinsia.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), Davis Lumala, alisema katika kuhakikisha wanakabiliana na changamoto za ukeketaji, mimba na ndoa za utotoni wamekuwa wakitoa elimu katika shule mbalimbali.
Pia wameanzisha kampeni ya kupinga na kuzuia matukio ya ukatili wa kijinsia katika wilaya saba za Tanzania Bara na tatu za visiwani Zanzibar
Maoni