Shuleni kuanzishwa Madawati ya Jinsia Serikali imesema itaanzisha madawati ya jinsia katika shule za msingi na sekondari , ili wanafunzi waripoti matukio ya kikatili wanayofanyiwa na wazazi na jamii inayowazunguka. Lengo la hatua hiyo ni kuendelea kupunguza vitendo hivyo vinayoendelea kushamiri nchini. Mkakati huo, ulitangazwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, wakati akifungua mdahalo wa wahariri wa vyombo vya habari kuhusu ukeketaji, ndoa na mimba za utotoni katika kuelekea Siku ya Mtoto wa Kike Oktoba 11, jana jijini Dar es Salaam. Dk. Ndugulile alisema sababu ya kuanzisha madawati hayo katika shule ni baada ya kubaini wanaofanya vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa watoto chini ya miaka 18 ni wazazi, walezi, ndugu wa karibu na majirani. “Matukio ya ukatili wa kijinsia yanaendelea kushamiri ndani ya jamii kwa sababu wanaohusika wapo ndani ya familia. Hivyo hayaripotiwi kwenye vyombo...