Serikali ya Marekani imezitaka nchi nyingine kuongeza shinikizo kwa Iran kutokana na kuhusika kwake katika mzozo wa Mashariki ya Kati. Taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Marekani imelikosoa Jeshi la Mapinduzi la Iran, kutokana na vitendo vyake vya kuchangia katika kusababisha ushawishi wa kukosekana kwa amani na utulivu katika Mashariki ya Kati, licha ya watu wa Iran kuwa waathirika wa uchumi unaosuasua. Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Sarah Huckabee Sanders amevitolea mfano vitendo hivyo vya Iran ambavyo inavifanya katika nchi za Syria na Saudi Arabia na ameyataka mataifa mengine duniani kuishinikiza Iran kuachana na tabia yake hatari. Taarifa hiyo ya Marekani imevikosoa vikosi hivyo kwa kurusha makombora dhidi ya Israel katika milima ya Golan mwanzoni mwa juma hili, hali iliyosababisha Israel kujibu pia kwa mashambulizi siku ya Alhamisi dhidi ya vikosi vya Iran. Hali hiyo imezusha hofu ya kuzuka kwa mzozo katika ukanda huo na hivyo kuhatarisha amani na usalama wa Mashariki ya Kati...