Nchi za Ulaya ambazo zilihusika katika kujadili na kusaini makubaliano hayo ya mwaka 2015 kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran zinafanya kila juhudi kuyanusuru makubaliano hayo, ambayo yanakabiliwa na kitisho kikubwa kutoka na hatua ya Rais Donald Trump ya kuindoa Marekani hapo jana. Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anatarajiwa kufanya mazungumzo ya simu na mwenzake wa Iran Hassan Rouhani, kumuhakikishia kwamba Umoja wa Ulaya utafanya uwezavyo kuendeleza ahueni ya kiuchumi ambayo Iran iliahidiwa ili ipunguze upeo wa mpango wake wa nyuklia.
Tangazo la pamoja lililotolewa na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron muda mfupi baada ya Rais Trump kubainisha uamuzi wake, viongozi hao wa Ulaya wamesema wamesikitishwa na hatua hiyo ya Marekani.
Akizungumza na kituo kimoja cha redio cha Ufaransa, waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Jean-Yves Le Drian, amesema mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Uingereza, Ufaransa na Ujerumani watakutana na mwenzao wa Iran Jumatatu ijayo, kutafakari mazingira ya makubaliano hayo baada ya pigo la Donald Trump. Ahadi nyingine ya kuyalinda makubaliano hayo kuhusu Iran imetolewa na China na Urusi ambazo pia ziliyatia saini.
Hakuna mwenye haki ya kusambaratisha makubaliano ya kimataifa
Federica Mogherini, Mkuu wa sera za nje za Umoja wa Ulaya
Mkuu wa sera za nje za Umoja wa Ulaya Federica Mogherini, amesema Marekani haina haki ya kuchukua hatua za peke yake kuyasambaratisha makubaliano hayo.
''Makubaliano haya ya nyuklia ya Iran sio kati ya pande mbili, na hakuna nchi yenye haki ya kuyasambaratisha inavyotaka. Yaliidhinishwa kwa kauli moja na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika azimio nambari 2231, na nguzo muhimu ya kuzuia kuenea kwa silaha za nyuklia duniani'' Amesema Mogherini, na kuongeza kuwa mpango huo vile vile ni ishara njema katika mazingira ya sasa yanayotoa matumaini ya kuondoa kitisho cha nyuklia katika rasi ya Korea.
Rais wa Iran Hassan Rouhani amemshutumu Rais Trump kwa kuendeleza vita vya kisaikolojia, na kusema nchi yake itaanza tena kurutubisha madini ya urani, ingawa itasubiri kwanza kujadiliana na wadau wengine kabla ya kupitisha uamuzi kamili.
Polisi wa uchumi wa dunia
Rais Trump akitia saini sheria ya kuiondoa Marekani katika mpango wa nyuklia wa Iran
Akitangaza uamuzi wake jana Trump alisema msingi wa makubaliano hayo umeoza, na kwamba hayana uwezo wa kuizuia Iran kupata silaha za nyuklia, na alitoa wito wa kuwepo mkataba mpya ambao unatoa suluhisho la kudumu. Mshauri wake mkuu kuhusu usalama wa taifa John Bolton aliyapa makampuni ya Ulaya yanayofanya biashara na Iran kipindi cha miezi sita kusimamisha biashara hiyo, la sivyo yatakabiliwa na vikwazo vya Marekani.
Waziri wa uchumi wa Ufaransa Bruno Le Maire amesema haikubaliki kwamba Marekani inataka kujifanya polisi wa uchumi wa dunia. Makampuni makubwa ya Ulaya yamejiweka katika hali ya tahadhali, yakisubiri uamuzi wa kisiasa kujua njia ya kufuata.
Uamuzi wa Rais Trump kuiondoa Marekani katika makubaliano hayo juu ya mpango wa nyuklia wa Iran yamekaribishwa kwa furaha na washirika wake wa Mashariki ya Kati ambao ni mahasimu wa Iran, Israel na Saudi Arabia
Maoni