Serikali ya Marekani imezitaka nchi nyingine kuongeza shinikizo kwa Iran kutokana na kuhusika kwake katika mzozo wa Mashariki ya Kati.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Marekani imelikosoa Jeshi la Mapinduzi la Iran, kutokana na vitendo vyake vya kuchangia katika kusababisha ushawishi wa kukosekana kwa amani na utulivu katika Mashariki ya Kati, licha ya watu wa Iran kuwa waathirika wa uchumi unaosuasua.
Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Sarah Huckabee Sanders amevitolea mfano vitendo hivyo vya Iran ambavyo inavifanya katika nchi za Syria na Saudi Arabia na ameyataka mataifa mengine duniani kuishinikiza Iran kuachana na tabia yake hatari. Taarifa hiyo ya Marekani imevikosoa vikosi hivyo kwa kurusha makombora dhidi ya Israel katika milima ya Golan mwanzoni mwa juma hili, hali iliyosababisha Israel kujibu pia kwa mashambulizi siku ya Alhamisi dhidi ya vikosi vya Iran. Hali hiyo imezusha hofu ya kuzuka kwa mzozo katika ukanda huo na hivyo kuhatarisha amani na usalama wa Mashariki ya Kati.
Trump na May walaani shambulizi
Marekani imesema pia Iran imeanzisha mashambulizi ya makombora dhidi ya Saudi Arabia. Jana Rais wa Marekani, Donald Trump alizungumza kwa njia ya simu na Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May na wote kwa pamoja wamelaani vikali mashambulizi hayo ya makombora yaliyofanywa na Iran kutoka Syria dhidi ya Israel na kujadiliana njia nzuri ya kuishughulikia tabia hiyo ya hatari ya Iran.
Hata hivyo, ofisi ya May imesema kuwa kiongozi huyo amerudia kuelezea msimamo wake wa kuendelea kuunga mkono mkataba wa nykulia kati ya Iran na mataifa yenye nguvu, licha ya Trump kujiondoa wiki hii.
Ayatollah Ahmad Khatami
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amesema nchi yake haitovumilia uchokozi wowote ule wa Iran wala kujiimarisha kijeshi nchini Syria. Hata hivyo, Iran imesema ina washauri tu nchini Syria na sio vikosi vya kijeshi.
Khatami aonya
Hayo yanajiri wakati ambapo kiongozi maarufu wa kidini wa Iran, Ayatollah Ahmad Khatami ametishia kwamba miji miwili ya Israel itaharibiwa vibaya kama nchi hiyo itaendeleza kile alichokiita ''vitendo vya kijinga'' na kufanya mashambulizi tena.
Khatami ambaye ameelezea mawazo ya Kiongozi wa kidini mwenye ushawishi mkubwa nchini Iran Ayatollah Ali Khamenei aliyesema Israel haitokuwepo katika kipindi cha miaka 25 ijayo, amebainisha kuwa taifa hilo la Kiyahudi huenda likaharibiwa iwapo litaendelea kuishambulia Iran.
Akizungumza kupitia televisheni ya taifa, Khatami amesema Iran itaimarisha uwezo wake wa makombora siku baada ya siku, na Israel ikifanya jambo lolote la kijinga, basi nchi hiyo itaiangamiza miji ya Tel Aviv na Haifa.
Kwa upande mwingine taarifa iliyotolewa jana na serikali ya Iran imeonya kwamba itachukua hatua yoyote inayoona inafaa, ikiwa haitolipwa fidia sawasawa kutokana na Marekani kujiondoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya Iran kama ilivyokubaliwa katika mkataba huo.
Iran imezitolea wito pande nyingine zilizosaini, hasa Uingereza, Ufaransa na Ujerumani, kuulinda mkataba huo na kuongeza kusema kuwa hakuna masharti au kuhusu muda wa makubaliano hayo ya mwaka 2015 yanayoweza kujadiliwa kwa namna yoyote ile
Maoni