Idadi ya watu waliothibitishwa kufariki kufuatia tetemeko kubwa la ardhi lililoikumba Ecuador imegonga 233
Idadi ya watu waliothibitishwa
kufariki kufuatia tetemeko kubwa la ardhi lililoikumba Ecuador imegonga
233 na kunahofu idadi hiyo itaongezeka maradufu.
Rais wa taifa
hilo Rafael Correa amesema katika hotuba fupi kuwa wanajeshi elfu kumi
(10,000) wametumwa kusaidia na shughuli za uokozi.Aidha Polisi 3,500 pia watajiunga nao kusaidia kuokoa maisha ya majeruhi wa janga hilo la kitaifa.
Tetemeko hilo kubwa lililotikisa maeneo ya Kusini mwa pwani ya Ecuador lilikuwa la kiwango cha 7.8 kwenye vipimo vya Richter.
Makamu wa rais wa nchi hiyo ametangaza hali ya tahadhari katika mikoa sita nchini humo, huku maafisa wa huduma za dharura wamepelekwa kusaidia .
Kitovu chake kilikuwa takriban kilomita 27 kutoka kwa mji wa pwani uitwao Muisne mji ambao kwa kawaida hauna wakaazi wengi.
Maafisa wakuu wanahofia kuwa idadi hiyo ya vifo huenda ikaongezeka kwani maeneo ya mashambani mbali na kitovu cha tetemeko hilo yaani mji wa pwani wa Muisne ndiyo yameanza kutoa taarifa kwa vyombo vya dola kuhusu athari ya tetemeko hilo.
Maafisa katika kituo cha Marekani cha utafiti wa kijiologia wamesema tetemeko hilo la ardhi lilitikisa hadi sehemu ya mpakani na taifa jirani ya Colombia.
Image copyright AFP
Rais Correa amewahakikishia wahasiriwa wa mkasa huo kuwa msaada wa serikali uko njiani.
Hata hivyo mabasi na malori ya kijeshi yanatatizika kuwafikia wahanga walioporomokewa na majengo yao kufuatia maporomoko makubwa ya ardhi yaliyoziba mabarabara.
Aidha misaada ya chakula na madawa kutoka mataifa jirani yameanza kupokewa kutoka Venezuela na Mexico.
Takriban watu 600 wamejeruhiwa japokuwa idadi hiyo bila shaka inatarajiwa kupanda.
Meya wa mji wa Pedernales Gabriel Alcivar amesema kuwa mji wote umeporomoka
Mji wa Guayaquil ulioko takriban kilomita 300km kutoka kitovu cha tetemeko hilo pia limeathirika vibaya na hata daraja la pekee linaloiunganisha limeporomoka.
Visa vya utovu wa nidhamu pia vimeripotiwa huku watu wakipora majengo ya watu na maduka
Maoni