MTEULE THE BEST
Kwako Mheshimiwa Rais,
Kwanza kabisa nakupongeza kwa kazi nzuri unayoifanya ya kuongoza taifa hili la Tanzania na pia pole kwa majukumu uliyonayo,kuna mengi mazuri unayafanya huenda sisi watanzania wa kawaida hatuyaelewi na kuona unakosea ila naamini mwisho wa siku tutaelewa.
Lengo la ujumbe huu kwako ni kuhusiana na kilio tulichonacho sisi vijana ambao kwa muda sasa tunasubiri ajira. Ni muda wa miezi 9 umepita tangu uliposema mbele ya vyombo vya habari kuwa zoezi la uhakiki litadumu mwezi mmoja na nusu haitozidi miwili utakuwa umetoa ajira ambapo wengi tukawa tuna matumaini kuwa zitatoka ajira zile 71,000 lakini mpaka leo kwa taarifa mzitoazo ni kuwa mmetoa ajira 5000 kuachia mbali za wakurugenzi na wenyeviti wa taasisi mbalimbali.
Si kweli kwamba vijana wote ni wavivu na tumeshindwa kujiongeza la hasha kinachopelekea tuonekane wazembe, hatuwezi kujiongeza,mizigo kwa wazazi,hatutaki kujiajiri sababu kubwa ni hizo ahadi zenu mnazotupa za miezi miwili miwili zinafanya tuwe na matumaini makubwa na kungoja ahadi maana hii serikali tunaiamini sana katika utekelezaji wa mambo.
Kutotolewa kwa ajira mpaka sasa kumepelekea hata wazazi wetu waliokupenda sana wakati wa kampeni,kubishana kuwa wewe ni bora kuliko wengine na hata kuimba sana ule wimbo wa waisome namba wameanza kukuchukia kwa sababu walitoa ada zao, gharama zao ili kuwasomesha watoto wao ili wakipata kazi basi waendeleze familia na kuwasaidia ndugu zao. Imepelekea hata kuchukia kauli zako pale wanapolalamika hela hakuna mtaani,imepelekea kuona kila ukisemacho kama hakina maana kwao na sisi vijana kuona serikali hii haitujali tena.
Ombi langu kwako Mheshimiwa Rais Magufuli ni kuwa tuambie ukweli ni lini umepanga kutoa ajira hata kama ni baada ya mwaka huu kuisha au miaka miwili mbele tutaumia ila itatusaidia kujipanga vyema na kamwe hutosikia tukilalamika kuhusu ajira. Chondechonde kupitia mawaziri wako naomba msitupe ahadi tamu za kuwa ajira zitatoka baada ya muda mfupi wakati mipango ya serikali si kutoa ajira mapema.
Maoni