Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema mkoa umetenga shule za Sekondari za Bweni za Serikali kuwa maeneo ambayo yatatumika kuwahifadhi washukiwa wa Virusi vya Corona endapo watapatikana mkoani hapa; baada ya serikali kufunga shule na vyuo nchini kwa siku 30 lengo likiwa kukabiliana na ugonjwa huo.
Mhe. Mtaka ameyasema hayo wakati akipokea mchango kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ya shule ya sekondari Anthony Mtaka uliotolewa na umoja wa madhehebu ya kikirsto Lamadi na kuongeza kuwa mbali na maeneo ya shule Mkoa pia umetenga maeneo ya hoteli ambayo yatatumika endapo washukiwa/watu wanaohisiwa kuwa na ugonjwa huo ambao hawatahitaji kukaa kwenye maeneo ya shule.
"mkoa hautatumia hoteli kwa ajili ya kuhifadhi mtu yeyote atakayeshukiwa kuwa na maambukizi ya virusi vya corona badala yake tutatumia shule za zetu za sekondari za bweni lakini ikitokea mtu anahitaji kukaa hotelini tayari tumeandaa hoteli za kutosha"alisema Mtaka.
" Tumechukua uamuzi huu ili kuwapunguzia watakaoshukiwa kuwa na ugonjwa huo gharama ila utaratibu huu hautawafunga watu wenye uwezo ambao watapenda kwenda hotelini; kwa mara nyingine tena niwaombe wananchi kuendelea kuchukua tahadhari na kuzingatia maelekezo yanayotolewa na viongozi kuzuia maambukizi ya CORONA" aliongeza Mtaka
Hata hivyo aliongeza kuwa tayari kila wilaya imetenga shule yenye vitanda vya kutosha na mazingira mazuri kwa ajili ya washukiwa wa ugonjwa huo, huku akiwataka wananchi wa mkoa huo kuendelea kuchukua tahadhari.
Mbali na hayo amewataka wazazi wa wanafunzi wa madarasa ya mitihani mkoani humo kuhakikisha wanawasimamia watoto wao wanajisomea katika wa kipindi hiki ambacho shule zimefungwa kutokana na ugonjwa huo.
Maoni