KATIBA YA CCM YARUHUSU MIKUTANO YAKE KUFANYIKA KWA NJIA YA MTANDAO




Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameongoza Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, kufanya mabadiliko madogo ya Katiba ya CCM ambapo sasa Katiba hiyo inatambua ufanywaji wa mikutano ya ngazi mbalimbali kwa njia ya mtandao maarufu kama E- Meeting.

Kulingana na Dkt. Samia wakati akitangaza mapendekezo hayo kwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM, Mabadiliko hayo ni katika kuhakikisha kuwa Chama hicho kinaenda sawa na mabadiliko mbalimbali ya teknolojia yanayotokea duniani,suala ambalo limewezesha CCM pia kufunga Mitambo ya teknolojia yenye kuwezesha Ngazi za CCM wilaya na Mikoa kuweza kuunganishwa pamoja na Makao Makuu kwa njia ya mtandao.

Rais Samia amebainisha kuwa Idara ya Oganaizesheni ilipendekeza vikao vitakavyoweza kufanyika kimtandao ni Vikao vya Sekretarieti ya Wilaya, Kamati za siasa za wilaya, Sekretarieti za Mikoa, Kamati za siasa za Mikoa, sekretarieti ya Kamati maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Kamati Maalum ya halmashauri kuu ya CCM Taifa, Halmashauri kuu ya CCM Taifa pamoja na Mkutano Mkuu wa Taifa.

"Vikao husika vitafanyika kwa njia ya mtandao endapo tu kuna ulazima, vikao husika kwa ngazi ya Mkoa vitafanyika kwa idhini ya Katibu Mkuu. Watamjulisha Katibu Mkuu kwanini wafanye kikao kwa mtandao na hii ni kuepusha kutumika vibaya kwa mitandao hii." Ameongeza Dkt. Samia.

Mabadiliko mengine ya Katiba yaliyofanywa na Mkutano Mkuu wa CCM Leo Alhamisi ni pamoja na Kuongeza idadi ya mabaraza ya wadhamini kutoka nane hadi tisa pamoja na mabadiliko madogo ya kutaka miradi ya maendeleo inayotekelezwa ngazi ya Mikoa kukasimiwa kwa maandishi tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

ZIJUWE SHERIA 17 ZA SOKA

MAPENZI: Kuna faida na ni muhimu Mpenzi wako kuwa rafiki yako pia

KUMTUMAINIA MUNGU