MTEULE THE BEST
Upinzani nchini Venezuela umeahidi kuendelea kumshinikiza rais wa nchi hiyo, Nicolas Maduro, baada ya maelfu ya waandamanaji kumiminika majiani katika mji mkuu wa Caracas hapo jana
Waandamanaji hao wanataka kuitishwe kura ya maoni ya kumuondoa madarakani kiongozi huyo, kabla ya Januari 10. Iwapo Maduro atashindwa katika kura hiyo ya maoni, italazimika kufanyike uchaguzi wa mapema.
Kiongozi wa upinzani wa chama cha Democratic Unity Roundtable, Jesus Torrealba, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba yalikuwa ni maandamano makubwa kuwahi kutokea katika miongo kadhaa iliyopita. Alisema kuwa kati ya watu 950,000 hadi milioni moja na laki moja walijitokeza katika maandamano hayo. Na wameahidi kuendelea na shinikizo hilo hadi pale rais wa nchi, Nicolas Maduro,
"Leo ndiyo mwanzo wa jitihada zetu tukiwa pamoja na raia wote wa Venezuela, wanaotimiza haki yao ya kikatiba ya kuandamana kwa amani hadi pale kutakapopatikana mabadiliko ya kikatiba na yaliyo ya kidemokrasia,” amesema Jesus Torrealba.
Waandamanaji waliokuwa wamevalia nguo vyeupe walikuwa wakipiga mayowe wakisema "Venezuela imekumbwa na njaa. Na serikali hii lazima itaanguka."
Wananchi wa Venezuela wanalalamikia hali mbaya ya uchumi, pamoja na uhaba wa chakula na madawa.
Hali ilibadilika na kuwa ya wasiwasi wakati maandamano hayo yakiendelea. Serikali ya Maduro iliwakamata wanaharakati kadhaa pamoja na kutuma vikosi vya polisi katika kila kona ya mji na kuonya kutatokea umwagikaji wa damu.
Wafuasi wa Maduro pia walijitokeza
Kundi dogo la watu waliokuwa wamejifunika nyuso huku wakirusha mawe, walikabiliana na polisi karibu na mwisho wa maandamano hayo. Polisi ilitumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya na pia iliwatia mbaroni baadhi ya vijana miongoni mwao.
Sambamba na maandamano hayo ya upinzani, wafuasi wa rais Maduro nao waliandamana kumhakikishia kiongozi huyo kwamba wapo naye pamoja, wengi wao wakiwa ni watumishi wa serikali. Idadi ya wafuasi wa Maduro waliojitokeza inakadiriwa kuwa watu 30,000.
Akiwahutubia wafuasi wake, Maduro aliwaambia kuwa upinzani unapanga mapinduzi dhidi yake kama yale yaliyoiondoa kwa muda mfupi serikali ya mtangulizi wake, Hugo Chavez mwaka 2002.
"Tumewakamata wanachama kadhaa wa ngazi za juu wa siasa za mrengo wa kulia ambao walitaka kufanya mapinduzi. Walikuwa na mipango ya kutega mabomu, walimiliki silaha, pamoja na maelfu ya dola ya fedha haramu. Walikuwa na mipango ya kuwashambulia watu wao wenyewe," amesema Nicolas Maduro.
Baada ya kauli yake hiyo, upinzani umetangaza mipango ya kufanya maandamano mengine mawili ya kitaifa, ya Septemba 7 yatazilenga ofisi za tume ya uchaguzi na ya pili yatafanyika Septemba 14.
Matumaini ya upande wa upinzani ni kushinikiza kuitishwa kwa kura ya maoni ya kumuondoa Maduro madarakani kabla ya mwaka huu. Iwapo Maduro atashidwa, kutaitishwa uchaguzi mkuu wa mapema na upinzani unatarajiwa kushinda kulingana na utafiti wa maoni ya jamii. Lakini kama kura hiyo itacheleweshwa hadi baada ya Januari 10 na Maduro akashidwa, makamu wake wa rais atalazimika kumpokea wadhifa wa urais hadi muhula wake utakapo malizika mwaka 2019.
Maoni