MTEULE THE BEST
Watu wawili wameuawa kwa kupigwa risasi wakati wa maandamano ya muungano wa upinzani katika mji wa Bondo, magharibi mwa Kenya.
Taarisa zinasema wawili hao wamefariki baada ya polisi kuwafyatulia risasi waandamanaji ambao inadaiwa walijaribu kuvamia kituo cha polisi cha Bondo katika kaunti ya Siaya.
Mkuu wa polisi wa eneo hilo John Kiarie ameambia BBC kwamba hawezi kukanusha au kuthibitisha vifo hivyo kwani bado hajapokea maelezo ya kina kuhusu tukio hilo.
Muungano wa upinzani National Super Alliance wake waziri mkuu wa zamani Raila Odinga umekuwa ukifanya maandamano kushinikiza mageuzi kwenye Tume ya taifa ya Uchaguzi IEBC kabla ya uchaguzi mpya kufanyika.
Alhamisi, serikali ilipiga marufuku maandamano katika maeneo ya kati ya miji ya Nairobi, Mombasa na Kisumu baada ya visa vya uporaji kushuhudiwa wakati wa maandamano ya awali.
Jijini Nairobi, polisi leo wamekuwa wakishika doria katika barabara kuu kuwazuia waandamanaji kuingia katikati mwa jiji.
Katika baadhi ya maeneo, polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya au kuwadhibiti waandamanaji.
Katika jiji la Nairobi, kumukuwepo na taarifa za wanahabari kushambuliwa na polisi hao wa kupambana na fujo.
Mahakama ya Juu nchini humo ilifuta matokeo ya uchaguzi wa urais uliofanyika tarehe 8 Agosti ikisema ulijaa kasoro nyingi kiasi kwamba ilikuwa vigumu kubaini nani alishinda kwa njia halali.
Tume ya uchaguzi ilitangaza uchaguzi mpya ungefanyika tarehe 17 Oktoba lakini baadaye ikabadilisha tarehe hiyo hadi 26 Oktoba.
Bw Odinga ambaye alitarajiwa kukabiliana na Rais Uhuru Kenyatta alijiondoa Jumanne akisema mageuzi ambayo yanahitajika bado hayajatekelezwa.
Mahakama Kuu baadaye iliagiza kuongezwa kwa jina la Ekuru Aukot miongoni mwa wawaniaji wa urais hatua iliyoifanya IEBC kutangaza baadaye kwamba wagombea wote wanane watashiriki.
Hali ya utata kuhusu kuandaliwa kwa uchaguzi huo imezidi kwambi Nasa wameendelea kusisitiza kwamba hawatashiriki.
Bw Odinga kwa sasa yuko ziarani Uingereza na amesisitiza kwamba hatatia saini Fomu 24A ambayo tume ya uchaguzi ilisema anafaa kujaza ndipo ajiondoe rasmi kutoka kwa uchaguzi huo.
Pendekezo la IEBC kuhusu fomu hiyo limekosolewa na baadhi ya mawakili wanaosema fomu hiyo inaweza tu kutumiwa iwapo kumefanyika uteuzi wa wagombea jambo ambalo haliwezekani wakati huu kwani uchaguzi ni wa marudio.
Jijini Mombasa waandamanaji walifaulu kuingia katikati mwa jiji kabla ya polisi kuwarushia vitoa machozi na kuwatawanya.
Wabunge wa eneo hilo wanasisitiza kuwa marufuku ya serikali kuzuia maandamano katikati ya miji mikubwa inakiuka katiba. Kutoka Mombasa, Mwandishi wa BBC aliyepo Mombasa Ferdinand Omondi anasema waandamanaji walifika jijini Mombasa alfajiri na kukusanyika katika bustani moja maarufu, wakiwa na baadhi ya wabunge ya mji huo.
Waliandamana kwa amani huku wakiimba wakielekea katika afisi za tume ya uchaguzi.
Walipita katikati ya mji kwa muda huku polisi wakionekana kusita kuwatawanya kwani waandamani walionekana kutotaka kuzua rabsha zozote. Lakini ghafla tu, askari wakaanza kuwarushia vitoa machozi na kuwatawayanya. Baadaye wakaanzisha msako wa kuwatafuta waandamanaji kwa kuavamia majumba ya watu.
Mbunge wa Upinzani Badi Twalib amelaani hatua hiyo akisema wao hawakufanya lolote lililostahili polisi kutumia nguvu kuwatawanya.
Mbunge mwenzake Abdulswamad Shariff Nassir naye ameambia BBC kuwa amri la waziri wa usalama Fred Matiang'i ya ni kinyume na katiba inayoruhusu wananchi kulalamika kwa njia ya maandamano.
Wabunge wa Mombasa sasa wameitisha mkutano wa hadhara siku ya jumapili katika bustani ya ufukwe wa Mama Ngina kisiwani Mombasa , ili kuwapa wafuasi wao muelekeo wa hatua watakayochukua.
Maoni