iovngozi hao wameeleza mkutano huo wa Zanzibar kuwa wa kihistoria
Vyama sita vya upinzani nchini Tanzania vimekutana na kutoa azimio la pamoja katika kile kinachotazamwa kama juhudi za mapema za kutaka kuungana nchini humo.
Viongozi hao waliahidi kuungana na kuutangaza mwaka 2019 kuwa ni 'Mwaka wa Kudai Demokrasia', na kadhalika wakaahidi kufanya mikutano ya siasa bila kujali katazo la mikutano ya hadhara.
"Ni mwaka ambao tutapambana kuzidai haki zetu zote tunazonyimwa kinyume na sheria na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania," taarifa ya pamoja ya viongozi wa vyama hivyo inasema.
"Kama vyama vya siasa vyenye uhalali na vyenye utaratibu uliowekwa rasmi kisheria na kikatiba, tutatangaza rasmi namna na utaratibu wa kufanya mikutano yetu ya hadhara katika kila kona ya nchi yetu, hatutaruhusu katazo haramu na lisilo na mashiko ya kisheria litumike kutuzuia kutekeleza wajibu wetu."
Waliotia saini azimio hilo ni Maalim Seif Sharif Hamad (Katibu Mkuu, CUF), James Francis Mbatia(Mwenyekiti Taifa, NCCR Mageuzi), Oscar Emanuel Makaidi (Mwenyekiti Taifa, NLD), Salum Mwalimu (Naibu Katibu Mkuu - Zanzibar, CHADEMA), Hashim Rungwe Spunda (Mwenyekiti Taifa, CHAUMMA) na Kabwe Z. Ruyagwa Zitto (Kiongozi wa Chama, ACT Wazalendo).
"Tunao wajibu wa kutoa dira kwa wananchi. Tunasema sasa basi, imetosha," walisema.
Maalim Seif: Yanayotokea chini ya Magufuli, hatujawahi kuyaona Tanzania
Viongozi hao walisema madhumuni ya kuandaa kikao hicho cha siku tatu yalikuwa kuandaa mkakati mpya na wa pamoja wa kupambana na hali ya demokrasia kudorora sana Tanzania.
Kwa sasa Kiongozi wa Kambi Upinzani Bungeni Freeman Mbowe ni mahabusu naye Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni Tundu A. Lissu akiendeleza kuuguza majeraha ya kupigwa risasi mwaka uliopita.
Miongoni mwa mambo wanayosema ni dalili za utawala wa kiimla nchini Tanzania ni kufutwa kwa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa mwaka 2015 ambao upinzani walidai kushinda; kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara na maandamano ya vyama vya siasa na kutekwa na kukamatwa kwa wananchi, wakiwemo viongozi wa kisiasa, waandishi wa habari na wafanyabiashara.
Kadhalika, wametaja shambulio dhidi ya Bw Lissu na uwepo wa sheria mbaya za Habari na Takwimu, pamoja na kanuni za uendeshwaji wa Asasi za Kiraia (AZAKI), Kanuni za Sheria ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na Mswada wa mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa.
'Vita dhidi ya upinzani'
Viongozi ha wanaituhumu serikali ya Rais Dkt John Magufuli kwa kuendeleza vita dhidi ya vyama vya upinzani "pamoja na wote wanaonekana wana mawazo mbadala juu ya namna nchi yetu inavyoendeshwa" hata ndani ya chama tawala cha CCM.
"Imekuwa ni kawaida sasa kwa Mkuu wa Nchi yetu, pamoja na wafuasi wake, kuwaita viongozi na wanasiasa wa vyama vya upinzani, pamoja na wakosoaji wa serikali kuwa ni 'Mawakala wa Nchi za Nje' na si Wazalendo," wamesema.
Viongozi hao wametofautiana na msimamo wa serikali kwamba uchumi wa taifa hilo la Afrika Mashariki unaimarika, na kusema hali ni kinyume."Baada mwelekeo mzuri kiasi wa hali ya uchumi wa nchi yetu kwa miaka kumi, hali ya uchumi wetu imeharibika katika kipindi cha miaka hii mitatu tu ya awamu ya tano," wanasema.
Lowassa: Kuna dalili za āudiktetaā serikali ya Magufuli Tanzania
Viongozi hao wamewaeleza Freeman Mbowe na Esther Matiko, ambao mpaka sasa wako mahabusu, kuwa wafungwa wa kisiasa na kusema msimamo wao utasalia hivyo hadi pale watakapoachiwa.
"Tutapambana kuhakikisha kuwa wao na wafungwa wenzao wote wa kisiasa, nchi nzima, wanapewa nafasi ya kupata haki katika mfumo ulio huru, mbele ya mahakama na mbele ya macho ya umma," walisema viongozi hao
Maoni