Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya England Manchester City wamepangiwa kucheza na klabu ya Schalke ya Ujerumani katika hatua ya 16 bora Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya baada ya droo kufanywa.
Manchester United wamekabidhiwa miamba wa Ufaransa Paris Saint Germain.
Mabingwa hao watetezi wa ubingwa Ufaransa hawajashindwa msimu huu ligini nyumbani ambapo wanaongoza wakiwa na alama 44 kutoka mechi 16. Wana washambuliaji nyota kama vile Neymar, Kylian Mbappe na Edison Cavani.
Walimaliza viongozi Kundi C, kundi ambalo lilikuwa na Liverpool, Napoli na Red Star Belgrade katika hatua ya makundi.
Lakini walishindwa na Liverpool uwanjani Anfield.
United hawajawahi kukutana na Paris St-Germain katika michuano ya Ulaya.
Hata hivyo, mashetani hao wekundu hawajawahi kushinda na klabu yoyote kutoka Ufaransa katika michuano ya Ulaya tangu mwaka 2005.
Droo kamili:
Manchester United v PSG
Schalke v Manchester City
Atletico Madrid v Juventus
Tottenham v Borussia Dortmund
Lyon v Barcelona
Roma v Porto
Ajax v Real Madrid
Liverpool v Bayern Munich
Kwa mashabiki wengi wa Manchester City, wanaonekana kufurahia kukabidhiwa Schalke, ambao kwa kuangalia viwango vya soka ilikuwa ndiyo klabu 'hafifu' zaidi ambayo wangekabidhiwa.
Schalke wamo nafasi ya 13 Bundesliga na wameshinda mechi nne pekee kati ya 15.
Schalke walimaliza wa pili Kundi D nyuma ya Porto lakini mbele ya Galatasaray na Lovomotiv Moscow.
Tofauti na Manchester United na PSG ambao hawajawahi kukutana, Manchester City wamekutana na Schalke awali.
Mara ya karibuni zaidi walikutana Gelsenkirchen mwaka 2008 si muda mrefu baada yao kununuliwa na Sheikh Mansour.
City walishinda mechi hiyo ya hatua ya makundi Europa League kwa mabao 2-0, mabao yao wakifungiwa na Benjani na Stephen Ireland.
Mechi za kwanza zitachezwa 12-13 na 19-20 Februari, na mechi za marudiano 5-6 na 12-13 Machi, 2019.
Katika Europa League, Arsenal wamepangiwa kucheza na Bate Borisov ya Belarus, nao Chelsea - walioshinda kombe hilo mwaka 2013 - wakapewa Malmo ya Sweden.
Mechi hizo nyingi yazo zitachezwa kati ya 14 na 21 Februari 2019.
Arsenal watacheza mechi yao ya marudiano mnamo 20 Februari.
Droo ya Europa League 32 bora
Viktoria Plzen v Dinamo Zagreb
Club Brugge v Red Bull Salzburg
Rapid Vienna v Inter Milan
Slavia Prague v Genk
Krasnodar v Bayer Leverkusen
FC Zurich v Napoli
Malmo v Chelsea
Shakhtar Donetsk v Eintracht Frankfurt
Celtic v Valencia
Rennes v Real Betis
Olympiakos v Dinamo Kiev
Lazio v Sevilla
Fenerbache v Zenit St Petersburg
Sporting Lisbon v Villarreal
Bate Borisov v Arsenal
Galatasaray v Benfica
Maoni