Mamlaka ya Usafiri wa Anga TCAA nchini imekanusha taarifa ya kuzuiwa kwa ndege za Shirika la Ndege la Fastjet, kama ilivyoelezwa na Mwenyekiti Mtendaji wa shirika hilo Laurence Masha, kwa kile ilichokisema ilipokea barua ya shirika hilo Desemba 24 mwaka huu.
Mwenyekiti Mtendaji wa Shirika la Ndege la FastjetLawrence Masha.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es salaam Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari amesema baadhi ya barua za kuomba kuwasilisha ndege hizo zilifikishwa kwao Desemba 24 na hazikushughulikiwa kutokana na kuwa ni kipindi cha sikukuu.
"Nakanusha taarifa si za kweli hatujawahi kukataa ombi la kuleta ndege na hatuwezi kukataa kwa sababu ni maagizo tuliyowaambia." amesema Johari.
"Walileta andiko la mabadiliko ya utawala na fedha tarehe 24 Desemba mwaka huu , na wataalamu wameanza kulifanyia kazi na muda si mrefu tutawajibu," ameongeza.
Aidha Mkurugenzi huyo amesema miongoni mwa masharti ambayo shirika hilo halijafanyiwa kazi ni upatikanaji wa mtaalamu wa uendeshaji wa masuala ya ndege ikiwa ni takwa la kisheria.
"Tuliwaambia wateue 'Accountable Manager' lakini siku ya Desemba 24, tulipokea barua kutoka kwa Mwenyekiti Mtendaji wa Fastjet ambaye ni Laurence Masha, amejiteua mwenyewe kuwa mtaalamu wa ndege wa Fastjet." amesema Johari.
Desemba 17 mamlaka ya usafiri wa anga Tanzania ilitangaza kutoa siku 28 kwa shirika la ndege la Fastjet kushughulikia baadhi ya changamoto zinazowakabili ikiwemo kulipa madeni wanayodaiwa.
Maoni