Wafanyakazi wa shirika la uokoaji wakiwa wanajiandaa kuondoa miili kutoka kwenye helikopter
Idadi ya waliopoteza maisha kutokana na kimbunga Idai kilichoikumba eneo la kusini mwa Afrika zaidi ya juma moja lililopita,imeongezeka kwa kasi siku ya Jumamosi.
Idadi ya waliothibitishwa kupoteza maisha nchini Msumbiji imeongezeka kutoka 242 mpaka 417,waziri wa ardhi na mazingira nchini humo Celso Correia ameeleza.
Idadi hii mpya inafanya waliopoteza maisha Msumbiji, Zimbabwe na Malawi kufikia 700.
Idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka zaidi.
Kimbunga kimeua takribani watu 259 nchini Zimbabwe na Malawi 56.Watu walipoteza maisha kutokana na mvua kubwa iliyonyesha na kusababisha mafuriko.
Lakini Umoja wa mataifa limesema maafisa wataweza kutathimini madhara pale maji yatakapopungua.
Maelfu ya watu wakiwa wanasubiri kuokolewa kutoka kwenye maeneo yaliyokumbwa na mafuriko kusini mwa Afrika
Ofisi ya Umoja wa mataifa inayoshughulikia masuala ya kibinaadamu, OCHA imesema kuwa mto wa Buzi na Zambezi iko kwenye hatari ya kuvujika kingo zake kwa mara nyingine.
''Tutasubiri mpaka maji yaliyotokana na mafuriko yaishe kisha tutafahamu kwa hakika kuhusu idadi ya waliopoteza maisha nchini Msumbiji.Mratibu wa OCHA Sebastian Rhodes Stampa alieleza.
Maelfu wamenasa kutokana na mafuriko, na vituo vingi vya uokoaji vya nchini Msumbuji vimeanza kupokea vyakula.
Watu takriban milioni 1.7 wameathirika kusini mwa Afrika, wakiwa hawana umeme, na maji hasa kwenye maeneo yaliyoathiriwa na kimbunga hicho.
'Kimbunga kibaya' kuwahi kushuhudiwa kimetua Msumbiji
Kimbunga Idai huenda kikaathiri mvua Afrika mashariki
Siku ya Ijumaa, ilielezwa kuwa kumetokea mlipuko wa maradhi ya kipindupindu mjini Beira, katikati mwa Msumbiji.Shirika la Msalaba mwekundu lilionya hatari ya kutokea maradhi mengine ya mlipuko, huku tayari kukiwa na taarifa ya mlipuko wa maradhi ya malaria.
Wafanyakazi wa mashirika ya misaada wanawasilisha misaada taratibu lakini wakikabiliwa na changamoto ya kuwafikia wengine walio kwenye maeneo yasiyofikika huku vyombo vya anga vya kupeleka misaada vikielezwa kuwa vichache.
Makundi ya watoa misaada nchini Msumbiji yanasema kuwa takriban watu 90,000 wanaishi kwenye maeneo ya muda mfup, huku maelfu wengine bado wakiwa kwenye maeneo yaliyofurika kutokana na mvua.Shirika la Habari la Ufaransa limeripoti
Maoni