Wazee, watoto, wanawake wajawazito na watu wenye ulemavu wanaendelea kuumia kutokana na ukosefu wa chakula na maji.
Huku Wakenya wakiendelea kujadili haja ya serikali kushughulikia ukame, makali ya njaa yanaendelea kushuhudiwa katika kaunti ya Turkana ambayo imekumbwa na ukame.
Chini ya #WeCannotIgnore , Wakenya kupitia mitandao ya kijamii wamekuwa wakiitaka serikali ichukua hatua juu ya njaa inayoendelea kusababisha vifo .
Mjadala huo unaendelea huku idadi ya watu waliokufa kutokana na njaa ikipanda ambapo shule zimelazimika kufungwa huku wanafunzi wakiwafuata wazazi wao kwenye maeneo ya misitu kutafuta chakula.
Wakenya wanauliza 'Ni nini kilitokea kwa mfumo unaotoa taarifa za mapema za maafa?' na kwanini Wakenya wanakabiliana na njaa, katika nchi ambayo usalama wa chakula imekuwa ndio ajenda inayopewa kipaubele zaidi?.
Wazee, watoto, wanawake wajawazito na watu wenye ulemavu wanaendelea kuumia kutokana na ukosefu wa chakula na maji.
''Kila kijiji ninachotembelea, nakutana na kina mana na watoto pekee, hali yao ya afya ikiwa imedorora kabisa. Mifupa kwenye miili yao inaonekana ishara kuwa wamestahimili njaa kwa siku kadhaa'' amesema mwandishi wa BBC Faith Sudi aliyetembelea eneo la Turkana. na kuongeza kuwa hata miti ya miiba ambayo inajulikana kustahimili na kushamiri katika mazingira ya jangwa imekauka.
Hii ndio sura ya njaa Kenya
Watu 1000 wahofiwa kufariki kutokana na kimbuga Msumbiji
Fahamu miji yenye gharama kubwa duniani
Masomo ni miongoni mwa huduma ambazo zimekatizwa katika vijiji vingi ambavyo ukame umekithiri.
Katika shule ya msingi ya Lotukumo iliyoko katika kaunti ndogo ya Turkana ya Kati, wanafunzi wa darasa la nane pekee ndio wako madarasani kwa wote.
"Kwa sababu ya ukosefu wa chakula, wanafunzi wengi wanajiunga na wazazi wao kutafuta chakula popote watakapopata, kwa hiyo hawawezi kufika shuleni" anasema mwalimu mkuu wa shule hiyo Ebong'on Charles.
Mbunge Mwakilishi wa Wanawake katika kaunti ya Turkana Joyce Emanikor anasema baa la njaa linapaswa kuwa historia nchini Kenya.
Darasa la pili ambalo kwa kawaida huwa na wanafunzi 70, liko na wanafunzi 11 pekee.
Darasa la kwanza halina mwanafunzi hata mmoja kwa muda wa wiki mbili sasa.
Katika kijiji cha Nadoto, nyumba nyingi havina watu. Waliobakia katika maboma ni wanawake hasaa wajawazito, wakongwe na watoto wadogo.
Bi Selina Ebei ana mimba ya miezi saba lakini amelazimika kulala siku kadhaa bila chakula.
"Kutokana na hali yangu siwezi kwenda mwituni kila siku kutafuta matunda ya Mkoma kwa sababu ni mbali na jua pia ni kali mno. Wakati mwingine ninakaa siku tano bila kutia chochote mdomoni."
Katika kijiji kimoja nyumba nyingi hazina watu wamebakia wanawake hasaa wajawazito, wazee na watoto wadogo, huku wanaume wakienda msituni kutafuta matunda mwitu
Selina ana mtoto mdogo mwenye umri wa miaka miwili na ambaye pia anamtegemea.
"Mikoma niliyochuna ikiisha, tunakaa njaa tu hadi nitakapojikaza tena kwenda mwituni kuchuma Mikoma ingine. Ninambeba huyu mwanangu mgongoni na kutembea mwendo mrefu kwa sababu hakuna mtu ambaye ninaweza kumwachia amchunge."
"Tunayachemsha na kukunywa supu yake"
Wanaume hawako vijijini kwani wameenda na mifugo kwenye milima kuwatafutia chakula
Mbunge Mwakilishi wa Wanawake katika kaunti ya Turkana anasema kwamba wakati huu ambapo kuna serikali ya Kaunti, baa la njaa linapaswa kuwa historia.
"Ni aibu sana watu kufariki kutokana na baa la njaa katika kaunti ambayo inapokea mgao mkubwa wa mapato. Serikali ya Kaunti iko na uwezo mkubwa kuhakikisha wakaazi wanapata chakula cha kutosha wakati wa janga Kama hili". Anasema Joyce Emanikor.
Kulingana na ripoti kutoka Kwa Wizara ya Majanga na huduma Kwa umma ya kaunti ya Turkana, wakaazi wengi katika kaunti ya Turkana hutegemea ufugaji ili kujikimu kimaisha.
Kwa sasa zaidi ya mifugo 30,000 wamefariki na wengine zaidi ya 100,000 wamehamishwa nchi jirani ya Uganda.
"Tumepoteza mifugo wengi kutokana na ukosefu wa usalama, kisha wale mifugo wadogo ambao wamesalia wanauawa na ukame. Ni sharti serikali ya Kaunti hii irejelee bajeti yake ili kuhakikisha kwamba inazingatia zaidi mahitaji ya wakaazi wa eneo hili. Na iwapo fedha zitatengwa kushughulikia ukame zisifujwe." anasema Joyce Emanikor.
Naibu rais wa Kenya William Ruto alisema kuwa Kenya iko katika fursa nzuri sasa ya kukabiliana na ukame ikilinganishwa na miaka iliyopita.
Serikali hata hivyo imekanusha taarifa kwamba watu kadhaa wamekufa kutokana na njaa inayosababishwa na ukame ambao kwa sasa umeyaathiri maeno ya kaskazini magharibi mwa nchi .
Waziri wa tawala za kaunti Eugene Wamalwa amesema kulikuw ana vifo , lakini akaongeza kuwa haviwezi kuhusishwa na ukame.
Mwisoni ma juma, gazeti la, Daily Nation nchini humo liliripoti kuwa watu kadhaa walikufa kutokana na matatizo yenye uhusiano na njaa katika eneo la Tiaty kaunti ya Baringo.
Gazeti hilo lilisema familia zilizoathirika zilikuwa zinaishi kwa matund ya mwitumi ambayo yanachemshwa kwa saa kadhaa ili kumaliza sumu iliyomo kwenye matunda hayo.
Wakati huo huo Naibu rais wa Kenya William Ruto alisema kuwa Kenya iko katika fursa nzuri sasa ya kukabiliana na ukame ikilinganishwa na miaka iliyopita na akapinga madai kwamba watu wamekufa kutokana na njaa.
Ruto alisema kuwa nchi inachakula cha kutosha na kuongeza kuwa hakuna haja ya kuwa na hofu.
Maoni