Waziri Kivuli wa Mambo ya Nje wa Uingereza akosoa Sheria ya Vyama vya Siasa Tanzania
Waziri Kivuli wa Mambo ya nje wa Uingereza Liz McInnes aimeikosoa Sheria ya Vyama vya Siasa
Waziri Kivuli wa Mambo ya Nje wa Uingereza ameeleza kusikitishwa kwake na kupitishwa kwa sheria ya vyama vya siasa nchini Tanzania ambayo anadai inaminya vyama vya upinzani.
Liz McInnes ambaye ni mbunge kupitia chama cha upinzani Labour amekaririwa na mtandao wa chama chake akisema wapinzani inabidi waachiwe uhuru wao.
''Inasikitisha kusikia kuwa bunge la Tanzania limepitisha sheria ambayo inazuia vikali shughuli za kisiasa na kutoa mamlaka kwa msajili wa vyama vya siasa kuvifutia usajili vyama vya upinzani''.
''Wanasiasa wa upinzani wanapaswa kuwa na uhuru wa kuipa changamoto serikali na si kuhofia kufungwa kwa kutoa maoni yao ikizingatiwa kuwa kuna chaguzi za serikali za mitaa na uchaguzji mkuu mwakani''.
Mwanasiasa huyo ametahadharisha kuwa matendo ya serikali ya Tanzania yana athari mbaya kwa uchumi wa taifa hilo.
"Kwa namna ambavyo wahisani na wawekezaji wa kigeni wanavyoingiwa na hofu kuhusu mazingira ya siasa ya sasa. Rais Magufuli amefanya jitihada kuokoa fedha za nchi ya tatu kwa uchumi mkubwa Afrika Mashariki tangu alipochaguliwa mwaka 2015, lakini kuwe na tahadhari kuhusu sheria hii mpya,'' amekaririwa McInnes akisema.
Sheria mpya ya Vyama vya Siasa imekumbana na upinzania mkali toka muswada wake ulipowasilishwa kwa mara ya kwanza Bungeni.
Vyama vya upinzani na asasi za kirai vimekuwa vikilalamikia sheria hiyo wakidai inafanya shughuli za siasa kuwa kosa la jinai.
Bunge lipitisha muswada huo mwezi Januari na hatimaye kusainiwa kuwa sheria na rais Magufuli.
Bunge lilipitisha muswada huo mwezi Januari na hatimaye kusainiwa kuwa sheria na rais Magufuli.
Wakati wa kupitishwa kwake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama alilieleza Bunge kuwa muswada huo ni kiboko.
Mhagama kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi ni amesema pamoja na mambo mengine muswada huo unalenga kumpa Msajili wa Vyama vya Siasa kuhakiki chama cha siasa wakati wowote.
"Lengo ni kuhakikisha chama cha siasa kinakuwa na sifa za usajili muda wote wa uhai wake na kueleza bayana mamlaka ya msajili wa vyama vya siasa kuhakiki muda wowote utekelezaji wa sheria ya vyama vya siasa ili kuhakikisha chama cha siasa kinazingatia na kutekeleza masharti ya usajili," amenukuliwa na Mwananchi akisema.
Toka kuingia madarakani rais John Magufuli amekuwa akilaumiwa kwa kuminya demokrasia nchini Tanzania. Pia analaumiwa kwa kuminya uhuru wa habari na kujieleza.
Baadhi ya yale yanayolalamikiwa kwenye sheria hiyo ni pamoja na msajili wa vyama vya siasa kupewa mamlaka ya kuingilia mfumo wa uchaguzi ndani ya vyama.
Malalamiko mengine ya uonevu kwa mujibu wa upinzani ni masharti ya namna ya utoaji wa elimu ya uraia kwa kuzuia vyama rafiki kutoka nje kushiriki.
Moja ya kifungu kinachopingwa ni cha Kifungu cha 19 ambacho kinasema msajili anaweza kukisimamisha usajili wa chama kwa sababu atakazozitaja na kwa muda atakaouweka mpaka ili chama hicho kiweze kujirekebisha.
Chama ambacho kimesimamishiwa usajili hakitaweza kufanya shughuli zote za kisiasa.
Na iwapo msajili ataona chama hicho hakijajirekebisha anaweza kukifutia usajili.
Kifungu hiki, wapinzani wanadai kinaweza kutumika kuzuia vyama kushiriki uchaguzi kwa jusimamishiwa usajili kabla yay a uchaguzi na kurudishiwa usajili baada ya uchaguzi kupita
Maoni