Ruka hadi kwenye maudhui makuu

KUYANYAMAZIA MAFUNDISHO YA UONGO NI KUYASHIRIKI

HADI hapo, nilitaka kutoa picha tu ya mafundisho tusiyoyasomea ambayo baadhi yetu wameshajiingiza katika kufundisha. Lakini, kwa nini tunafanya hivyo? Bila shaka, sababu ni tatu: mosi, kutokujua mafundisho ya Kanisa Katoliki ni yapi; pili, kutekwa na vyama vya kitume au vikundi vya dini visivyojali wala kujua mafundisho ya Kanisa Katoliki na tatu, ni tatizo la kumkubali bwana wa pili, ndiye pesa (Mt 6:24).

Mintarafu, kutokujua mafundisho ya Kanisa Katoliki ni yapi ni aibu. Ni aibu kwa padri aliyeandaliwa kuwa mwalimu katika Kanisa kutokujua kitu. Ni aibu kuketishwa chini na kufundishwa mambo batili na kishapo kuinuka yeye mwenyewe kufundisha mambo yasiyo ya Kanisa lake. Tuseme, basi ā€œtumeliwa akiliā€ na wapagani, Wapentekoste, Waislamu na kadhalika.

Inakuaje tuache mafundisho ya kwetu nasi tutumikie dini au makanisa mengine? 

Inakuwaje sisi tulioandaliwa kuwa walimu tugeuzwe kuwa wanafunzi na wale tuliotazamiwa kuwaongoza, yaani walei? Hii ni ajabu ya mwaka!  Kwa aliyeyaona ya Musa haya ndiyo ya Firauni! Tuulizane, je, tutafika? Lakini, ikiwa ni hivi hatuweza kufika salama miaka 300, tusitaje 600 wala 1,000. Pili, kutekwa na vyama vya kitume au vikundi vya dini visivyojali wala kujua mafundisho ya Kanisa Katoliki.

Vyama au vikundi visivyosimama kwenye mafundisho sahihi ya Kanisa Katoliki, hususan, vikiwa na watu maarufu na vikiwa na pesa, vina silika ya kuziba vinywa waliopaswa kuyasimamia mafundisho ya kweli. Huo ni mkasa wa mapadri kuruhusu kufumbwa vinywa kwa pesa. Jambo, hilo ni aibu pia. Haifai padri kunyamazishwa na watu uliopaswa kuwaongoza kuelekea uzima wa milele. Tatu, ni kupotoshwa na sifa binafsi na pesa.

Si siri, tupo wengine ambao tumeshageuka wapenda pesa na ā€œwapiga pesaā€. Lakini tukiachilia mafundisho ya uongo yatamalaki kwa sababu ya sisi kupata au kupewa fedha, tumeshakuwa na mabwana wawili, Mungu na pesa, ambao hatutawamudu kuwatumikia kwa moyo sawa. Huu ni mwanzo wa moja kutuponyoka, na naona atakayetuponyoka kwa wepesi ni Mungu. Yohane anasema, tukiupenda ulimwengu hatuwezi kuwa na Mungu (1Yoh 2:15-16).

Mapadri ilitupasa tuwe macho ya waamini

Mapadri,  acha tukumbushane. Ulikuwa ni wajibu wetu kuangalia ubora wa imani yetu na siyo kuachia mafundisho ya Kanisa yakibomolewa. Huko ni sawa na kukata mti tuliokwea wenyewe. Mti utakapoanguka na sisi tutaanguka pia. Kama wadau wa elimu ya imani yetu, ilitupasa kuangalia nani anafundisha katika eneo letu.

Ilitupasa kuangalia nini kinafundishwa katika eneo letu. Ilitupasa kuangalia wapi kinafundishwa kitu cha uongo na ambacho kitafubaisha Kanisa na mustakabali wake. Kanuni ya kimaadili yasema, kuyaachia au kuyanyamazia mafundisho ya uongo ni kuyashiriki. Kwa hiyo, siyo tu dhambi ya kutotimiza wajibu bali ni mchango wa kuukata mti ambao tumeukwea sisi wenyewe.

Kuhamishia mikazo mahali pengine

Si siri, siku hizi, mapadri kadhaa, badala ya imani, tumehamia kwenye kutenda miujiza, karama za kuponya na kunena kwa lugha. Wapi na wapi mikazo hii! Karama zitokazo kwa Roho Mtakatifu hazikamiwi. Huwa zinatolewa na Roho Mtakatifu kama apendavyo mwenyewe, yaani kwa hiyari yake.

Laiti kila padri angegundua karama yake halisi na kuiweka katika matendo, tungepata ufanisi mkubwa zaidi kuliko kumangamanga na kufedheheka kunakobainika sasa. Tatizo hili linachangiwa na kutomakinika kwetu. Lakini, hata kama si kuhamia kwenye karama hizo, karama zilizo bora zaidi ni upendo na unabii (1Kor 14).

Tunageukaje waigaji mambo?

Jinsi tunavyoendelea baadhi yetu ni kana kwamba hakukuwa na haja ya kujifunza lolote Seminarini. Yaani ni kama ilitosha kuwapadrisha watu na wao kufundisha kwa kuwatazamia wengine. Tunaiga wanachofanya makanisa mengine badala ya sisi kudumu katika uelewa wetu halisi mintarafu karama.

Makanisa mengine hawana utulivu wa mafundisho ya sakramenti saba, ndiyo kisa wanahangaika na kukamia karama mbalimbali lakini hasa kufanya miuji na kunena kwa ndimi (lugha). Lakini, haikupasa mambo kuwa hivi katika Kanisa Katoliki. Mambo ya kuponyana yangeliendelezwa vizuri katika mitandao yetu ya zahanati, vituo vya afya na hospitali. Wamisionari walishatuanzia ujenzi wa miundombinu ya matibabu ya kisasa na elimu nzuri.

Lakini, inaonekana kama tunakataa hayo nasi kupeleka yote kwa Roho Mtakatifu. Lakini ingekuwa Roho Mtakatifu atatufanyie yote, Mungu asingelitupa akili na utashi pamoja na neema bali angelitufanya tuishi kwa silika kama wanyama wa kufugwa na hayawani.

Mambo ya kunena kwa lugha, tungeliweza kunena wenyewe na kuwanenesha waamini wetu kwa elimu ya kweli katika mtandao wetu wa elimu tangu chekechea, shule za msingi, shule za sekondari, vyuo vya ufundi na ualimu pamoja na vyuo vikuu vyetu. Lakini, siku hizi, tunaacha kumakinika na mitandao hii, tunangā€™angā€™aniza moja kwa moja karama za kufanya miujiza, uponyaji na unenaji wa ndimi.

Mimi, sijui ni nani aliyetusadikisha kwamba karama hizi ni bora zaidi kuliko karama zingine? Je, Biblia haijasema upendo ndiyo karama namba wani na inayofuatia ndiyo unabii (1Kor 14)? Kumbe, kungā€™angā€™aniza kwetu karama ambazo hatuna ndiko kunakosababisha tushindwe kufanikisha karama zenyewe.

Injili haitahubirika

Kwa jinsi mapadri tunavyosuasua na imani Katoliki tutasababisha maafa makubwa kwa Injili: haitahubirika. Tunafanya mizaha au tunaachilia mizaha itendeke kwenye matakatifu ya Mungu. Ni mizaha mingi mno:  kulialia, unenaji lugha feki, miujiza feki,  mafuriko ya sala na vitendo vya woga, ā€œkupiga pesaā€,  kujiabisha na kuponzwa kwa wasichana na akinamama wetu, uongo bayana katika uponyaji,  kulegea kwa akinamama wetu, ubishi wa kijinga na kadhalika..

Haya yataugharimu Ukatoliki. Yanawakera sana wanaotutazama. Ukatoliki utageuka kuwa mzaha na dini ya wagonjwa au wajinga tu. Hapo ndipo utume utakapogota. Uinjilishaji hautawezekana kwa sababu watu tunaotaka kuwafikia watakuwa wametutia katika kapu moja na wahuni au wajinga. Watatupuuza na wataupuuza ujumbe wetu. Nahoji.

Hivi tunadhani watu hawafuatilii maendeleo ya Ukatoliki na kugundua jinsi tunavyoudhalilisha? Nimewahi kuwakuta Waislamu wakisema na kushukuru kwamba zamani sana waliwahi kupata matibabu mazuri sana katika hospitali moja iliyokuwa inaendeshwa na ā€œWakatoliki wale wale wenyeweā€. Nilishangaa sana lakini hii ilimaanisha wamegundua siku hizi kuna ā€œWakatoliki wasio wenyeweā€, yaani kuna ā€œWakatoliki fekiā€. Kama mambo ndiyo hivi, hii ni balaa kubwa!

Tano, kuwatoa watu hofu kwa kuwahakikishia Yesu yupo nao

Mintarafu kuwatoa watu hofu kwa kuwahakikishia kwamba Yesu pamoja nao, tatizo ni moja: kupamba moto kwa mafundisho ya kutia watu hofu kutoka kwa makanisa mengine na dini zingine wanayodakia Wakristo wetu. Badala ya kuwafikishia watu Habari Njema yenye furaha, waamini siku hizi wanasongwa na mafundisho ya kutisha: majini, laana, kufungwa na mikosi, Shetani na kadhalika. Kituko hiki ni nini?

Wala tusisahau, mtaji wa makanisa mengine na wachungaji wao ni kuwahubiria watu habari za kutisha kusudi watu wakitishika ā€œwawapige pesaā€. Natoa mifano. Mafundisho hayo ni hasa, ā€œkuathirika kwa Wakristo na laanaā€, ā€œkusongwa kwa watu na majiniā€, ā€œkujiinua kwa Shetaniā€, ā€œwatu kufungwa kwa mikosi na balaa mbalimbali jambo linalohitaji huduma ya kuwafungulia watu vifungo vyaoā€, ā€œkuathirika kwa watu kwa uchawi na uloziā€, ā€œkusongwa kwa watu na Frimasoniā€ na kadhalika.

 Kuna mkasa umezuka. Waamini wetu wameyasikia mafundisho haya kutoka kwa makanisa jirani na hivyo na wao kujihisi wanahusika nayo. Kwa namna hiyo wamejinasisha wenyewe kwenye matatizo ambayo hayakuwa lao.

Kumbe, baada ya kujisikia wanahusika nayo wanahisi Kanisa Katoliki ā€œlinazubaaā€ katika kuyashughulikia. Ndipo wanapohangaika na kutaka mapadri wajitose kwa haraka katika kushughulikia hofu hizo. Hapo ndipo, kwa kudhani Kanisa Katoliki linazubaa, baadhi wanapoipokea Karismatiki kama chombo cha kuzishughulikia hofu za namna hiyo.

Mapato yake ni mahangaiko ambayo, mapadre, badala ya kuwatuliza watu na kuwaweka sawa, baadhi wanaunga mkono pamoja na mapendekezo ya ā€œdawaā€ wanazozianisha ā€œwatawa na waleiā€ na wengineo wahangaikao. Huko ndiko kutolewa kwa mapadre kwenye njia nyofu. Kwa kujua au kwa kutokujua, mapadri wengine wametumbukizwa kwenye hofu hizo mno kiasi cha kusahau kabisa elimu yao na teolojia waliyosomea kwa jasho la kutosha.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MAPENZI: Kuna faida na ni muhimu Mpenzi wako kuwa rafiki yako pia

Kuna faida kubwa kwa wapenzi kuwa marafiki KUTOKANA na mila mbalimbali, baadhi ya watu wamekuwa wakiamini kwamba mwanamke ni daraja la pili. Daraja la kwanza na lenye kuthaminiwa ni mwanaume. Yaani mwanamke hana kauli kwa mwanaume. Anakuwa kama mtumwa fulani hivi.  Mwanaume akiongea, basi ni maelekezo kama vile rais wa nchi anavyotoa maelekezo kwa watu walio chini yake. Hakuna wa kupinga. Akisema sitaki kitu fulani kifanyike, basi ni mpaka atakapotoa maelekezo mengine. Vinginevyo, maelekezo ya awali yatabaki kusimama kama sheria.  Wapo baadhi ya wanawake wanaofurahia aina hii ya uhusiano kwa sababu ya mazoea. Kwamba wamekuzwa hivyo, mwanaume ni mwanaume. Huu ni mfumo ambao watu wengi wamekuwa wakiuishi. Kuna ambao wanakubaliana nao, wengine hawakubaliani nao.  Watu wengi sana wamekuwa wakiishi katika malumbano katika mahusiano yao kutokana na mfumo huu wa maisha. Mwanamke hataki kuishi kama mtumwa, mume anakomaa kuonesha uanaume wake. Hakuna anayekubali kushuka,...

Urusi: Vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini havitafua dafu

MTEULE THE BEST Image caption Waziri wa maswala ya kigeni nchini Urusi Sergei Lavrov na mwenzeka wa Marekani Rex Tillerson Waziri wa maswala ya kigeni nchini Urusi Segei Lavrov amemwambia waziri wa ulinzi nchini Marekani Rex Tillerson kwamba kuiwekea vikwazo zaidi Korea Kaskazini hakutafua dafu. Taarifa iliochapishwa na wizara ya kigeni nchini Urusi inasema kuwa wawili hao walizungumza kwa njia ya simu na kushutumu majaribio ya makombora ya hivi karibuni yaliotekelezwa na Pyongyang . Lakini inasema kuwa bwana Lavrov alisisitiza kwamba diplomasia ndio njia ya pekee ya kumaliza wasiwasi katika rasi ya Korea, na kutaka hatua zozote dhidi ya taifa hilo kusitishwa akionya huenda zikasababisha madhara yasiojulikana. Waziri wa ulinzi nchini Marekani amesisitiza kuwa bado kuna fursa ya kidiplomasia katika kukabiliana na Korea Kaskazini. Mapema rais Trump alichapisha ujumbe katika akaunti yake ya Twitter akisema mazungumzo sio suluhisho.

Fuvu la binadamu wa kale liligunduliwa miaka 60 iliyopita nchini Tanzania

Fuvu la binadamu wa kale liligunduliwa miaka 60 iliyopita nchini Tanzania Miaka 60 siku kama ya leo ugunduzi mkubwa ulifanyika katika eneo la Olduvai Gorge, kwenye kreta ya Ngorongoro. Wanaakiolojia Louis na Mary Leakey waligundua fuvu la mtu anayeaminika kuwa ni wa kale zaidi waliyompa jina la Zinjanthropus. Ugunduzi huo uliofanyika saa nne asubuhi Julai 22, 1959 kipindi hicho kwenye eneo la Tanganyika ulikuwa wa vipande zaidi ya 100 ukasaidia katika kutambua asili ya watu wa awali duniani. Kabla ya ugunduzi huo, wanasayansi na wanahistoria walikuwa wakiamini kuwa binadamu wa kale walitokea Uchina baada ya ugunduzi wa mafuvu ya kale baina ya 1923 na 1927 nchini humo ya Homo eractus, ama maarufu kama Peking Man. Mafuvu hayo ya Uchina yalikuwa na umri wa takribani miaka 750,000. Mafuvu ya Olduvai eneo ambalo kwa sasa lipo Tanzania wakati wa ugunduzi wake lilikuwa na umri wa takribani miaka milioni 1.75, na hakuna mabaki ya mtu wa kale zaidi ambayo mpaka sasa yamegundul...