Mkufunzi mkuu wa Real Madrid Zinedine Zidane amesema washambuliaji wake Gareth Bale, 28, na Karim Benzema, 30, "watasalia" katika klabu hiyo licha ya tetesi kudokeza kwamba huenda wakahama. (Star)
Bournemouth wanaaminika kuwa tayari kushindana na Tottenham na Manchester United katika kutafuta saini ya beki wa Celtic kutoka Scotland Kieran Tierney, 20. (Sun)
Meneja wa Arsenal anayeondoka Arsene Wenger atachukua "miezi minne hadi mitano" kuamua kuhusu mustakabali wake. (London Evening Standard)
Mshambuliaji wa zamani wa Celtic Chris Sutton anasema "litakuwa jambo zuri sana kwa soka ya Scotland iwapo Steven Gerrard atakuwa meneja wa Rangers". Hata hivyo amemtahadharisha nahodha huyo wa zamani wa Liverpool kwamba "hatua kama hiyo inaweza kufuta matumaini yake ya kuwa mkufunzi tajika hata kabla yake kuanza" (Mail)
Meneja wa Tottenham Mauricio Pochettino amekataa kuthibitisha iwapo atakuwa kwenye klabu hiyo msimu ujao. (Mirror)
Naye meneja msaidizi wa Liverpool Zeljko Buvac ameihama klabu hiyo baada ya kuzozana na meneja wa sasa Jurgen Klopp. (Daily Record)
Mshambuliaji wa Crystal Palace mwenye miaka 27 Christian Benteke, ambaye amesalia na miaka miwili pekee katika mkataba wake na klabu hiyo, amesema atajadiliana kuhusu hatima yake na klabu hiyo mwisho wa msimu. (Mail)
Mfanyabiashara Mmarekani Shahid Khan anaweza akaukubali mpangilio wa "lipia ukiendelea kuchezea" kati yake na Chama cha Soka cha England kama sehemu ya makubaliano kati yake na chama hicho kuhusu ununuzi wa uwanja wa Wembley. Mpangilio kama huu unaweza kuifanya nafuu kwa FA kutumia viwanja vya nje kucheza mechi zake. (Times )
Klabu ya West Brom ambayo imo hatarini ya kushushwa daraja itapigania kusalia na beki wa England Craig Dawson mwenye miaka 27 ambaye anatafutwa na Burnley, Wolves na West Ham. (Mirror)
Kipa wa West Brom Ben Foster, 35, amesema kaimu meneja wao Darren Moore amefanikiwa kurejesha tena umoja katika timu hiyo na angependa mkufunzi huyo amepewe kazi hiyo kwa mkataba wa kudumu. (Telegraph)
Meneja wa Chelsea Antonio Conte amesema matatizo ambayo yameikumba timu hiyo msimu huu ni kutokana na kutomakinika vyema zaidi kwenye goli. (Express)
Meneja wa Manchester City Pep Guardiola ametania kwamba mabingwa hao wa Ligi ya Premia wanaweza kutumia £1bn kipindi cha kuhama wachezaji mwisho wa msimu. (ESPN)
Guardiola amesema Manchester City hawatasaini wachezaji zaidi ya wawili mwisho wa msimu. (Manchester Evening News)
Meneja wa Manchester United Jose Mourinho ana wasiwasi kwamba huenda mshambuliaji wake Romelu Lukaku, 24, huenda asiweze kucheza fainali ya Kombe la FA dhidi ya Chelsea baada yake kuumia mguuni akicheza dhidi ya Arsenal Jumapili. (Times )
Ajax wanamtaka kinda wa miaka 19 wa Chelsea anayecheza safu ya kati Mason Mount. Mount alikuwa kwenye kikosi cha England kilichoshinda ubingwa wa Ulaya kwa wachezaji wa chini ya miaka 19 mwaka jana. (Sun)
Wolves wamewaomba radhi mashabiki wao baada ya kusahau kuandaa gwaride la kusherehekea kushinda ligi ya Championship Jumamosi. (Birmingham Mail)
Wachezaji wa Newcastle hatimaye walipata fursa ya kushiriki sherehe yao ya Krismasi mwishoni mwa wiki. (Newcastle Chronicle)
Mkufunzi mkuu wa Watford Javi Gracia amesema ana imani kikamilifu na watabibu wa timu hiyo licha ya kutokea kwa msururu wa visa vya wachezaji wa klabu hiyo ya Vicarage Road kuumia. (Watford Observer)
Meneja wa Leicester City Claude Puel amesema pengine wachezaji wameanza kuleweshwa na Kombe la Dunia au mambo mengine baada ya uchezaji wa timu yake kudorora. Walichapwa 5-0 na Crystal Palace. (Guardian)
Claude Puel
Mpenzi wa mchezaji wa zamani wa Newcastle Davide Santon amesema ana wasiwasi kuhusu kukaa kwao nyumbani baada yake na beki huyo wa Inter Milan kutumiwa ujumbe wa vitisho. (Football Italia)
Brighton wanatarajiwa kukoleza ushirikiano na Gereza la Lewes kama sehemu ya mpango wa kuwasaidia wafungwa kuzoea maisha ya kawaida baada ya kuachiliwa huru. (Argus
Maoni