Magufuli akizungumza na wananchi katika sherehe za ufunguzi wa Barabara ya Iringa-Dodoma Jumapili
Rais wa Tanzania Dkt John Magufuli amewataka raia nchini humo kuwapuuza wanaodai Serikali inakopa sana.
Kiongozi huyo alisema mikopo inayochukuliwa na taifa hilo ina manufaa na itachochea ukuaji wa uchumi.
Dkt Magufuli alikuwa akihutubu alipokuwa anaifungua rasmi barabara ya lami ya Iringa - Migoli - Fufu yenye urefu wa kilometa 189.
Barabara hiyo inaunganisha Mkoa wa Iringa na Mkoa wa Dodoma na Barabara hiyo ambayo ni sehemu ya barabara kuu ya kuanzia Cape Town nchini Afrika Kusini hadi Cairo nchini Misri (The Great North Road).
Ujenzi wa barabara hiyo uligharimu Shilingi Bilioni 207.457 ikiwa ni ufadhili wa benki ya maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa asilimia 65.9, Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) kwa asilimia 21.3.
Serikali ya Tanzania ilitoa asilimia 12.8.
Tanzania imekuwa ikikopa kutoka kwa mashirika ya kimataifa kufadhili miradi mingi ya miundo mbinu ikiwemo miradi ya barabara na reli.
Ripoti ya mwaka wa kifedha wa 2016/2017 ripoti ya Bank Kuu ya Tanzania inaonesha deni la taifa hilo limefikia Dola 23.78 bilioni (zaidi ya Sh52.29 trilioni).
Deni hilo liliongezeka kwa asilimia 9.1 katika mwaka huo ulianza Juni 2016.
Hata hivyo, serikali imesisitiza kwamba kiwango hicho cha deni badi hakijapita kiwango kinachokubalika kimataifa.
Deni hilo ni sawa na asilimia 48.9 ya pato la Taifa, kwa mujibu wa ripoti hiyo ya BOT.
Sehemu kubwa ya deni hilo ni kutoka kwa wakopeshaji wa nje ambao wameikopesha Tanzania dola za Marekani bilioni 18.5.
Kiasi hicho kiliongezeka kwa asilimia 8.9 ukilinganisha na kiwango cha deni mwaka uliodangulia ambapo deni lilikuwa dola za Marekani bilioni 16.4.
Baadhi ya wachanganuzi wameikosoa hatua ya serikali kukopa kiasi kikubwa cha fedha lakini Dkt Magufuli amesema hakufai kuwa na wasiwasi wowote.
Akihutubu Iringa, Rais huyo alisema na fedha hizo hukopwa kwa masharti nafuu, riba ndogo na hulipwa kwa muda mrefu, na kwamba ndizo zinatumika kujenga miundombinu ya kuchochea uchumi.
Wakati wa kuadhimisha miaka 54 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar katika sherehe zilizofanyika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, kiongozi huyo alieleza matumaini kwamba uchumi wa Tanzania utatengemaa.
"Taifa letu linakwenda vizuri, uchumi wetu unakua vizuri, mwaka jana umekuwa kwa wastani wa asilimia 7 na mwaka huu tunatarajia utakua kwa wastani wa asilimia 7.1, mfumuko wa bei umeendelea kuwa chini kwa wastani wa asilimia 4," alisema.
Baadaye alikutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt Akinumwi Adesina.
Taarifa iliyotolewa na ikulu ilisema Dkt Adesina alimpongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya kuimarisha uchumi wa Tanzania na kusema wamejadiliana mambo kadhaa yakiwemo namna benki hiyo ilivyosaidia juhudi za maendeleo za Tanzania tangu mwaka 1971 na inavyoendelea kusaidia katika ufadhili wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Alitaja baadhi ya maeneo ambayo AfDB itatoa ufadhili kuwa ni uzalishaji na usambazaji wa nishati, uboreshaji wa miundombinu ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya Jiji la Dodoma hasa barabara.
"Yote kwa yote nimemhakikishia Rais Magufuli kuwa AfDB itamuunga mkono katika mipango yake na maono yake ili tuweze kuisaidia Tanzania kukua zaidi, nimefurahi kuzungumza na Mhe. Rais na naona Tanzania ipo katika njia sahihi," alisema Dkt Adesina kwa mujibu wa taarifa hiyo ya ikulu.
Kwa mujibu wa Dkt Magufuli, AfDB imefadhili miradi ya maendeleo yenye thamani ya Dola za Marekani Bilioni 3.457 (sawa na Shilingi Trilioni 7.78 Tanzania) zikiwemo fedha za miradi 25 zilizotolewa kuanzia mwezi Novemba, 2017 yenye thamani ya Dola za Marekani Bilioni 1.986 (Shilingi Trilioni 4.47 Kitanzania).
Maoni