Prof Mussa Assad ametiwa hatiani na Bunge kwa tuhuma za kudharau chombo hicho.
Mkaguzi na mdhibiti wa Hesabu za Serikali nchini Tanzania Prof Mussa Assad amesisitiza kuwa ataendelea kutumia neno dhaifu.
Akiongea na waandishi wa habari baada ya ripoti zake kuwasilishwa Bungeni, Prof Assad amesema neno hilo ni la kawaida kwenye fani ya uhasibu.
"Neno 'dhaifu' naendelea kusisitiza ni lugha ya kawaida katika ukaguzi wetu. Na tutaendelea kulitumia," Prof Assad amesema.
Hata hivyo Prof Assad hakuwepo Bungeni kama ilivyokuwa miaka ya nyuma. Mkutano wake na wanahabari umefanyika kwenye ofisi yake mjini Dodoma.
"Hatujakurupuka kufanya mkutano huu hapa ofisini kwetu. Tulihisi mapema hatutakaribishwa bungeni. Tumeongea nanyi hapa kwetu, hata kama ninyi waandishi wa habari hamtatoa hiki tulichozungumza, sisi tutatoa kwa umma," amesema Prof Assad.
Azam TV@azamtvtz
āKwa mwaka 2017 tulitoa mapendekezo 350, yaliyotekelezwa kwa ukamilifu ni mapendekezo 80 sawa na asilimia 23ā ā CAG Prof Assad#AzamTVUpdates #AzamTVApp #RipotiYaCAG2018
120
28 people are talking about this
Mwisho wa ujumbe wa Twitter wa @azamtvtz
Mapema leo ripoti za CAG ziliwasilishwa Bungeni baada ya vuta ni kuvute toka wiki iliyopita.
Hatua hiyo imeondoa wingu jeusi lililokuwa linazagaa kwa wiki mbili juu ya utata wa kikatiba kuhusiana ushirikiano wa Bunge na CAG.
Wiki iliyopita, Bunge lilipitisha azimio la kutofanya kazi na Profesa Assad kwa sababu ya kauli yake aliyoitoa wakati akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa (UN) kuwa Bunge ni dhaifu.
Mgororo uliopo ulianza Disemba 2018 baada ya CAG kuiambia Idhaa ya Kiswahili ya redio ya Umoja wa Mataifa (UN) jijini New York kuwa Bunge la Tanzania halina meno na hivyo limeshindwa kuiwajibisha ipasavyo serikali.
Lakini kwa mujibu wa Katiba, Bunge linatakiwa kupokea na kufanyia kazi ripoti ya ukaguzi wa CAG.
Tayari Prof Assad alishawasilisha ripoti ya ukaguzi wa hesabu kwa mwaka 2017/18 kwa Rais John Magufuli, na matakwa ya katiba yanataka ripoti hiyo iwe imewasilishwa Bungeni ndani ya siku saba baada ya Bunge kuanza. Bunge la bajeti lilianza mwanzoni mwa wiki iliyopita.
Macho na masikio ya watu nchini Tanzania yalielekezwa Bungeni iwapo ripoti hiyo ya CAG kama itawasilishwa Bungeni.
Hata Hivyo, Spika wa Bunge Job Ndugai wiki iliyopita alitoa ufafanuzi kuwa, azimio lilopitishwa na Bunge ni kutofanya Profesa Mussa Assad na si ofisi yake.
"Hakuna wakati wowote ambao Bunge limekataa kufanya kazi na taasisi ambayo ni ofisi ya CAG. Bunge hili limekataa kufanya kazi na mtu anayeitwa Profesa Assad basi. Tusiripoti tofauti tukauchonganisha umma na kuuchanganya," alisema Ndugai.
Mgogoro ulianzia mwezi Disemba ambapo Prof Assad aliiambia UN redio: "ā¦Kama tunatoa ripoti na inaonekana kuna ubadhilifu halafu hatua hazichukuliwi huo kwangu mimi ni udhaifu kwa Bunge. Bunge linatakiwa liisimamie (serikali) na kuhakikisha kuwa pahali penye matatizo basi hatua zinachukuliwa...Sie kazi yetu ni kutoa ripoti tu na huo udhaifu nafikiri ni jambo la kusikitisha lakini ni jambo tunaamini muda si mrefu huenda likarekebishika. Lakini tatizo kubwa tunahisi kwamba bunge linashindwa kufanya kazi yake kama inavyotakiwa."
Spika Job Ndugai aliagiza CAG ahojiwe mwezi Januari akidai kuwa amelidharau Bunge
Spika Ndugai alilieleza Bunge mwezi Januari kuwa maelezo ya Assad yalioonesha dharau kubwa dhidi ya mhimili huo na kumtaka aende mbele ya kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa hiyari yake, ama apelekwe kwa pingu.
Hata hivyo, alipohojiwa na kamati hiyo, Assad aliendeleza msimamo wake.
Kumekuwa na uungwaji mkono mkubwa kwa msimamo wa Prof Assad ambapo inaarifiwa kuwa watu zaidi ya 15,000 wamesaini waraka unaolitaka Bunge kufuta azimio lake.
Chama cha upinzani cha ACT kupitia umoja wake wa vijana ulipanga kufanya maandamano Jumanne lakini wakaahirisha baada ya kukatazwa na polisi
Maoni