Bakwata imerejesha umiliki huo baada ya kushinda kesi kufuatia halmashauri ya Jiji la Mwanza kushindwa kutimiza masharti iliyopewa na mahakama.
Shauri hilo namba 150 ya mwaka 2020 lililotokana na kesi namba 58 ya mwaka 2017 liliamuliwa Juni 3, 2022 ambapo Mahakama ilithibitisha kwamba kiwanja hicho ni mali halali ya Bakwata.
Akitoa taarifa kwa umma wa kiislam leo Juni 5, 2023 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Bakwata jijini Mwanza, Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Hasani Kabeke amesema katika uamuzi wake mahakama ilitoa masharti mawili kwa halmashauri ya Jiji ikitakiwa kulipa fidia ili kukitwaa kiwanja hicho ama irudishe kiwanja hicho kama fidia itashindwa kufikiwa ndani ya miezi mitatu, ambapo halmashauri hiyo ilishindwa kutekeleza yote mawili hadi leo Juni 5, 2023.
Amesema kiwanja hicho ni sehemu ya mali zilizokuwa zinamilikiwa na East Africa Welfare Society ambazo baadae zilihamishiwa Bakwata, ambapo Baraza hilo litaendesha dua maalum Juni 7, mwaka huu saa 4 asubuhi kupongeza maamuzi ya mahakama, kumuombea Rais Samia Suluhu Hassan na wazee waliotoa maeneo hayo kwa ajili ya jamii ya kiislamu.
"Tunajua ni wajibu wa mahakama kutenda haki lakini tunashukuru ili kutimiza maelekezo ya mtume wetu na kupaza sauti kuiombea mahakama Mungu awape uimara katika kuwatendea haki Watanzania kama ilivyofanya kwetu," amesema Kabeke
Kwa upande wake, Mhasibu wa baraza hilo, Said Mrisho amesema mahakama iliipa halmashauri ya Jiji la Mwanza sharti la kulipa fidia ya Sh 539 milioni kama inataka kutwaa eneo hilo baada ya uthamini kufanyika lakini imeshindwa kufanya hivyo, ambapo sasa litaendelea kuwa mali ya Bakwata.
Maoni