Kituo hicho kipya cha televisheni kimezua mjadala kuhusu wamiliki wake tangu kilipoanza matangazo ya majaribio, baadhi wakisema kinamilikiwa kwa asilimia 100 na nyota huyo wa Bongo Fleva.
Dar es Salaam. Ni Diamond Platnamuz au Joseph Kusaga?
Ndio mjadala mkubwa uliodumu tangu mwanamuziki huyo nyota wa miondoko ya Bongo Fleva aanze kukitangaza kituo kipya cha televisheni cha Wasafi TV.
Baadhi wanadai mmiliki ni Diamond na wengine wanasema Kusaga, mmoja wa manguli katika biashara ya burudani na ofisa mtendaji mkuu wa Clouds Media, wakidai anamtumia nyota huyo wa Bongo Fleva kutangaza televisheni hiyo mpya.
Wakati mjadala huo ukiendelea, Mamlaka ya Usimamizi wa Mawasiliano (TCRA) imetoa tangazo linalodokeza majibu ya mjadala huo.
Katika tangazo lake kwa umma kutaka maoni au pingamizi kuhusu maombi ya leseni ya Wasafi TV, mamlaka hiyo imewataja wamiliki watatu wa televisheni hiyo, ambayo tayari ipo hewani.
TCRA imemtaja mtu anayeitwa Juhayna Zaghalulu Ajmy na ambaye ni Mtanzania, kuwa anamiliki asilimia 53 ya Wasafi TV, akifuatiwa na Nasibu Abdul Juma, maarufu kama Diamond, kuwa anamiliki asilimia 45 na Ali Khatib Dai kuwa anamiliki asilimia mbili.
"Kwa mujibu wa Kifungu cha 8 cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta, Sura ya 306 ya Sheria za Tanzania, maoni ya maandishi yanakaribishwa kutoka kwa mtu anayeguswa kuhusu kutolewa leseni kwa mwombaji na yaifikie Mamlaka ndani ya siku 14 tangu kuchapishwa kwa tangazo hili," linasema tangazo hilo la mwezi Novemba.
"Maoni hayo yatazingatiwa wakati Mamlaka itakapokuwa ikifikiria kutoa leseni."
Kampuni ya Wasafi, ambayo pia inamiliki lebo ya muziki ya Wasafi, imeingia kwenye mvutano mkubwa na Clouds Media, ambayo inamiliki kituo cha televisheni cha Clouds TV na redio ya Clouds FM.
Clouds Media hujishughulisha zaidi na biashara ya burudani, ikiwa na kampuni ndogo zinazosimamia wanamuziki na studio za kurekodi muziki, kufundisha wanamuziki inayofanywa, hali kadhalika kuandaa matamasha ya muziki, kazi ambayo hufanywa na Primetime Promotions.
Hata hivyo, wengi wamekuwa wakichukulia mzozo huo kuwa ni kiini macho kutokana na kuhisi kuwa Kusaga, ambaye ni ofisa mtendaji mkuu wa Clouds Media, ana hisa katika televisheni ya Wasafi TV, hivyo ndugu wawili hawawezi kugombana.
Lakini tangazo la TCRA halijamtaja DJ huyo wa zamani, ingawa mmoja wa wamiliki waliotajwa, Juhayna Zeghalulu anahusishwa na umiliki wa Primetime Promotions na ni mzazi mwenza wa mmoja wa wamiliki wa Clouds Media.
Mzozo wa pande hizo mbili umesababisha nyimbo za Diamond kutochezwa na vituo vya Clouds, huku wanamuziki wakianza kujitofautisha kwa kutumia kampuni hizo mbili; wako wanaofanya kazi za Clouds Media pekee na wapo wanaofanya kazi za Wasafi.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, kampuni hizo mbili zilipambana katika sakata la uandaaji wa matamasha. Ingawa matamasha hayo mawili--Wasafi Concert lililofanyika Mtwara, na Fiesta Festival lililopangwa kufanyika Dar es Salaam yalikuwa mikoa miwili tofauti, upinzani mkali ulionekana katika matangazo hadi Serikali ilipozuia tamasha la Fiesta kutokana na sababu za kiafya.
Baada ya barua hiyo ya Serikali kusambaa mitandaoni, Diamond alituma video fupi inayomuonyesha akinywa soda. Na baada ya kushusha chupa, Diamond anaonekana akitoa kicheko kirefu, mithili ya mtu aliyeona mpinzani wake amefeli.
Zaidi ya sauti ya kucheka, video hiyo haina kitu kingine chochote, hali iliyotafsiriwa kuwa anachekeshwa na kitendo cha Fiesta kufutwa.
Clouds hawajazungumza zaidi ya kituo chake cha redio kucheza nyimbo za faraja, ukiwemo wenye maneno yasemayo "hauwezi kushindana na binadamu mwenye kinywa" wa Gozbert Goodluck, ambao huchezwa kila mara tangu Jumamosi.
Wakati baadhi ya wanamuziki wakiilalamikia Clouds kuwa inawabagua, Wasafi inajitangaza kuwa wanaleta "mapinduzi ya burudani".
Maoni