KUSAYA AONGOZA MAPOKEZI YA NDEGE YA ATCL MUSOMA
Musoma, Mara- Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Ndugu Gerald Musabila Kusaya, leo Septemba 17, 2026 ameongoza mapokezi ya ndege ya abiria ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) katika Uwanja wa Ndege wa Musoma, ikiashiria kurejea rasmi kwa safari za abiria baada ya takribani miaka minane.
Safari ya mwisho ya ndege ya abiria katika kiwanja hicho ilikuwa Machi 2018 ya Shirika la Precision Air, kabla ya kufungwa kupisha upanuzi na ukarabati.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mara wakati wa mapokezi hayo, Kusaya amesema kurejea kwa huduma hizo ni fursa muhimu kwa uchumi wa Mkoa wa Mara.
"Kurejea kwa ATCL ni fursa muhimu kwa wananchi kutokana na mchango wa usafiri wa anga katika kurahisisha usafirishaji wa watu na mizigo pamoja na kukuza biashara, utalii na uwekezaji," amesema Kusaya.
Kusaya ametoa shukrani kwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa wa kuboresha kiwanja hicho na kulipa fidia kwa wananchi 58 waliopisha ujenzi. Amewataka wananchi wa Mara na mikoa jirani kuitumia huduma hiyo kwa wingi ili kuhakikisha safari zinaendelea.
Kuhusu Ukarabati wa Kiwanja
Uwanja wa Ndege wa Musoma umepanuliwa na kukarabatiwa kwa gharama ya shilingi bilioni 36.3. Mradi huo ulianza mwaka 2018 na sasa umefikia hatua za mwisho. Miundombinu muhimu ikiwemo njia ya kutua na kuruka ndege (runway), maegesho ya ndege na maungio yake imekamilika kwa asilimia 100.
Serikali imesema kukamilika kwa uwanja huo ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha miundombinu ya usafiri wa anga nchini.
Ratiba ya Safari
Kwa mujibu wa ATCL, safari za Dar es Salaam - Musoma - Mwanza zitafanyika mara mbili kwa wiki, kila Alhamisi na Jumamosi, kwa kutumia ndege yenye uwezo wa kubeba abiria kati ya 78 na 80



Maoni