MTEULE THE BEST
Chama cha Jubilee, chake rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, kimepinga kundi la maafisa tisa wakuu wa Tume ya Uchaguzi nchini humo ambao wanatarajiwa kusimamia uchaguzi mpya mwezi ujao.
Chama hicho kimetoa orodha ya majina ya maafisa hao ambao kinasema wanajulikana kwamba "wanapendelea upande fulani".
Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi IEBC alitangaza kundi la maafisa saba watakaoongoza maandalizi ya uchaguzi utakaofanyika tarehe 17 Oktoba siku ya Jumanne.
Maafisa hao ambao wanajumuisha mkuu wa kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) na msimamizi wa kituo cha taifa cha kujumlishia matokeo watahudumu kwa miezi mitatu.
- Odinga apinga tarehe mpya ya uchaguzi Kenya
- Rais Kenyatta: Ni haki yangu kuikosoa mahakama
- Chama cha mawakili Kenya chamkosoa Uhuru Kenyatta
Mahakama ya Juu, ikifutilia mbali matokeo ya uchaguzi uliofanyika tarehe 8 Agosti ambapo Rais Kenyatta alitangazwa mshindi, iliiwekea lawama IEBC na kusema haikuandaa uchaguzi huo kwa njia na kwa kiwango kinachokubalika kikatiba.
Chama cha Jubilee kimesema: "Tuna habari za kuaminika kwamba kwenye orodha ya maafisa hao (watakaosimamia uchaguzi) kuna watu wanaofahamika wazi kuegemea upande Fulani."
"Ikizingatiwa makossa mengi ya kutotenda au ya kutenda ambayo yalichangia uchaguzi kufutiliwa mbali ambayo chanzo chake kilikuwa wafanyakazi wa IEBC, tunawasilisha pingamizi zetu kwa watu hawa tuliowataja hapa juu."
Muungano wa National Super Alliance (Nasa), ambao mgombea wake alikuwa waziri mkuu wa zamani Raila Odinga, ulikuwa umeitisha mabadiliko makubwa kwenye IEBC kabla ya uchaguzi mpya kufanyika.
Chama hicho kilisema hakitashiriki uchaguzi huo mpya iwapo mabadiliko hayatafanywa tume hiyo.
Haijabainika iwapo Bw Odinga na muungano wake wanakubaliana na majina ya watu walioteuliwa na Bw Chebukati.
Nasa hata hivyo wamepinga tarehe mpya iliyotangazwa na tume hiyo ya 17 Oktoba. Muungano huo umesema maafisa wa tume hawakushauriana nao kabla ya kutangaza tarehe hiyo.
Rais Kenyatta hata hivyo ameunga mkono tarehe hiyo na kusema hakuna hitaji la tume hiyo kushauriana na wanasiasa kabla ya kutangaza tarehe ya uchaguzi.
Bw Kenyatta, aliyekutana na viongozi wa kidini ikulu leo, amesema tarehe iliyotangazwa inafaa ili kutovuruga kalenda ya mitihani ya taifa ambayo imepangiwa kuanza mwishoni mwa mwezi Oktoba.
Maoni