Serikali yamfurusha Miguna Miguna na kumpeleka Canada
Mwanasiasa wa muungano wa upinzani nchin Kenya Nasa, Miguna Miguna amefurushwa na kupelekwa nchini Canada kupitia ndege ya KLM , kulingana na wakili wake Nelson Havi na Cliff Ombeta.
Bwana Ombeta amesema kuwa aliarifiwa kwamba bwana Miguna aliingizwa katika ndege iliokuwa ikielekea Amsterdam na baadaye kuelekea Canada.
Wakili mwengine Dkt. John Khaminwa alisema kuwa mteja wake tayari ameondoka Kenya.
"Ni kweli .Alilazimishwa kuingia katika ndege ya KLM dakika chache tu kabla ya saa nne usiku na tumebaini kwamba anaelekea Canada. Ni ukiukaji mkubwa wa haki'', alisema Dkt Khaminwa kwa simu.
Haijulikani ni sheria gani iliotumiwa na serikali kumuondoa nchini Kenya kwa kuwa katiba inampatia haki kama raia wa Kenya kwa kuwa ni mzaliwa wa taifa hilo.
Anasema kwamba wakati Miguna alipokamatwa , serikali ya Canada ilikuwa imeiandikia Kenya kionyesha wasiwasi kwamba raia wake alikuwa ananyanyaswa na walitaka arudishwe nchini humo.
Bwana Miguna siku ya Jumanne alielezea vile alivyokamatwa bila mawasiliano na familia yake ama wakili wake kwa siku tano.
Alisema kuwa maafisa wa polisi walimnyanyasa kwa kumfungia katika maeneo ambayo hayafai kwa binaadamu.
Bwana Miguna alikuwa akizungumza katika mahakama ya kajiado ambapo alipelekwa baada ya kukamatwa kwake siku ya Ijumaa kwa tuhuma za kushiriki katika sherehe ya kumuapisha kiongozi wa upinzani Raila Odinga ambaye aliapishwa kuwa rais wa wawananchi tarehe 30 Januari.
Ripoti za kufurushwa nchini Kenya zilijiri saa chache baada ya jaji wa mahakama kuu Luka Kimaru kumzuia mkurugenzi wa Ujasusi na inspekta jenerali wa polisi dhidi ya kumwekea mashtaka yoyote.
Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga akila kiapo cha kuwa rais wa wananchi
Jaji huyo awali alikuwa ameamuru kwamba inspekta jenerali wa polisi na mkurugenzi wa shirika la ujasusi walikuwa wamekiuka agizo la mahakama lililowataka kumwachilia kiongozi huyo.
Huku Jaji huyo wa Kajiado akiagiza awasilishwe mbele ya jaji Kimaru katika mahakama ya Milimani, bwana Miguna hakuwasilishwa katika mahakama hiyo huku mawakili wake wakilazimika kusubiri hadi usiku wakisubiri kuachiliwa kwake.
Miguna alikamatwa Ijumaa iliopita huku jaji wa mahakama kuu James Wakiaga akimwachilia kwa dhamana ya ksh. 50,000 lakini hakuachiliwa.
Mkurugenzi wa shirika la ujasusi baadaye alisema kuwa bwana Miguna alikamatwa baada ya kukiri kumpatia kiapo kiongozi wa Nasa Raila Odinga mbali na kuwa mwanachama wa kundi lililopigwa marufuku la NRM
Maoni