Tamko la Marekani na Uingereza linagusia kesi ya Erick Kabendera kama mfano wa hivi karibuni
Ubalozi wa Uingereza na Marekani nchini Tanzania wametoa tamko la pamoja kuhusu kile walichokiita "wasiwasi wa kuzorota kwa kwa haki za kisheria nchini Tanzania."
Katika tamko hilo, ofisi hizo mbili za ubalozi zinadai kuwa imedhihirika kwa zaidi ya mara moja watu kutiwa kizuizini kwa muda nchini Tanzania bila kupelekwa mahakamani na kubadilishiwa mashitaka na mamlaka zake za kisheria.
"Tuna wasiwasi hasa kwa tukio la hivi karibuni -- jinsi ambavyo halikushughulikiwa kwa haki la kukamatwa, kuwekwa kizuizini na tuhuma za mashtaka ya mwandishi wa habari za uchunguzi Bw Erick Kabendera, ikizingatiwa ukweli kwamba alinyimwa haki ya kuwa na mwanasheria kwenye hatua za awali na kutiwa kizuizini kwake, ambapo ni kinyume cha sheria ya makosa ya jinai," inasema sehemu ya tamko hilo.
"Tunaisihi serikali ya Tanzania kutoa hakikisho la mchakato wa kutenda haki kisheria kwa raia wake, kama ilivyotambua kwamba ni haki ya msingi na kuridhia kwenye mikataba mbali mbali ya haki za kibinaadamu ya Umoja wa Mataifa, miongoni mwao ikiwemo azimio la kimataifa la haki za kirai na kisiasa."
Erick Kabendera alipandishwa kizimbani Jumatatu ya wiki hii ikiwa ni wiki moja toka alipokamatwa na vyombo vya usalama nchini Tanzania.
Mwanahabari huyo meshtakiwa kwa makosa matatu ya ubadhirifu wa kiuchumi. Mosi anashtakiwa kwa kujihusisha na genge la uhalifu na uhujumu wa uchumi, pili kukwepa kulipa kodi ya zaidi ya milioni mia moja sabini za Kitanzania na tatu utakatishaji fedha zenye thamani ya zaidi ya millioni mia moja na sabini.
Kumekuwa na wasiwasi ndani na nje ya Tanzania kuhusu namna ambavyo amekamatwa, na taswira inayotokana na hatua hiyo kwa uhuru wa yombo vya habari nchini humo.
Pia baadhi ya wanaharakati wameonyesha kushangazwa na kubadilika kwa yaliominika kuwa ndio makosa anayotuhumiwa nayo.
Awali maafisa wa polisi na wale wa idara ya uhamiaji walisema anachunguzwa kuhusu utata wa uraia wake.
Baadae mawakili wake walitoa taarifa wakieleza mteja wao atashtakiwa kwa kuhusika na ripoti iliyochapiswha katika jarida la The Economist, lakini mahakamani kibao kikageuka tena na kuwa kesi ya ubadhirifu wa kiuchumi.
Makosa aliyoshtakiwa nayo hayana dhamana na ataendelea kusalia rumande mpaka mwisho wa kesi yake. Agosti 19, kesi hiyo inatarajiwa kusikilizwa tena mahakamani
Maoni