
Mmiliki mwenza wa Simba SC Mohammed Dewji anijtahidi kuona klabu hiyo inakuwa ndani na nje ya uwanja (Picha kwa hisani ya Mahmoud Bin Zubeiry)
Siku ya Jumanne mashabiki wa mojawapo wa timu kongwe Tanzania watakusanyika katika uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam kusherehekea "Simba Day".
Ni katika kuidhinisha wiki ya Simba au kwa umaarufu "Simba Week" na inahusisha mechi ya kirafiki dhidi ya Power Dynamos ya Zambia pamoja na mechi za timu za wanawake walio chini ya miaka 20.
Shughuli zilizopangwa kwa siku saba zimenuiwa kuongeza ukaribu na ushirikiano baina ya wachezaji na mashabiki wa timu hiyo pamoja na Simba kuisaidia jamii kupitia miradi tofuati.
Ni sehemu ya azimio la Bilionea Mohammed Dewji, mmiliki mwenza wa klabu hiyo anayeitaka klabu hiyo ikuwe ndani na nje ya uwanja ili kuhakikisha ufanisi zaidi.
"Niliwahi kukutana na mojawapo ya viongozi wa Zamalek (mnamo 2003) na niligundua wakati huo kuwa bajeti ya Zamalek ni mara 50 zaidi ya bajeti ya Simba," anaielezea BBC Sport."
"Naweza kuilinganisha na dereva anayeendesha Toyota na mwingine anayeendesha Ferrari - mtu hufanya awezalo."
Azimio la Dewji

Simba ilicheza dhidi ya Asante Kotoko ya Ghana mnamo 2018 "Simba Week" (Picha kwa hisani ya Mahmoud Bin Zubeiry)
Aliporudi Tanzania baada ya mashindano hayo ya ubingwa barani Afrika, Dewji alifahamu kuwa mambo yanahitaji kubadilika katika namna ambavyo klabu hiyo inaendeshwa iwapo inataka kushindana.
Kwa wakati huo, pendekezo lake la kubadilishi mfumo wa umiliki wa klabu hiyo, haukupokewa vizuri na alijitoa Simba mnamo 2004.
Miaka 11 baadaye, katika televisheni nchini humo alijadili atakachokifanya kuongeza mara tatu bajeti ya klabu hiyo, kuwekeza katika miundo mbinu na namna ambavyo wangeliliziba pengo katika kufikia klabu kubwa barani Afrika.
"Ilikuwa kama mzaha tu lakini Simba ilikuwa haifanyi vizuri na mzaha ukashika kasi," alifafanua.
Miaka miwili baadaye 'mzaha' huo ulimfanya shabiki sugu wa Simba arudi na kumiliki 49% ya hisa katika klabu hiyo.
Umiliki na mageuzi hayo yalioidhinishwa na wafuasi wa klabu ya Simba ulikuwa kama kivuko kuingia katika ufanisi wa klabu hiyo msimu uliopita.
Mnamo 2018 walifanikiwa kuidhinisha usajili wa wachezaji mahiri katika safari ya Uturuki na ilionuiwa kuimarisha ushindani wa klabu hiyo nchini na kimataifa.
Zaidi ya hapo walifanikiwa kuwekeza katika miundo mbinu msingi, ikiwemo ujenzi wa uwanja wa kisasa na wa kufanya mazoezi.

Hisia ya mashabiki wa Simba baada ya mchezo
Simba ilifikia malengo yake msimu uliopita - kwa kushinda katika ligi na kufika kiwango cha makundi katika ligi ya mabingwa, walifanikiwa zaidi kwa kufuzu katika robo fainali ya mashindano ya klabu barani.
Licha ya kufanikiwa kuiongeza bajeti ya mwaka zaidi ya mara mbili kwa klabu hiyo, Dewji anafahamu kuwa ipo kiwango cha chini ikilinganishwa na klabu nyingine barani zilizofanikiwa, lakini anaamini itazifikia kifedha katika miaka mitano ijayo.
"Miaka miwili iliyopita tumeongeza bajeti yetu mara mbili kutoka takriban $1m kwa mwaka hadi $2.5m," Dewji amefafanua.
"Tutashirikiana na makampuni kama Mohammed Enterprises na Total. Tunafahamu kuwa kila Mtanzania ni lazima anunuwe mafuta, mchele na sukari.
"Iwapo mashabiki watanunua bidhaa kutoka Mohammed Enterprises watapata punguzo la bei, na kwa upande wao, washirika watawapa thamani ya kutosha ya mauzo hayo."
Kuwaleta mashabiki

Simba imewahimiza mashabiki zaidi wajitokeze na kuinga mkono timu hiyo (Picha kwa hisani ya Mahmoud Bin Zubeiry)
Njia nyingine ambayo klabu hiyo inatumai kushindana ni kwa kuimarisha ushirikiano na mashabiki wake.
"Tunawavutia. Tumekusanya taarifa kuwahusu. Tumelenga thamani inayostahili katika suala la kiingilio," Dewji ameendelea kusema.
"Tumezusha shauku kubwa. Tumeidhinisha ukaribu na magazeti na vituo vya redio. Nadhani ndio mwanzo mkoko unaalika maua."
Simba imejaribu kuifanya soka iwe na bei nafuu na inayowavutia kila mtu aliye na fikra kama vile tiketi za gharama ya chini zinazo wavutia walio na kipato cha chini.
Wakati huo huo kuna tiketi za gharama ya juu - platinum level - kwa wanaojiweza na inayojumuisha fulana ya Simba, usafiri wa basi kwenda na kutoka uwanjani, na viti vya watu muhimu.
Shauku ya mashabiki wao 60,000 katika mechi za nyumbani zimewavutia watazamaji wengi wa soka Afrika.
"Nilikuwa ninazunguma na rais wa shirikisho la soka Caf Ahmad na amesema hajawahi kuona mashabiki wa Afrika wakijaza uwanja katika mechi za nje kama ilivyokuwa kwa Simba. Mpango wetu wa kuwa na uwazi una manufaa."
Uwazi huo umehimiza ushirikiano wa karibu baina ya mashabiki na Dewji amesisitiza umuhimu wa hilo kwa wanachama wa bodi yake.
"Simba ni klabu kubwa. Ni nembo kubwa," aliongeza.
" Ni jukumu letu kama viongozi wa klabu hii na kama mmiliki wa klabu hii kwamba A) tuwe na maadili katika tunachokifanya B) Tunahitaji kuwa na uwazi mkubwa katika tunachokifanya na C) tunahitaji kuwasiliana na mashabiki wetu kupitia vyombo vya habari kufafanuwa azimio letu ni lipi."
Ushawishi wa Simba kwa timu ya Taifa

John Bocco wa Simba ni moja kati ya wanne katika kikosi cha klabu hiyo Tanzania katika kombe la mataifa ya Afrika
Ufanisi wa Simba umeathiri pia timu ya taifa ya Tanzania wakati Taifa Stars ilipofuzu kwa mara ya kwanza katika miaka 39 kushiriki fainali za kombe la mataifa ya Afrika.
Dewji aliongoza kamati iliyohakikisha mechi muhimu ya kufuzu kwa Tanzania dhidi ya Ugnada ilipata uungwaji mkono mkubwa wa mashabiki.
"Kuwaona mashabiki wengi kulitupatia nguvu ya kwenda na kupambana na kufuzu," alisema mchezaji wa kiungo cha kati wa timu hiyo ya taifa Himid Mao, anayeichezeka klabu ya Misri Petrojet.
"Tulipokuwa njiani tukielekea uwanjani, tukawaona mashabiki wengi ilitufanya tuhisi kama tuna deni la kuwalipa."
Mpango ulifanikiwa huku mashabiki wakiwashangilia, timu hiyo ilipata ushindi wa 3-0 ikiwemo mkwaju wa penalti wake Ernesto Nyoni wa klabu ya Simba dhidi ya majirani zake na kufanikiwa kufuzu katika mashindano hayo nchini Misri.
Nyoni wa Simba ni moja kati ya wanne waliocheza katika kikosi cha Tanzania katika kombe la mataifa ya Afrika nchini Misri akiwemo pia Kipa John Bocco, Aishi Manula, na mchezaji wa ziada Mohamed Hussein.
Na kulikuwa na wachezaji wawili pia wa Simba katika kikosi cha Uganda nchini Misri, nao ni Murushid Juuko na Emmanuel Okwi, ambaye ameondoka kujiunga na Al Ittihad ya Misri.
Matumaini ya Simba sasa ni kushinda katika ligi ya mabingwa na kwa mkono wa biashara wa Dewji anayeushikilia usukani, gari hilo ambalo halikuweza kushindana katika siku za nyuma, linaonekana kusogea katika muelekeo mzuri na linashika kasi
Maoni