MTEULE THE BEST
ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani (DMP), ameshindwa kujisafisha dhidi ya tuhuma kuwa amezini na mchungaji wake,
Askofu Dk. Alex Malasusa, anatuhumiwa anatuhumiwa kujihusisha kimapenzi na mchungaji wa kanisa hilo ambaye ni mke wa mtu, Leita Ngowi.
Akizungumza kwenye mkutano wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), mjini Dodoma, Alhamisi wiki hii, Askofu Dk. Malasusa ameishia kusema, “kuchafuliwa kwangu ni vita maalum ya watu wa Kaskazini wakiongozwa na maaskofu wao.”
Amesema, chanzo cha kuchafuliwa kwake kunatokana na hatua yake ya kukataa kumuunga mkono aliyekuwa mgombea wa urais UKAWA, waziri mkuu mstaafu, Edward Lowassa.
Alisema, “unajua wenzetu kule Kaskazini wote ni UKAWA. Sasa mimi nilikataa upuuzi huo wakanichukia.”
Mtoa taarifa wa gazeti hili amesema, kabla ya kwenda Dodoma, Askofu Dk. Malasusa alinukuliwa akisema, jitihada za kumchafua zinaendeshwa na baadhi ya viongozi serikalini na ndani ya kanisa.
Anasema, baadhi ya maaskofu wenzake wa kanisa hilo, hasa wale wanaotoka ukanda wa Kaskazini, walipomuona anaunga mkono John Pombe Magufuli, aliyekuwa mgombea urais kupitia CCM, waliamua kumshtaki kwa Reginald Mengi na Lowassa.
Aidha, Askofu Dk. Malasusa alimtuhumu maaskofu wengine wa Kanda ya ziwa Victoria, akiwamo Askofu mmoja (jina linahifadhiwa), kuwa ndiye kinara wa yeye kuchafuliwa.
Anasema, Askofu huyo ambaye anaonekana kuwa na nguvu ndani ya kanisa hilo amekuwa na chuki binafsi dhidi yake.
Kuibuka kwa Askofu Dk. Malasusa, kutuhumu maaskofu na viongozi wengine wa kisiasa nchini, kumekuja wiki moja baada ya Mchungaji Leita kunusurika kifo.
Mchungaji huyo anayedaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Askofu Malasusa, alinusurika kifo wiki mbili zilizopita, baada ya jaribio lake la kutaka kujiua kwa kutumia sumu kugonga mwamba.
na Leita Ngowi, mchungaji na mkurugenzi wa idara ya wanawake usharika wa Azania Front, jijini Dar es Salaam anadaiwa kutaka kujiua baada ya Askofu Malasusa kulazimisha uongozi wa kanisa lake kumpa likizo ya lazima mchungaji wake.
Leita Ngowi, ni mke wa Venance Mwakilima, mkazi wa eneo Vikawe, Bagamoyo, ambaye ni mfanyakazi wa Shule ya Msingi Dunda.
Akizungumza katika mkutano huo wa viongozi wa kiroho, Askofu Dk. Malasusa ametaja maaskofu wawili kutoka ukanda wa Kaskazini, kuwa ndiyo wanaoendesha kampeni za kumchafua.
Anasema, sababu ya maaskofu hao kumchafua inatokana na kukasirishwa na hatua yake ya kuwakatalia kuwa warithi wa nafasi yake ya ukuu wa kanisa.
Amesema, “tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa kanisa letu, maaskofu hao wa Kaskazini wamekuwa wakinichukia; na nilipoona huu uchafu magazetini nilijua kuwa watakuwa ni wahusika wakuu, kwa sababu kila mmoja alitaka kuwa mkuu wa kanisa. Nimekataa.”
Mtoa taarifa anasema, taarifa kuwa Askofu Malasusa anatuhumu watu wa Kaskazini kumchafua, tayari zimetinga kwa mkuu wa sasa wa kanisa hilo, Askofu Dk. Fredrick Shoo; ambapo alilazimika kufanya safari hadi jijini Dar es Salaam kwa lengi la kukutana na Malasusa.
Hata hivyo, Askofu Malasusa aligoma kukutana na mkuu wake, Dk. Shoo kwa madai kuwa hata yeye ni mtuhumiwa kwa sababu ni rafiki wa karibu wa “wabaya” wake.
“Kwa kweli ndugu yangu, Baba Askofu Shoo amelazimika kusafiri hadi Dar es Salaam kukutana na Malasusa ili kuzungumza mambo haya. Lakini ameshindwa kumuona.
“Askofu Malasusa amekataa Dk. Shoo kufika ofisini kwake Luther House; badala ya majadiliano mengi na baadhi ya watu kuingilia, ndipo Askofu Malasusa aliamua kumfuata Askofu Shoo hotelini akiwa ameambatana na mkewe,” ameeleza.
Naye Dk. Shoo ananukuliwa na mtoa taarifa akisema, “…ni kweli nilitaka kuonana na Baba Askofu Malasusa. Lakini alipofika na mkewe hotelini kwangu, nimeshindwa namna ya kusema naye. Nimeishia kumpa pole na akaondoka kwa manunguniko makubwa.” Hakufafanua.
Maoni