Ruka hadi kwenye maudhui makuu

Mabadiliko ya Simba, Yanga na kukodi lori la mchanga

MTEULE THE BEST




KWA muda mrefu kumekuwa na sauti zinazopazwa na watu wa kada mbalimbali wakikosoa na kutaka mabadiliko makubwa kwenye mfumo wa uendeshaji wa klabu kongwe za soka nchini za Simba na Yanga.
Msingi wa ukosoaji umekuwa ukijikita katika ukweli ulio wazi kwamba, pamoja na klabu hizi kuwa kongwe kwa zaidi ya nusu karne bado hakuna mafanikio ya maana yaliyofikiwa iwe ni katika malengo ya kuanzishwa kwao kisoka na hata kiuchumi.
Mathalani, tangu kuanzishwa kwa klabu hizi hakuna hata moja iliyofanikiwa kutwaa ubingwa wowote wa michuano mikubwa ya Afrika inayoendeshwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf). Mara zote tangu enzi za uwepo wa mashindano ya Klabu Bingwa Afrika mpaka Ligi ya Mabingwa ama Kombe la Washindi, Kombe la Caf mpaka sasa Kombe la Shirikisho zimekuwa wasindikizaji tu.
Mafanikio pekee makubwa ni Simba kufikia nusu fainali za Klabu Bingwa mwaka 1974, kisha kucheza fainali za Caf mwaka 1993 na kucheza makundi Ligi ya Mabingwa 2003, huku Yanga rekodi kubwa ni kucheza robo fainali tatu tofauti za Klabu Bingwa 1969 na 1970 na ile ya Kombe la Washindi mwaka 1995 kabla ya kutinga makundi mara mbili Ligi ya Mabingwa 1998 na Kombe la Shirikisho mwaka huu.
Mfumo tatizo
Aidha, katika eneo la menejimenti na uendeshaji wa klabu hizo bado kumekuwa  na matatizo lukuki ambayo kimsingi ndiyo chanzo cha kushindwa kufikia mafanikio katika soka la Afrika.
Zinaendelea kuendeshwa kwa mfumo wa uanachama ambao katika hali ya sasa hauwezi kabisa kukidhi changamoto zinazojitokeza.
Soka la sasa linahitaji misuli ya kiuchumi kiasi kwamba michango ya wanachama na makusanyo ya mapato getini hayawezi kabisa kusaidia chochote zaidi ya kutatua gharama ndogo ndogo. Mfumo huu ni wa utegemezi, unatengeneza matundu mengi katika kuendesha klabu hizi.
Ni mfumo ambao hakika ndio chanzo cha mkwamo wa klabu zetu nyingi zilizowahi kutamba huko nyuma. 
Itoshe kusema kwamba mfumo huu ndio sasa umekuwa chanzo cha kuzalisha ‘miungu watu’ ndani ya klabu hizo. Kila anapojitokeza mtu mwenye uwezo wa kifedha na akaonesha kujiweka karibu na klabu hizi hata kwa maslahi yake binafsi ataonekana mwokozi.
Neno lake huwa sheria na ndilo hufuatwa. Anaweza kutoa amri zozote na asipingwe na yeyote hata kama ni fyongo.
Tatizo zaidi
  • Miungu hawa wamekuwa na nguvu hata ya kuamua hatma ya timu zinapocheza uwanjani. Ndio wanaosajili na kupanga wachezaji uwanjani. Ndio wanaoamua ushindi wa timu zao kupitia kuwamiliki wachezaji na kuwaelekeza nini wafanye uwanjani. Wanawekeza rasilimali na fedha kuwaridhisha mashabiki kupitia ushindi wa uwanjani, huku klabu zikiwa hoi bin taabani kwenye akaunti.
Baadhi ya wanachama wenye njaa zao nao hawako nyuma katika kutumia mfumo huu kujinufaisha. Wataanzisha migogoro ili wazimwe kwa fedha. Wengine wameshajipachika kazi ya ukusanyaji na usimamizi wa mapato ya getini. Mapato haya ya getini yamekuwa yakiishia mikononi mwao huku klabu zikifa njaa.
Kwa ujumla mfumo wa wanachama katika uendeshaji klabu za soka umepitwa na wakati, haufai na hauna tija katika maendeleo ya soka la kisasa. Haishangazi kelele na ukosoaji kuongezeka katika kudai mabadiliko makubwa katika mfumo huu.
Mabadiliko lazima
Hata hivyo, kuna maswali kadhaa ya kujiuliza. Je, wanachama wa klabu hizi wamezisikia kelele hizi za mabadiliko ya mfumo na wako tayari au wamesukumwa tu? Je, kama wameafiki, mabadiliko haya yanapaswa kuongozwa na watu gani? Na mabadiliko hayo ni yepi hasa? Wanachama wanayaelewa na wako tayari kwa matokeo? Je, kuna utafiti na upembuzi wa kina umefanywa katika kuyafikia mabadiliko hayo?
Lazima ieleweke kwamba ili mabadiliko yoyote ya klabu yafanyike lazima yaanze na mfumo wa umiliki kwa maana ya wamiliki kuwa tayari kuridhia kwa kushirikishwa ipasavyo mwanzo mwisho. Kwa maana hiyo kwa Simba na Yanga ambazo mfumo wake wa umiliki ni wa wanachama lazima kuwe na maridhiano ya pamoja katika kuyafikia mabadiliko ya klabu.
Hivi ndivyo kwa mfano ilivyoanza miaka ile ya tisini kulipoibuka kambi za Yanga Kampuni na Yanga Asili. Majadiliano yalifanyika kwenye vikao ingawa ilikuwa katika hali iliyokuwa inatishia uhai wa timu yenyewe ya Yanga maana kulikuwa na hatari ya mgawanyiko na kupasuka kwa klabu ya Yanga katika makundi haya mawili.
Msingi wa ushirikishwaji wa wanachama bila kuwashurutisha ni wa muhimu sana katika kuendea mabadiliko ya klabu hizi maana pamoja na changamoto zote za miaka yote bado wamesimama na klabu hizi na kuzisimamisha katika hadhi ya chapa (brands) zinazovuma kuliko nyingine zozote nchini.
Elimu muhimu
Kwa kuwa wanachama hawa ni mchanganyiko, wenye uelewa na elimu tofauti kulikuwa na sababu za msingi kuwaelimisha na kuwafahamisha hatua kwa hatua kile kinachoendelea sasa cha mabadiliko ya kiuendeshaji ya klabu hizi.
Ukweli ni kuwa klabu hizi za Simba na Yanga ukiacha suala la sokauwanjani ni vitega uchumi na fursa muhimu kwa mfanyabiashara yeyote mwenye kutafuta mafanikio ya kibiashara. Uwingi wa wanachama na mashabiki wake, idadi kubwa ya watazamaji wa mechi zao ni fursa ya mafanikio kwa mfanyabiashara yeyote makini.
Hivyo umuhimu na fursa nyeti za kibiashara (Business Potentiality) zilizogandana na klabu hizi zinawafanya wanachama wawe na kila sababu ya kuringa na kutembea vifua wazi dhidi ya mtu yeyote. Hawapaswi hata kidogo kutishiwa na kupelekeshwa na mihemuko ya mfanyabiashara yeyote maana wao ndio wenye mali tena iliyo adhimu.
  • Wengi tulitegemea uwekezaji na mabadiliko kwenye mfumo wa uendeshaji wa klabu hizi utazingatia misingi ya kibiashara kwa maana ya kuainisha na kuzingatia aina mbalimbali za ubia katika uendeshaji wa vitega uchumi kama vilivyo vitega uchumi vingine vyovyote.
Aina ya uwekezaji
Mathalan, msingi mkubwa wa kwanza wa kumpata mwekezaji au mbia ni kwa kutangaza zabuni ya wazi yenye kuainisha masharti au vigezo mbalimbali kulingana na mahitaji ya klabu. Hata hivyo, hili halikuzingatiwa katika yanayoitwa mabadiliko yaliyotangazwa juma lililopita. Kilichoshuhudiwa ni wafanyabiashara kuja na matamanio yao pekee.
Jambo la pili la msingi ni kwamba, mwekezaji au mbia lazima aje na mtaji wake na aeleze namna gani atauwekeza na kuhakikisha faida inapatikana. Hasara huwa haizungumzwi maana mwekezaji anakuwa ameshapiga hesabu zake vema na kubaini nini atavuna. Bahati mbaya uwekezaji kwa klabu ya Simba ulitajwa wazi wakati ule wa Yanga hadi kesho haufahamiki. Uko kwenye mabano na hakuna aliyehoji. Hata ule uwekezaji wa Simba uliotajwa bado watu makini wanahoji thamani yake ukilinganisha  na ile ya klabu.
Jambo la tatu ni namna ya uendeshaji wa kitega uchumi kwa maana ya klabu zenyewe. Kuna njia tatu katika hili. Mosi, kumkabidhi kila kitu mwekezaji na yeye kuleta faida kulingana na makubaliano. Hii haijalishi mwekezaji kapata faida au la. Pili, kumkabidhi sehemu ya uendeshaji huku klabu ikiendeshwa kwa pamoja. Hapa faida hugawanywa kulingana na kiwango kilichokubaliwa.
Njia ya mwisho katika uendeshaji, ni kuuza umiliki na kumkabidhi mwekezaji. Hapa wamiliki kwa maana ya wanachama hawana chao, maana wanakuwa wamekabidhi kila kitu. Hawana haki yoyote. Umiliki wa klabu unahamia kwa mwekezaji baada ya kulipa fedha za manunuzi.
Ukweli ulivyo
Ukiziangalia njia zote tatu utaona wazi kuna matege katika kile kilichoitwa mabadiliko ya uendeshaji wa klabu kongwe. Ukiacha ukweli mchungu kwamba wanachama watabaki wanakodoa macho tu uwanjani (ndivyo inavyopaswa iwe ila wengi wao hawaelewi) bado uhalisi wa mapato utabaki kuwa ndoto.
Hatujajua menejimenti za klabu hizi zitakuaje, ila ni wazi kwa mabadiliko haya ya kibiashara itabidi wanachama wakae kando na wawekezaji waajiri wataalamu wa kufanya kazi. Kwa maana hiyo kama uendeshaji hautachorwa vema ni wazi kuna hatari ukawa mwanzo na mwisho wa wanaojiita wanachama kujua nini kinaendelea katika klabu zao hasa Yanga ambayo imeingia kwenye mfumo wa kukodi huku anayekodishwa akishindwa kutaja kiasi anachokodishwa na kuweka msimamo tata kuhusu urejeshaji wa faida baada ya kukodishwa.
Kwa kawaida dhana ya kukodi huanza kwa mwenye kukodishwa kulipa fedha za kukodishwa. Aidha, suala la hasara au faida haliwezi kuwa juu ya mkodishaji bali mkodishwaji.
Ni sawa na anayekodi lori la mchanga halafu umwambie mwenye lori utamlipa utakapopata faida. Hadi ufikie hatua ya kukodi ushapima faida na hasara.  Simba na Yanga zina fursa (potentiality) kubwa kuliko yanayotokea sasa. Zimejengwa kwa machozi, jasho na damu hadi kufikia kuwa brands kubwa pengine nambari moja nchini. Umakini katika ubia na maandalizi ya muda mrefu yalihitajika.
Muhimu
  • Jambo moja wanachama wa klabu hizi hawajalewa ni kwamba sasa inabidi wakae kando waache wawekezaji wafanye kazi. Wao watabaki na hisa tu ambazo kama ilivyo kwa timu kubwa za Ulaya na kwingineko haziwapi mamlaka kuingilia mwenendo wa timu vinginevyo hisa ziwe nyingi kiasi cha kumpiku kauli ‘bwana mkubwa’.
Aidha, wanachama inabidi waelewe kwamba udhibiti wa klabu hizi utakuwa mkubwa na utaathiri maslahi ya baadhi yao ili klabu hizi ziwe na misuli ya kiuchumi. Wengi wanaweza kuona mabadiliko haya ni kawaida lakini yana mshindo mkuu.
Pamoja na matege ya mchakato ulipopitia, mabadiliko haya ni mema kama yatachorewa mistari na kuwekewa mikataba makini itakayosimamiwa na pande zote. Hata hivyo, bado naona kiza totoro mbele kwa wanachama ambao inabidi waelewe dhana hizi mpya. Siamini tutavuka. Tusubiri tuone, muda si mrefu.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Urusi: Vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini havitafua dafu

MTEULE THE BEST Image caption Waziri wa maswala ya kigeni nchini Urusi Sergei Lavrov na mwenzeka wa Marekani Rex Tillerson Waziri wa maswala ya kigeni nchini Urusi Segei Lavrov amemwambia waziri wa ulinzi nchini Marekani Rex Tillerson kwamba kuiwekea vikwazo zaidi Korea Kaskazini hakutafua dafu. Taarifa iliochapishwa na wizara ya kigeni nchini Urusi inasema kuwa wawili hao walizungumza kwa njia ya simu na kushutumu majaribio ya makombora ya hivi karibuni yaliotekelezwa na Pyongyang . Lakini inasema kuwa bwana Lavrov alisisitiza kwamba diplomasia ndio njia ya pekee ya kumaliza wasiwasi katika rasi ya Korea, na kutaka hatua zozote dhidi ya taifa hilo kusitishwa akionya huenda zikasababisha madhara yasiojulikana. Waziri wa ulinzi nchini Marekani amesisitiza kuwa bado kuna fursa ya kidiplomasia katika kukabiliana na Korea Kaskazini. Mapema rais Trump alichapisha ujumbe katika akaunti yake ya Twitter akisema mazungumzo sio suluhisho.

*DKT. MAGUFULI, MNANGAGWA WAWEKA HISTORIA MPYA*

Rais wa Zimbabwe, Emerson Mnangagwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli Rais wa Zimbabwe, Emerson Mnangagwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli wameweka historia mpya kwa kukubaliana kushirikiana kwenye maeneo makuu matatu yenye tija pande zote. *Kwanza*, *Kuimarisha uchumi* wa nchi hizi mbili kwa kukuza uwekezaji na biashara ambao umeanza kuonesha matunda makubwa. Mathalani, katika eneo la biashara kumeonyesha mafanikio makubwa kila mwaka. Mfano mwaka 2016 biashara kati ya Tanzania na Zimbabwe ilikuwa ni Tsh. Bilioni 18.3. Mwaka 2017 biashara ilikuwa Tsh. Bilioni 21.1. *Pili*; *kushirikiana* vyema kwenye masuala ya *utalii* kwa kutumia wingi wa vivutio vya utalii kama vile mbuga za wanyama, fukwe, maeneo ya kihistoria pamoja na Mlima Kilimanjaro. *Tatu*; Kushirikiana na kuimarisha eneo la *huduma za kijamii* zikiwemo afya, utamaduni, elimu na kukuza lugha ya kiswahili ambapo Tanzania ina Waalimu wa kutosha na hivyo...

MAPENZI: Kuna faida na ni muhimu Mpenzi wako kuwa rafiki yako pia

Kuna faida kubwa kwa wapenzi kuwa marafiki KUTOKANA na mila mbalimbali, baadhi ya watu wamekuwa wakiamini kwamba mwanamke ni daraja la pili. Daraja la kwanza na lenye kuthaminiwa ni mwanaume. Yaani mwanamke hana kauli kwa mwanaume. Anakuwa kama mtumwa fulani hivi.  Mwanaume akiongea, basi ni maelekezo kama vile rais wa nchi anavyotoa maelekezo kwa watu walio chini yake. Hakuna wa kupinga. Akisema sitaki kitu fulani kifanyike, basi ni mpaka atakapotoa maelekezo mengine. Vinginevyo, maelekezo ya awali yatabaki kusimama kama sheria.  Wapo baadhi ya wanawake wanaofurahia aina hii ya uhusiano kwa sababu ya mazoea. Kwamba wamekuzwa hivyo, mwanaume ni mwanaume. Huu ni mfumo ambao watu wengi wamekuwa wakiuishi. Kuna ambao wanakubaliana nao, wengine hawakubaliani nao.  Watu wengi sana wamekuwa wakiishi katika malumbano katika mahusiano yao kutokana na mfumo huu wa maisha. Mwanamke hataki kuishi kama mtumwa, mume anakomaa kuonesha uanaume wake. Hakuna anayekubali kushuka,...