MTEULE THE BEST
Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki,yuko ziarani nchini Urusi kwa lengo la kuanzisha " enzi mpya ya uhusiano" pamoja na rais Vladimir Putin wakati ambapo uhusiano wa Uturuki na nchi za magharibi umeingia madowa.
Rais wa Urusi Vladimir Putin na mwenzake wa Uturuki Tayyip Erdogan walipokutana 23.09.2015 mjini Moscow
Ziara ya Erdogan katika mji alikozaliwa Vladimir Putin-Saint Petersburg ni ya kwanza pia kufanywa nchi za nje na rais huyo wa Uturuki tangu njama iliyoshindwa ya mapinduzi dhidi yake mwezi uliopita,njama iliyosababisha wapinzani wake kadhaa kutiwa ndani na kuzusha kiwingu katika uhusiano wa nchi hiyo na nchi za magharibi.
Rais Vladimir Putin amepangiwa kukutana na mgeni wake wa kutoka Ankara,saa saba mchana kwa saa za Afrika Mashariki katika kasri la Konstantinovsky,umbali wa kilomita 15 kusini mwa Saint Petersburg. Mkutano na waandishi habari utafuatia mwishoni mwa mazungumzo hayo saa kumi jioni.
Uhusiano mwema kati ya uturuki na Urusi utasaidia kuifumbua mizozo tofauti
"Ziara hii inafungua ukurasa mpya katika uhusiano wa pande mbili " amesema rais Erdogan katika mahojiano na vyombo vya habari vya Urusi."Nchi zetu ni wadau muhimu katika eneo hili na kuna mengi tunayoweza kuyatekeleza kwa pamoja" amesisitiza.
Hoja kama hizo zimetolewa pia nchini Urusi ambako mshauri wa ikulu ya Kremlin,Iouri Ouchakov amesema anategemea "mazungumzo yenye umuhimu mkubwa". Mada mazungumzoni ni pamoja na kuimarishwa hatua baada ya hatua uhusiano jumla kati ya Urusi na Uturuki,pamoja pia na hali nchini Syria amesema mshauri huyo wa Kremlin.
"Ile hali kwamba Erdogan anakuja Saint Petersburg,muda mfupi baada ya njama iliyoshindwa ya mapinduzi "ni ushahidi kwamba waturuki wamedhamiria kwa dhati kuimarisha uhusiano pamoja na Urusi-ameongeza kusema Iouri Ouchakov.
Vladimir Putin alikuwa miongoni mwa viongozi wa mwanzo wa kigeni kuzungumza kwa simu na Erdogan,kulaani njama hiyo ya maapinduzi. Hata kama uhusiano kati ya Moscow na Ankara "si madhubuti hivyo, ile hali ya kuharibika uhusiano pamoja na nchi za magharibi inaweza kuharakisha hali ya kujongeleana Uturuki na Urusi-anasema mchambuzi wa baraza la Ulaya linaloshughulikia uhusiano na nchi za nje.
Ujerumani inakaribisha hali ya kujongeleana Uturuki na Urusi
Katibu wa dola katika wizara ya Mambo ya nchi za nje ya Ujerumani ,Gernot Erler
Hata hivyo maafisa wa serikali ya Ujerumani wanahisi uhusiano kati ya Uturuki na Urusi ni jambo la maana na wala si kitisho cha kuitenganisha Uturuki na jumuia ya kujihami ya NATO."Ni kwa masilahi ya Ulaya ikiwa uhusiano utaimarika kati ya Uturuki na Urusi,kwasababu uhusiano huo utasaidia kuimarisha juhudi za kusaka ufumbuzi mizozo nchini Syria na katika eneo la Caucasus" amesema hayo mshauri wa serikali kuu anaeshughulikia masuala ya uhusiano pamoja na Urusi,Gernot Erler.
Maoni