MTEULE THE BEST
Kila upande katika vita vya kuwania mji wa Aleppo, serikali na waasi, umejiimarisha kwa wapiganaji zaidi na silaha, katika kile kinachochukuliwa kuwa mapambano ya mwisho kuudhibiti mji huo muhimu wa Kaskazini mwa Syria.
Wapiganaji wa Jaish al-Fatah katika mapambano mjini Aleppo
Mkuu wa Shirika la Kuchunguza Haki za Binadamu nchini Syria lenye makao nchini Uingereza, Rami Abdel Rahman amesema wapiganaji wapya wapatao 2000, wakiwemo wasyria, wairaq, Wairan na wanamgambo wa Hezbollah kutoka Lebanon wameingia mjini Aleppo jana usiku, kushiriki katika mapambano yanayozidi kupamba moto mjini humo.
Aidha, gazeti la al-Watan linaloegemea upande wa serikali ya Syria limeandika leo kuwa jeshi na washirika wake wamepata msaada wa kutosha kukomboa maeneo lililoyaachia. Gazeti hilo limesema kundi la wanamgambo wa kipalestina lenye mafungamano na serikali ya mjini Damascus limepeleka msaada mkubwa kusaidia wanajeshi wanaokilinda kiwanda cha seruji Kusini mwa Aleppo.
Al-Watan limevinukuu vyanzo kutoka uwanja wa vita, ambavyo vimesema kuwa ndege za kivita zimefanya mfululizo wa mashambulizi dhidi ya ngome za waasi.
Kila upande wajizatiti
Vikosi vitiifu kwa rais wa Syria Bashar al-Assad vinasonga mbele kukabiliana na muungano wa wapiganaji wa kijihadi, ambao Jumamosi waliyakamata maeneo yanayozunguka chuo cha kijeshi cha Aleppo, na kuuvunja mzingiro wa serikali kwenye wilaya za Mashariki wanakoishi watu takribani 250,000.
Abdel Rahman wa shirika la kuchunguza haki za binadamu nchini Syria, amesema pia kuwa mamia ya wapiganaji waasi kutoka kundi la Fateh al Sham, ambao zamani walikuwa tawi la mtandao wa al-Qaida, wamewasili mjini Aleppo wakitokea sehemu nyingine za mkoa na pia kutoka mkoa wa Idlib.
Fateh al-Sham ambayo siku za nyuma ilijulikana kama al-Nusra Front kabla ya kujitenga na al-Qaida, inaongoza Jeish al-Fateh, au Jeshi la Ushindi linachangia pakubwa katika vita mjini Aleppo.
Aleppo, Mji uliogawika
Mji wa Aleppo ambao kabla ya kuanza kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe ulikuwa ndi wenye idadi kubwa zaidi ya wakazi nchini Syria hivi sasa umetengwa katika sehemu mbili, moja ikiwa chini ya udhibiti wa serikali, nyingine ikiwa imechukuliwa na waasi.
Mji wa Aleppo umetengwa katika sehemu mbili; ile iliyo chini ya serikali, na ile inayodhibitiwa na waasi
Rais Bashar al-Assad amepania kuukomboa kabisa mji huo,akisaidiwa na ndege za kijeshi za Urusi na wanamgambo wa Hezbollah kutoka Lebanon.
Hatua ya waasi kuyakamata maeneo zaidi ya mji huo inaweza kubadilisha urari wa nguvu za kijeshi, baada ya mafanikio ya jeshi la serikali mwanzoni mwa mwezi Julai, ambayo yalichukuliwa kama mwanzo wa kuukomboa kabisa mji wa Aleppo.
Kamanda mmoja wa cheo cha juu wa wa kundi la Fateh Halab Abu al-Hasanien, amesema wamejichimbia katika mahandaki kwenye eneo la Ramousah, wakikabiliwa na mashambulizi makali ya anga.
Ikiwa serikali ya Syria itaweza kuukomboa mji wa Aleppo, hilo litakuwa pigo kubwa kwa waasi.
Maoni