Serikali ya Tanzania imetetea hatua yake ya kuwakamata na kuwapiga mnada mifugo pamoja na kuteketezwa kwa vifaranga kutoka nchi jirani ya Kenya.
Wafugaji wa jamii ya Wamaasai kutoka Kenya wamekuwa wakivuka mpanga na kuingia Tanzania kutafuta malisho
Serikali ya Tanzania imetetea hatua yake ya kuwakamata na kuwapiga mnada mifugo pamoja na kuteketezwa kwa vifaranga kutoka nchi jirani ya Kenya.
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imesema kupitia taarifa kwamba Tanzania ilifuata utaratibu uliopo kisheria na kwamba mataifa hayo mawili yamekuwa yakiwasiliana.
Waziri wa mambo ya nje nchini Kenya Amina Mohamed ameilalamikia serikali ya Tanzania kufuatia hatua ya taifa hilo.
''Tulidhani kwamba mazungumzo ya kidiplomasia yangetatua mzozo huu, lakini tulishindwa kuafikia makubaliano. Ni wakati huo ambapo tuliamua kuzungumza na balozi wetu nchini humo kuwasilisha barua ya kupinga hatua ya kuwapiga mnada mifugo hao''.
''Historia ambayo tumekuwa nayo na Watanzania ni nzuri sana na kila kunapotokea tatizo tumekuwa tukitatua.Ni kwa sababu hiyo ambapo imekuwa hatua ya kushangaza miongoni mwa wafugaji wa Kenya'', waziri huyo alizungumza katika mkutano na vyombo vya habari.
Wizara ya mambo ya nje ya Tanzania imekiri kwamba Serikali ya Kenya ilimwita balozi wa Tanzania aliyeko Nairobi kutaka maelezo zaidi.
"Balozi wetu alisikiliza maelezo ya Serikali ya Kenya na akatumia fursa hiyo kuelezea masuala haya kwa Serikali ya Kenya. Vile vile Serikali imepokea barua kutoka Serikali ya Kenya kuhusu masuala haya, na Serikali itaijibu barua hiyo kutoa ufafanuzi," taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imesema.
"Serikali inapenda kuufahamisha umma kwa ujumla kuwa uingizwaji wa mifugo na bidhaa zake nchini Tanzania huongozwa na sheria za nchi, makubaliano ya kikanda na kimataifa."
Tanzania imesema kuwa ilipobainika kwamba kulikuwa na idadi kubwa ya mifugo kutoka nchi za jirani wameingizwa nchini humo pasipo kufuata sheria na taratibu zilizopo, serikali iliagiza mifugo hiyo irudishwe kwenye nchi kusika.
"Serikali ilitoa muda wa kutosha kwa wamiliki wa mifugo hiyo kuiondoa nchini. Tahadhari ilitolewa kwamba muda uliotengwa ukifikia ukomo, mifugo hiyo itakamatwa na kushugulikiwa kwa mujibu wa sheria za nchi," taarifa hiyo imesema.
Aidha, wizara hiyo imesema Waraka wa Kidiplomasia ulitumwa kwa kwa Serikali za Burundi, Kenya, Rwanda na Uganda, ikizihimiza kuwataka raia wao walioingiza mifugo nchini isivyo halali waiondoe.
"Wamiliki wengi walitii agizo hilo la Serikali ya Tanzania na kuondoa mifugo yao nchini.
"Hata hivyo, wapo wamiliki wachache kutoka nchi za jirani waliokaidi agizo hilo na hivyo ng'ombe wapatao 1113 walikamatwa katika Wilaya ya Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro na kupigwa mnada baada ya wamiliki wake kushindwa kujitokeza."
Tanzania imesema Kilimanjaro wapo ng'ombe 74 ambao wamiliki wake walijitokeza, wakalipa faini kwa amri ya mahakama na kuondoka na ng'ombe wao.
Katika Mkoa wa Kigoma ng'ombe 324 ambao wamiliki wake hawajajitokeza wamekamatwa na hatua stahiki zinachukuliwa.
Aidha, katika mkoa huo wa Kigoma ng'ombe 728 walikamatwa na wamiliki wao walijitokeza na kulipa faini kutokana na maamuzi ya Mahakama.
Katika mkoa wa Kagera jumla ng'ombe 1,536 ambao wamiliki wake bado hawajulikani wanashikiliwa na vyombo vya ulinzi na usalama na sheria itachukua mkondo wake.
"Kwa takwimu hizi ni wazi kwamba zoezi hili halijalenga nchi yeyote, kwa sababu sio nchi moja tu imeathirika," wizara hiyo ya mambo ya nje imesema.
"Hili suala halipaswi kusababisha mgogoro wa kidiplomasia na nchi yeyote, labda tu mtu aamue kwa makusudi yasiyo mema kupotosha na kuchochea mgogoro."
Tanzania imesema vifaranga vya kuku wa mayai 6,400 waliokamatwa Arusha kwa kuingizwa nchini bila kufuata sheria na kanuni waliteketezwa kutokana na msafirishaji wa vifaranga hivi kutokuwa na kibali cha aina yoyote kutoka mamlaka husika ya udhibiti wa magonjwa ya mifugo hapa nchini humo.
Wizara hiyo imesema Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo Tanzania alimpigia simu Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo wa Kenya kutaka kujua kama Mamlaka za Kenya zina habari kuhusu vifaranga waliokamatwa na kama Kenya ingekubali kuruhusu vifaranga hao warudishwe Kenya.
"Mkurugenzi huyu wa Kenya alisema hana taarifa kuhusu vifaranga hivyo na kwamba Kenya haiko tayari kuruhusu vifaranga hivyo kurudishwa nchini mwao kwa sababu havina nyaraka kulingana na miongozo ya kimataifa," taarifa hiyo imesema
Maoni