Iran imeonya iko tayari kurejesha mpango wake wa kutengeza silaha za kinyuklia kwa kile ilichokitaja kasi kubwa zaidi iwapo Marekani itajiondoa kutoka makubaliano yaliyofikiwa mwaka 2015 kuhusu mpango huo wa kinyuklia.
Waziri wa mambo ya nje wa Iran Javad Zarif ameonya kuwa iwapo Marekani itajiondoa kutoka makubaliano hayo yajulikanayo JCPOA, basi nchi yake haitakuwa na budi bali kuongeza kasi shughuli zao za kinyuklia.
Mapema mwezi huu, Rais wa Iran Hassan Rouhani alionya kuwa Marekani itajuta iwapo itajiondoa kutoka kwa makubaliano hayo yaliyofikiwa kati ya nchi sita zenye nguvu zaidi duniani na Iran yanayolenga kudhibiti mpango wa kinyuklia wa Iran na badala yake nchi hiyo ilegezewe vikwazo vya kiuchumi.
Je, Marekani itajiondoa kutoka JCPOA?
Rais wa Marekani Donald Trump amezitaka nchi za Ulaya kufanyia marekebisho makubaliano hayo ifikapo tarehe 12 mwezi Mei kwa kuiwekea Iran mbinyo zaidi la sivyo Marekani itajiondoa kutoka kwa makubaliano hayo yaliyofikiwa wakati wa utawala wa Barack Obama.
Waziri wa mambo ya nje wa Iran Javad Zarif
Suala hilo kuhusu hatma ya makubaliano hayo ya JCPOA ya mwaka 2015, litakuwa mojawapo ya ajenda kuu wakati wa ziara ya Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron mjini Washington inayoanza Jumatatu na pia Kansela wa Ujerumani Angela Merkel mbaye pia ataizuru Marekani Ijumaa wiki ijayo kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais Donald Trump.
Zarif amesema viongozi wa nchi za Ulaya wanapaswa kumshinikiza Trump kuheshimu makubaliano hayo iwapo Marekani inataraka kudumisha hadhi yake ya kuaminiwa katika jamii ya kimataifa.
Viongozi wa Ulaya wanatumai kumshawishi Trump kuyaokoa makubaliano hayo kuhusu Iran yaliyoko mashakani na kwa upande wao wataishinikiza Iran kufikia makubaliano kuhusu kusitisha majaribio ya makambora na kupunguza ushawishi wao katika nchi za kanda ya Mashariki ya Kati zinazokumbwa na mizozo- Yemen, Syria na Lebanon.
Iwapo Marekani itajiondoa katika makubaliano hayo kuhusu mpango wa kinyuklia wa Iran, inahofiwa kuwa Iran huenda isiyaheshimu makubaliano hayo yaliyofikiwa pia na Uingereza, China, Ufaransa, Ujerumani na Urusi.
Iran yatoa vitisho
Akizungumza na wanahabari mjini New York, Marekani anakohuduria mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu amani, waziri wa mambo ya nje wa Iran Javad Zarif amesema ni bayana kuwa ulimwengu hauwezi kuitarajia nchi yake kutekeleza na kuyaheshimu makubaliano hayo wakati upande mwingine umeyavunja.
Kiwanda cha kinyuklia cha Arak nchini Iran
Zarif ameongeza kuwa Iran haina nia ya kutengeza bomu la kinyuklia lakini nchi hiyo itajibu kujiondoa kwa Marekani katika makubaliano hayo ya kihistoria kwa kuanza tena kutengeza uranium, kiuongo muhimu katika utengezaji wa mabomu ya kinyuklia.
Iran imesema kuwa hatua ya Marekani kutaka kufanyia mageuzi vipengele vya makubaliano hayo unatuma ujumbe hatari sana kwa Wairan na ulimwengu kwa jumla kuwa nchi hazipaswi kufikia makubaliano na Marekani na pia kuwaonya Merkel na Macron kuwa kujaribu kumfurahisha Trump kuhusiana na suala hilo itakuwa na jaribio litakalofeli.
Trump anaamini kuwa makubaliano hayo ya JCPOA yana mapungufu makubwa ambayo yanahitaji kushughulikiwa ili kuizuia Iran kuwa na mwanya wa kuendeleza mpango wake wa kinyuklia
Maoni