Korea Kusini imesitisha matangazo ya propaganda kwenye eneo la mpaka na Korea Kaskazini, kabla ya viongozi wa nchi hizo mbili kukutana kwa mazungumzo yanayotarajiwa kujikita juu ya mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini.
Licha ya kuwepo matumaini ya Korea Kaskazini kusitisha mpango wake wa kinyuklia, Rais wa Marekani Donald Trump ameonya kuwa bado kuna njia ndefu ya kufikia suluhisho la mzozo wa Korea kaskazini huku kiongozi huyo wa Marekani akijitayarisha kwa mkutano wa kihisitoria na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un.
Korea zachukua hatua za maridhiano
Kama sehemu ya ishara ya kujitayarisha kwa mazungumzo ya maridhiano kati ya Korea Kusini na Korea Kaskazini ambayo ni ya tatu ya aina hiyo tangu kukamalizika vita vya Korea vilivyodumu kati ya mwaka 1950 hadi 1953, Korea Kusini imezima matangazo ya propaganda yanayotangazwa kupitia vipaza sauti katika eneo la mpakani.
Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un
Korea Kusini ilikuwa ikitangaza habari, ujumbe wa kuikashifu Korea Kaskazini na kupiga nyimbo kupitia vipaza sauti lakini taarifa ya Wizara ya ulinzi ya Korea Kusini imesema imesitisha matangazo hayo, kujaribu kupunguza mvutano wa kijeshi na kuweka mazingira bora kwa mazungumzo ya amani. Haijulikani kama baada ya mkutano huo wa Ijumaa, vipaza sauti vitawashwa tena.
Korea Kaskazini pia hutangaza taarifa na nyimbo mipakani lakini haijabainika iwapo nayo imezima vipaza sauti vyake.
Wachambuzi wanafuatilia umuhimu wa hatua kadha wa kadha zilizochukuliwa na Korea Kaskazini tangu mwaka huu uanze ikiwemo kutangaza kuwa tayari kufanya mazungumzo na Marekani na mahasimu wao Korea Kusini pamoja na mwishoni mwa juma lililopita kutangaza kuwa itasitisha mpango wake wa kinyuklia, baada ya kuwekewa vikwazo chungu nzima na jumuiya ya kimataifa na kusababisha hali ya taharuki katika rasi ya Korea.
Je, Korea Kaskazini itaachana kabisa na silaha za nyuklia?
Rais wa Korea Kusini Moon Jae-in leo ameipongeza hatua ya Korea Kaskazini kuahidi kusitisha majaribio ya silaha za kinyuklia na kuitaja hatua hiyo kuwa uamuzi muhimu utakaopelekea rasi ya Korea kuwa huru dhidi ya kitisho cha silaha za nyuklia.
Rais wa Marekani Donald Trump na wa Korea Kusini Moon Jae In
Moon anatarajiwa kukutana na Kim Ijumaa hii katika kijiji cha Panmunjom, eneo la mpakani kati ya nchi hizo na ambalo lina usalama mkali.
Itakuwa mara ya kwanza kwa Kim kukanyaga ardhi ya Korea Kusini tangu kuwa kiongozi wa Korea Kaskzini. Mikutano iliyopita kati ya Korea hizo mbili ilifanyika Pyongyang mwaka 2000 na 2007.
Mahusiano kati ya nchi hizo mbili yameimarika katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni kuanzia wakati Korea Kaskazini iliposhiriki mashindano ya Olimpiki ya majira ya baridi Korea Kusini mwezi Februari mwaka huu.
Lakini kinachosalia kushuhudiwa ni iwapo Kim kweli ataachana kabisa na mpango wa kutengeza silaha za kinyuklia na kurusha makombora ya masafa marefu yenye uwezo wa kufika Marekani na badala yake kuzingatia zaidi katika kuimarisha uchumi wa taifa lake na kupatikana amani.
Maoni