Jambazi sugu ametoroka jela kwa kutumia ndege aina ya helikopta katika jela moja mjini Paris , mamlaka ya Paris imesema.
Redoine Faid alisaidiwa na watu kadhaa waliojihami ambao walitengeneza mwanya katika lango la jela hiyo huku helikopta hiyo ikitua katika uwanja karibu na jela hiyo.
Ndege hiyo ilipaa hadi eneo la Gonessa lililopo karibu na jela hiyo ambapo ilipatikana na maafisa wa polisi.
Faid 46, amekuwa akihudumia kifungo cha miaka 25 kwa jaribio la wizi wa mabavu lililotibuka ambapo afisa mmoja wa polisi aliuawa.
Hii ni mara yake ya pili kutoroka jela: Mwaka 2013 alitoroka jela baada ya kuwatumia walinzi wanne kama ngao huku akilipua milango kadhaa kwa kutumia kilipuzi.
Alifanikiwa kutoroka chini ya nusu saa baada ya kuwasili katika jela hiyo iliopo kaskazini mwa Ufaransa.
Mwaka 2009 Faid aliandika kitabu kuhusu uzoefu wake katika mitaa ya Paris iliojaa uhalifu na kuwa mtu aliyekukuwa akivunja sheria mara kwa mara.
Alidai kuwacha uhalifu lakini mwaka mmoja baadaye alihusika katika jaribio la wizi lililotibuka ambapo alipelekwa jela ya Réau katika jimbo la Seine-et-Marne.
Faid na washirika wake walitorokea katika uwanja huo wa jela ambao haukuwa na ulinzi mkali, bila ya kumjeruhi yeyote kulingana na chombo cha habari cha Ufaransa Europe1.
Watu waliokuwa wamejihami kwa risasi walimchukua mfungwa huyo katika chumba cha kuwatembelea wageni kabla ya kumpeleka katika helikopta hiyo na kutoroka naye kulingana na duru za usalama zilizonukuliwa na chombo cha habari cha reuters.
Ripoti zinadai kwamba rubani wa helikopta huenda alikuwa ametekwa nyara. Usakaji wa maafisa wa polisi unaendelea katike eneo lote la Paris.
Hatua zote zinafanywa kumtafuta mtoro huyo , kulingana waziri wa maswala ya ndani.
Akiwa amezaliwa 1972, Faid alilelewa katika maeneo ya uhalifu mwingi ya mitaa ya Paris kabla ya kuanza maisha ya uhalifu
Miaka ya tisini , alikuwa akisimamia genge lililohusika na uhalifu wa kujihami na ulafi ktika mji mkuu wa Paris. Alikuwa akisema kwamba maisha yake yalipata msukumo wa filamu za uhalifu za Hollywood, ikiwemo Al Pacino na Scarface.
Mwaka 2001 alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa uhalifu
Maafisa wa polisi wa Ufaransa wanaamini kwamba Faid aliongoza uhalifu ambapo afisa wa polisi aliuawa, lakini akahukumiwa kwa uhalifu aliotekeleza mnamo Aprili.
Alikuwa amerudishwa jela 2011 kwa kukiuka masharti ya msamaha yanayohusiana na makosa ya awali.
Mwaka 2013, alitoroka katika jela ya kaskazini mwa Ufaransa ya Sequedin nje ya Lille, kwa kuwateka nyara walinzi wawili, lakini akakamatwa tena wiki sita baadaye
Mwaka uliopita, alihukumiwa kifungo cha miaka 10 jela kwa kutoroka jela 2013
Maoni