Viongozi wa Afrika wanakutana Mauritania Jumapili(01.07.2018)katika mkutano wa siku mbili utakaolenga biashara huria, upatikanaji wa fedha, mapambano dhidi ya rushwa pamoja na mizozo mingi ya kiusalama barani humo.
Zaidi ya viongozi wa serikali na taifa 40 wanatarajiwa kuwasili katika mji mkuu wa Mauritania , Nouakchott, wakiungana siku ya Jumatatu na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron , ambaye anatarajiwa kusukuma juhudi za kiusalama katika eneo la Afrika kaskazini.
Kiongozi wa Rwanda Paul Kagame, ambaye anashikilia urais wa kupokezana wa Umoja wa Afrika ( AU )wenye wanachama 55, atatoa rai kuhimiza biashara huru.
Paul Kagame (kulia) akisalimiana na rais Emmanuel Macron wa Ufaransa(kushoto)
Kwa hivi sasa, mataifa ya Afrika yanafanya baina yao biashara ya kiasi cha asilimia 16 tu , kiasi kidogo cha biashaa ya kimkoa ikilinganishwa na mataifa ya America kusini, Asia, Amerika kaskazini na Ulaya.
Lakini mabadiliko yako karibu.
Mwezi Machi , mataifa 44 yalitia saini mkataba kuunda eneo la biashara huru la bara la Afrika , African Continental Free Trade Area, (CFTA), unaoonekana kuwa ni eneo kubwa kabisa la kibiashara duniani kwa mujibu wa nchi zinazoshiriki.
Matunda ya majadiliano ya miaka miwili, CFTA ni mradi muhimu wa AU kwa ajili ya ujumuisho mkubwa zaidi wa bara la Afrika.
Iwapo mataifa yote 55 wanachama hatimaye yatatia saini, itaunda kundi ambalo linajumla ya pato jumla la taifa GDP linalofikia dola trilioni 2.5, na kukusanya soko lenye jumla ya watu bilioni 1.2.
Viongozi wa mataifa yaliyotia saini mkataba wa ACFTA
Mapambano dhidi ya rushwa
Lakini mataifa mawili yenye uchumi mkubwa katika bara hilo, Afrika kusini na Nigeria, ambayo rais wake, Muhammadu Buhari , anatarajiwa kufika katika mkutano huo, ni mataifa ambayo hayamo katika mkataba wa CFTA.
Kagame pia atasukuma mbele pendekezo la miaka miwili sasa lenye lengo la kuimarisha mfuko wa fedha na kupunguza Umoja wa Afrika kutegemea wafadhili wa nje, suala ambalo mara nyingi huzushwa na wakosoaji ambao wanauona umoja huo kuwa mkubwa kwa maneno lakini hakuna vitendo.
Wazo hilo ni kuhusu kodi ya asilimia 0.2 katika baadhi ya bidhaa zinazoingizwa katika bara la Afrika ili kuimarisha "Mfuko wa Amani" kwa ajili ya kugharamia ujumbe wa amani na usalama.
Katibu msaidizi wa Umoja wa Mataifa Vera Songwe akihutubia mkutano wa FTCA
Katika bajeti ya AU ya dola milioni 769, dola milioni 451 zinatoka kwa wafadhili wa kigeni, ambao huchangia pia asilimia 97 ya mipango yake.
Kupambana dhidi ya rushwa ni lengo kuu la mkutano huo, wanaopambana na rushwa wataangalia kwa kina kile ambacho Afrika inalenga kufanya katika kupunguza sifa yake kuwa ni eneo lililochafuka zaidi katika kufanya biashara duniani.
Shirika la Transparent International , katika kielelezo chake cha hivi karibuni katika rushwa kilichochapishwa mwezi Februari , imesema rushwa imejikita nchini Sudan Kusini na Somalia, miongoni mwa mataifa mengine. Lakini pia imesema picha ya jumla ya bara la Afrika imechanganyika, na kundi la uongozi linajitokeza katika kupambnana na rushwa
Maoni