MPANGO WA KUIMARISHA UBORA WA AFYA NA USTAWI WA WATOTO NI NYENZO MUHIMU- DKT. SHEKALAGHE



Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe amesema Mpango wa Kuimarisha Ubora wa Afya na Ustawi wa Watoto ni nyenzo muhimu katika kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa watoto na vijana nchini.

Dkt. Shekalaghe amesema hayo leo Julai 23, 2025 mkoani Arusha wakati wa kongamano la Pili la Kitaifa la Afya na Ustawi wa Watoto baada ya kuzindua rasmi mpango huo wenye lengo la kushughulikia changamoto zinazowakabili watoto na vijana ikiwemo matatizo ya lishe, mimba za utotoni na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU).

Mpango huo umeandaliwa na Chama cha Madaktari Bingwa wa Watoto Tanzania (Pediatric Association of Tanzania – PAT) kwa kipindi cha miaka Mitano (5) kuanzia mwaka 2025 hadi 2030 ambao umejikita katika kushughulikia vikwazo vinavyokwamisha maendeleo ya kiafya kwa watoto na vijana, hasa wenye umri wa miaka 15-19.

Vipaumbele vya mpango huo ni pamoja na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa Wizara ya Afya na wadau wa sekta ya afya, kushawishi na kuandaa sera zitakazosaidia kuimarisha afya na ustawi wa watoto,kuwekeza katika tafiti na ubunifu wa kitabibu ili kuboresha huduma,kutoa mafunzo endelevu kwa madaktari bingwa na watumishi wengine wa afya


Pia mpango huo unalenga kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, Sekta Binafsi pamoja na mashirika ya kimataifa katika kukuza na kuimarisha rasilimali zitakazowezesha utekelezaji wa huduma bora kwa watoto na vijana.

Awali, akizungumza katika uzinduzi huo, Rais Mteule wa Chama cha Madaktari Bingwa wa Watoto Tanzania Dkt. Alex Mphuru, ameiomba Serikali pamoja na wadau wa maendeleo kushirikiana katika utekelezaji wa mpango huo ambao unakadiriwa kugharimu jumla ya Shilingi Bilioni 2,241,810,000.

"Kwa ujumla mpango huu ni hatua muhimu katika kuelekea kujenga kizazi chenye afya njema, lishe bora, na ustawi wa kudumu kwa watoto na vijana nchini Tanzania," amesema Dkt. Mphuru.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

ZIJUWE SHERIA 17 ZA SOKA

MAPENZI: Kuna faida na ni muhimu Mpenzi wako kuwa rafiki yako pia

KUMTUMAINIA MUNGU