WAZIRI WA CANADA AFANYA ZIARA YA SIKU TATU TZ
Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Canada, Randeep Sarai, amewasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku tatu.
Akiwa nchini, Sarai anatarajiwa kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo inayofadhiliwa na Serikali ya Canada katika miji ya Dar es Salaam, Dodoma, na Zanzibar.
Miradi itakayotembelewa ni pamoja na Kituo cha Afya cha Makuburi na Kampuni ya Nishati Mbadala ya JAZA mkoani Dar es Salaam, Mradi wa Kurina Asali wa Central Park Bees na Kiwanda cha kuzalisha na kusambaza unga wa Sembe - Chamwino mkoani Dodoma pamoja na Kituo cha Afya cha Makole mkoani humo.
Akizungumza baada ya mapokezi ya Waziri huyo wa Canada, Waziri wa Afya, Jenista Mhagama ameishukuru Serikali ya nchi hiyo kwa mchango wake wa zaidi ya shilingi bilioni 120 katika kuboresha sekta ya afya nchini Tanzania kupitia miradi mbalimbali.
Naye waziri huyo wa Maendeleo ya Kimataifa wa Canada, Randeep Sarai, amesisitiza dhamira ya Canada kuendelea kushirikiana na Tanzania ili kuleta mabadiliko chanya na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili.
Maoni