Doria ya pamoja ya Urusi - China yazua tumbo joto Japan na Korea Kusini
Korea Kusini ilisema kuwa ndege ya kijeshi ya Urusi aina ya A-50 ilikiuka anga yake mara mbili
Urusi inasema kuwa imetekeleza doria yake ya kwanza ya pamoja na China , hatua iliyozifanya Korea Kusini na Japan kutuma ndege za kivita angani.
Waziri wa ulinzi nchini Urusi amesema kuwa ndege nne aina ya bombers zikisaidiana na zile za kivita zilipiga doria katika njia ambayo hazikupangiwa kupitia katika maji ya Japan na bahari iliopo mashariki mwa China.
Korea Kusini inasema kuwa ndege zake zilirusha makombora ya kutoa onyo wakati ndege za kijeshi za Urusi zilipoingia katika anga yake. Japan imelalamika kwa Urusi na Korea Kusini kwa tukio hilo.
Kisa hicho kilitokea juu ya visiwa vinavyozozaniwa vya Dokdo/Takeshima ambavyo vinamilikiwa na Korea Kusini lakini Japan pia inadai kuwa vyake.
Korea Kusini inasema kuwa ndege za kijeshi za Urusi na China ziliingia katika anga yake ilio na ulinzi mkali ya KADIZ siku ya Jumanne alfajiri na kwamba ndege moja ya kijeshi ya Urusi aina ya A-50 ilikiuka sheria za kimataifa na kuingia katika anga yake mara mbili karibu na visiwa hivyo. Urusi imekana madai hayo.
Ndege za kijeshi za Urusi na China aina ya Bombers mara kwa mara zimekuwa zikipitia eneo hilo katika miaka ya hivi karibuni lakini hicho ndio kisa cha kwanza kutokea kati ya Urusi na Korea Kusini.
Je Moscow inasemaje?
Wizara ya ulinzi inasema kuwa ndege zake mbili za kijeshi aina ya Tu-95MS zinazobeba makombora zilishirikiana na ndege nyengine mbili za China aina ya Hong-6k katika doria ambayo ilipitia katika njia ambayo hazikupangiwa juu ya anga ya maji yasiomilikiwa na taifa lolote.
Ndege hizo zilisaidiwa na ndege za kijeshi aina ya A-50 pamoja na Kongjing-2000 zinazotumika kutoa onyo .
Luteni jenerali Sergei Kobylash alisema kwamba wakati wa doria hiyo walifukuzwa mara 11 na ndege za kigeni.
Aliwashutumu manohodha wa ndege za Korea kusini kwa kufanya 'hatari' na kundi hilo la angani pamoja na hatari ya usalama wa ndege hizo.
Anasema kwamba ndege hizo za Korea Kusini zilirusha alama za moshi kutoa onyo.
Doria hiyo alisema ilifanyika zaidi ya kilomita 25 mbali na visiwa vya Doldo/Takeshima , na akawashutumu manahodha wa Korea kwa kufanya uhalifu angani.
Alisema kwamba Urusi ililalamika kwa Korea Kusini kuhusu vitendo vya hatari vya manahodha wake.
Muungano utakaoipatia Marekani tumbo Joto
Kulingana na mchanganuzi wa BBC wa maswala ya Ulinzi Johnathan Marcus , doria ya kwanza ya pamoja angani ilioshirikisha Urusi na China katika eneo la pacific Asia , inatuma ishara kuhusu hatua zilizopigwa na Mscow na Beijing.
Ijapokuwa nchi hizo mbili hazijaanzisha muungano rasmi wa pamoja zoezi hilo la pamoja ni kubwa na la kisasa.
Hatua hii ni ishara ya wazi ya uhusiano mzuri wa kiuchumi na kidiplomasia kati ya mataifa mawili ambayo licha ya kwamba bado yana wasiwasi yanaendelea kuleta uhusiano wa pamoja,
Yote mawili yana maono yanayofanana kuhusu ulimwengu wa sasa yakiwa maadui ya demokrasia iliopo magharibi,
Yakiwa tayari kukuza mbadala wa kutetea uhuru wao mbali na kuwa tayari kuonyesha uwezo wao dhidi ya mataifa mengine.
Swala hili linatoa changamoto kubwa kwa mkakati wa Marekani.
Ndoto ya Washington ni kuimarisha uhusiano wake na Urusi inayodorora na China inayoendelea kuimarika na tayari kuipiku Marekani kama taifa lenye uwezo mkubwa kiteknolojia na kiuchumi katika kipindi cha miaka kadhaa ijayo.
Je Korea Kusini inasemaje?
Jeshi la Korea Kusini linasema kuwa ndege hiyo ilikuwa mojawapo ya ndege tatu za Urusi na mbili za jeshi la China ambazo ziliingia katika anga ya KADIZ , ambapo ndege za mataifa mengine ni sharti zijitambulishe.
Ndege za kijeshi za Urusi na China zimekuwa zikiingia katika eneo hilo katika miaka ya hivi karibuni.
Hatahivyo Korea Kusini inasema kuwa moja ya ndege hizo ilipaa zaidi na kuingia katika anga ya nchi hiyo mwendo wa saa tatu alfajiri saa ya Korea.
Ndege za Kijeshi za Korea Kusini F-15k na F-16k zilitumwa kwenda kuizuia.
Mkuu wa kitengo cha usalama nchini Korea Kusini Chung Eui-yong amewasilisha malalamishi kwa baraza la usalama la Urusi na kulitaka kuchukua hatua kali.
''Tunakichukulia kitendo hiki kama kisichokuwa cha kawaida , na iwapo kitarejelewa tutachukua hatua kali, afisi ya rais wa taifa hilo ilimnukuu bwana Chung akisema. Hakujakuwa na tamko lolote kutoka China
Ndege ya kijeshi ya Korea Kusini aina ya F-15 ilitumwa kuizuia ndege hiyo ya Urusi
Na Japan Je?
Serikali ya Tokyo imewasilisha malalamishi dhidi ya Urusi na Korea Kusini.
Kwa kuwa inadaia umiliki wa visiwa hivyo, serikali ya Japan inasema kuwa Urusi ilikiuka anga yake.
Pia inasema kwamba jibu la Korea Kusini lilikuwa la kujutia.
Mkuu wa baraza la mawaziri nchini Japan Yoshihide Suga: Msimamo wa Japan kuhusu uumiliki wake wa Takeshima , hatua ya ndege za kijeshi za Korea Kusini kurusha moshi wa kutoa onyo ni swala ambalo haliwezi kukubalika na la kujutia.
Maoni