Ruka hadi kwenye maudhui makuu

RIWAYA: JERAHA LA HISIA SEHEMU YA SITA

MTEULE THE BEST



RIWAYA: JERAHA LA HISIA
MTUNZI: George Iron Mosenya
Mawasiliano: 0655 727325

SEHEMU YA SITA

KIMBOKA, ni moja ya baa maarufu sana jijini Dar es salaam. Umaarufu wake si kwa sababu ya huduma bora wanazotoa ama mandhari nzuri ya kuvutia katika baa hiyo.
Umaarufu wake ulisambaa sana kutokana na huduma ya bei rahisi pengine kuliko sehemu yoyote katika jiji hilo. Huduma ambayo inawasaidia makapela azidi kusahau kuhusu ndoa mathalani kuishi na mwanamke ndani.
Biashara ya uuzaji miili kwa bei nyepesi sana.
Baa hii ilikuwa makazi ya mwanadada Naomi kwa kipindi tangu akimbie shutuma za kuhusika katika kifo cha Maureen.
Naomi alikimbilia huku si kwa kuwa naye alikuwa wa bei rahisi sana kwa wakati huo la. Alihofia usalama wake na kubwa zaidi alikuwa amechanganyikiwa.
Dawa ya kutuliza mawazo aliamini kuwa ni kunywa pombe, basi kama kweli ni pombe Kimboka zinapatikana kwa bei ya kawaida bila nyongeza yoyote.
Naomi akawa Naomi wa Kimboka.
Dada yake naye alikuwa kitu kingine ambacho kilizidi kumchanganya akili. Tayari walishasahau kuwa walimzika mama yao miaka kadhaa nyuma, leo yule dada aliyemzika mama haishi kuhudhuria hospitali, leo Amana kesho Temeke, Mwananyamala na wakati mwingine Muhimbili.
Afya ilikuwa imezorota na alikuwa amekata tamaa ya kuendelea kuishi.
Haikuhitaji elimu kubwa sana kutambua kuwa mwanadada alikuwa katika siku za mwisho za uhai wake.
UKIMWI ulikuwa unamtafuna kwa kasi.
Changudoa wa zamani alikuwa ameukwaa.
Huenda yalikuwa malipo sahihi kwake.
Naomi akabaki kuishi katika mashaka, akahisi hata yeye alikuwa ameukwaa, kuna baadhi ya wanaume ambao walipita katika mwili wa dada yake na yeye akawapokea vivyo hivyo bila kutumia kinga akawapatia huduma stahiki, wakampa malipo.
Kama walivyomlipa dada yake na kisha kumwachia dubwana lile ambalo linamlaza kitandani, linakula ngozi yake kwa namna ya mkanda wa jeshi, linamfanya akohoe kwa maumivu makali na safari za chooni zikiwa hazina muda maalum.
Lazima naye awe na mashaka, tena mashaka makubwa.
Kwa kuwa wamemuambukiza dada yangu, ngoja nami niwaambukize.
Alijiapiza Naomi, n’do lengo haswaa la kujiweka katika soko jepesi la walalahoi. Buguruni katika baa ya Kimboka.

Katika ukumbi huu wa baa,Naomi licha ya kujiuza kwa kuvaa hovyo hovyo alikuwa na njia nyingine za kuutangaza mwili wake na pia kujiongezea kipato cha kumnunulia dada yake dawa na mahitaji mengine kwa mgonjwa.
Naomi akaamua kutumia kipaji chake ambacho amekuwa nacho tangu utotoni, kipaji cha kucheza muziki. Kila bendi ya muziki ilivyokuwa ikiwaburudisha walevi usiku kucha, Naomi alikuwa akicheza kwa umahiri mkubwa sana na mwishowe anatunzwa shilingi mbili tatu.
Bendi zikamtambua, hatimaye kikawa kibarua chake, kuwaburudisha walevi pindi wanausaka ulevi wao na mwishowe kuwaburudisha kitandani wakiwa tayari wamelewa.
Hawa waliolewa, Naomi alifanya kuwaibia wakizubaa.
Haya yakawa maisha rasmi ya Naomi hadi lilipotoka tangazo la mashindano ya kucheza kwa ajili ya tamasha kubwa la muziki.
Naomi akahudhuria kwa kujaribu.
Matokeo yake akashinda na hatimaye akaingia katika jukwaa kubwa la ukumbi wa Diamond Jubilee.
Ni huku ambapo jicho la Walter lilimuona bila yeye kujua.

Baada ya tamasha Naomi kama kawaida alikuwa ameopolewa na kibopa mwingine, alionekana ni mtu mwenye pesa zake. Naomi akatambua kuwa amepona kwa siku hiyo.
Akiwa na yule kibopa anasikia sauti inamuita kwa mbali, ilikuwa sauti ya kiume.
Sauti ilizidi kuita.
Naomi akatambua kuwa hao walikuwa wateja wake wa zamani na sasa walikuwa wanakaribia kumharibia.
Naomi akacheza karata sahihi. Akamkokota yule mwanaume wakaingia katika gari.
Milango ikafungwa.
“Sihitaji kuonana na mtu tafadhali, yaani mtu ukishakuwa ‘Superstar’ basi kero aziishi.” Naomi alijisemesha, huku kichwani akijishangaa ameitoa wapi hiyo kauli.
“Poleni sana mpenzi mnahangaika kweli. Kwa hiyo huyo anaweza kuwa nani?”
“Sio huyo ni hao wapo wengi, watakuwa waandishi wa habari hao, nishawaambia sipendi mambo yao, bado wananifatilia.”
Alipomalizia ile kauli, yule aliyekuwa anamuita akalifikia gari. Akaanza kugonga kioo.
Kibopa keshajazwa ujinga, akashusha kioo kidogo, akaanza kutukana kana kwamba amefungiwa kifaa kilichorekodiwa maneno yale.
Baada ya matusi gari ikaondolewa, huku Kibopa akiwa ametaharuki.
Aliamini kuwa yupo na mtu wa kuheshimiwa sana katika jamii.
Laiti kama angejua ni wapi ameshikilia, angeachia upesi mahali hapo.

****

UZURI wa jiji la Dar es salaam, kuna usafiri wa aina mbali mbali, ni wewe tu kuamua unataka kusafiri kwa starehe ili uchelewe ama kwa karaha ili uwahi.
Hata usiku ambao Walter alimaliza kushughulika jukwaani, alijikuta katika maamuzi hayo pia.
Bodaboda. Lilikuwa jibu sahihi kwake.
Hakuhitaji kumpoteza Naomi kabisa.
Aliamini kumpoteza kwa siku hiyo basi ungekuwa mtihani mwingine mgumu.
Walter akaamua kuchukua ‘bodaboda’ na kuanza kulifuatilia lile gari lililombeba Naomi.
Mwisho wa safari yao ukawa katika nyumba nzuri nyeupe ya kulala wageni.
Walter akakaza jicho, hakika aliyemuoana alikuwa ni Naomi wake ambaye bibi yake alimuita ‘mkamwana’ .
Kidogo Walter amvamie, lakini akkumbuka kuwa Naomi alikuwa mpenzi wake wa utoto tu si zaidi ya hapo. Na ni miaka zaidi ya kumi ilikuwa imekatika tangu waonane.
Walter akapiga moyo konde.
“Kaka ulikuwa unamfuatilia huyu demu?.” Dereva wa ile pikipiki akmuuliza Walter aliyekuwa anashangaa bado.
“Ndio kaka, lakini sijui kama nimemfananisha ama vipi.”
“Sio Naomi wa Kimboka yule.”
Walter akageuka na kumtazama yule dereva, akawa anamsikiliza anavyomuelezea Naomi.
“Nipe namba zako, kesho nakuchukua mida ya usiku nakupeleka Kimboka, hapo utaonana naye bila shaka, kama alikuibia simu sahau maana haogopi kupigwa huyo. Itakuwa imekula kwako.” Dereva akampatia namba Walter, naye akampatia za kwake.

Usiku huu ukapita katika hali ya kutia simanzi. Walter akiwa na maswali lukuki.
“Kivipi Naomi ajulikane kiasi hicho, na hapo Kimboka n’do kazini kwake nini?” alijiuliza Walter kabla ya kupitiwa na usingizi. Kisha ukauta usiku mwingine ambao kamwe hatausahau maishani mwake.
Usiku wa kukutana na Naomi wake. Msichana ambaye alikuwa amesalia kama faraja pekee ya nchini Tanzania.
Walter alionana na Naomi majira ya saa nane usiku, alikuwa amechoka sana na macho yake yalikuwa yamelegea, mavazi yalikuwa machafu upande wa mgongoni na hata kisogoni alikuwa na uchafu.
Walter akakumbwa na sintofahamu, amkabili ama aendelee kungoja.
Machangudoa nao kwa fujo walikuwa wakimsumbua Walter, mara wamfunulie mapaja, mara wambusu, mara wamtekenye. Ilimradi tu kumtia vishawishi.
Walter hakushawishiwa, badala yake alimsogelea Naomi.
Akamgusa bega.
Akaporomoshewa tusi zito.
“Naomi.” Akaita.
“Naomi mama yako…..” Alijibu yule dada aliyetawaliwa na hasira.
“Naomi njoo basi …”
“Una shi’ng ngapi wewe bata.”
“Njoo tuongee.” Walter alisihi.
Hatimaye sauti ikapiga ngoma za sikio la Naomi, akaanza kuogopa, aliwahi kuisikia mahali, akageuka upesi. Akakutana na sura ikiwa katika majonzi.
Cha mtu chake tu. Naomi angeweza kusahau kila kitu lakini sio sura ya Walter.
Naomi akasimama ghafla. Akayatumbua macho yake kama ambaye amekamatwa na polisi bila kutegemea.
Ana kwa ana na Walter.
“Walter…” akajikuta anaita bila kutaraji.
“Naomi.” Walter akajibu kwa sauti ya chini. Kisha akamshika mkono Naomi, wakajiweka mbali na kelele za muziki na machangudoa waliolewa.
Naomi akaanza kulia, Walter hakuweza kumbembeleza akabaki kulia pamoja naye. Wakakumbatiana.
Naomi aliendelea kutokwa na machozi kwa fujo.
Ilikuwa lazima atokwe machozi, alikuwa amepitia mengi machafu ya kusikitisha na Walter aliyeonekana mbele yake alikuwa na kila dalili za kuwa na upendo wa zamani. Macho yake yaling’ara kwa huba ya ajabu, midomo yake haikuzungumza lakini alikuwa anatangaza mambo kadhaa katika uso wake.
Ni kama vile alikuwa anasema “nakupenda kupita wasichana wote duniani.”
Hakika alikuwa katika hisia motomoto.
Hisia za kukutana na Naomi.
Lile jeraha lake la hisia sasa lilikuwa limempata wa kulitibu vyema.
Hisia za miaka zaidi ya kumi zimepata pa kuzitua.
Hisia za marehemu bibi.

Naomi bado alikuwa katika mshangao. Mshangao mkuu.
Hakuamini kama aliyepo mbele yake ni Walter.
Walter akamchukua hadi katika gari aliyokuja nayo. Akamfungulia mlango kama malkia ama mtu wa kuheshimiwa sana, kisha naye akaingia, huku nyuma vikabaki vicheko tele kutoka kwa machangudoa na baadhi ya wateja ambao walikuwa wanamfahamu Naomi. Waliamini kijana yule alikuwa amepotea njia kumuopoa changudoa yule.

****

“Walter, sio kwamba sikupendi tena. Hapana mimi sio msafi, mimi sistahili kuwa mkeo wala hadhi ya uchumba sina. Walter wewe tafuta mwanamke mwingine oa. Sistahili hata kuwa nawe katika chumba hiki cha kifahari, nielewe Walter sina hadhi ya kuitwa mke. Mimi ni makapi na mfano mchafu kabisa usiofaa kuigwa na jamii.
Walter kwa pale uliponikuta unadhani nilikuwa nafanya nini? Dunia imenisaliti tangu nikiwa mdogo, nilizaliwa maskini na nisiyekuwa na akili na nitakufa hivihivi, na sina siku nyingi za kuishi mimi natakiwa kufa Walter. Duniani si mahali sahihi kwangu. Sina vigezo vya kuwa hapa, ninatakiwa kwenda katika ulimwengu mwingine tu.
Niwe mkeo? Walter hapana, sitaki kukuaibisha mpenzi, sitaki uaibike mtaani, kila mtu anajua mimi ni chawote walter, nakuwa muwazi kwako kwa sababu ulinipenda tangu utoto wako, najiweka uchi kwa kila kitu ili unifahamu mimi, maskini wa kutupa niliyeangukia katika domo la uchangudoa nalo limenimeza na halitaki kunitapika. Niache Walter, niache na umtafute wa hadhi yako.” Alishindwa kuendelea kuzungumza Naomi, kilio kikachukua nafasi. Baada ya muda mrefu wa kulia kwa kuigiza igiza mbele ya wateja wake sasa alikuwa analia kilio cha ukweli mbele ya Walter.
“Naomi, niliyeko mbele yako ni yuleyule Walter uliyemwongoza utotoni na kunifunza mengi, ni yuleyule Walter ambaye alikuita baada ya kushuhudia bibi yake akiwa sakafuni akivuja damu, na ni yuleyule Walter ambaye alitoweka bila kupenda akaenda mbali nawe. Nimekutana na wasichana tofauti wa hadhi tofauti lakini sifurahii kuwa nao, kuna sauti ya bibi inaniambia, ‘Naomi ndiye mkeo. Muoe.’ Siwezi kuipuuza sauti ya bibi yangu, bibi aliyetupenda mimi na wewe.
Bibi aliyekufa nikimwona. Naomi mimi ni Walter na nitabakia kuwa Walter, kama wewe kutembea na wanaume wengi wanakuita changudoa kwa sababu tu unalipwa, basi hata mimi nimetembea na wasichana wengi tu. Mimi ni Malaya zaidi yako…….sote sisi ni wachafu, usijihukumu kwa sababu tu akina fulani wanajua wewe ni changudoa. Kwa ngu mimi wewe ni Naomi. Nafunga mjadala huu kwa sauti kutoka ndani ya moyo wangu, moyo wenye majeraha kadha wa kadha. Nitakuoa Naomi na kamwe sitamsikiliza mwanadamu yeyote.” Alimaliza Walter kuzungumza maneno yale makali, Naomi akawa analia kwa sauti ya juu kila neno lilikuwa kama msumari kwake.
Aliusikia uchungu haswa.
Walter alikuwa ameibua mambo mengi kwake. Mambo yanayoumiza haswaa.

**WALTER anahitaji ndoa ya changudoa…hajali amefanya nini, amefanya na nani…WALTER anaisikiliza sauti ya ndani…sauti inamsihi amuoe CHANGUDOA…….itakuwaje?

***NAOMI amekataa kuolewa anajihisi hana hadhi ya kuitwa mke?...je nini kitajiri???
SHARE ZAIDI NA ZAIDI iwafikie wadau wa simulizi murua za Kiswahili

ITAENDEELA

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Urusi: Vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini havitafua dafu

MTEULE THE BEST Image caption Waziri wa maswala ya kigeni nchini Urusi Sergei Lavrov na mwenzeka wa Marekani Rex Tillerson Waziri wa maswala ya kigeni nchini Urusi Segei Lavrov amemwambia waziri wa ulinzi nchini Marekani Rex Tillerson kwamba kuiwekea vikwazo zaidi Korea Kaskazini hakutafua dafu. Taarifa iliochapishwa na wizara ya kigeni nchini Urusi inasema kuwa wawili hao walizungumza kwa njia ya simu na kushutumu majaribio ya makombora ya hivi karibuni yaliotekelezwa na Pyongyang . Lakini inasema kuwa bwana Lavrov alisisitiza kwamba diplomasia ndio njia ya pekee ya kumaliza wasiwasi katika rasi ya Korea, na kutaka hatua zozote dhidi ya taifa hilo kusitishwa akionya huenda zikasababisha madhara yasiojulikana. Waziri wa ulinzi nchini Marekani amesisitiza kuwa bado kuna fursa ya kidiplomasia katika kukabiliana na Korea Kaskazini. Mapema rais Trump alichapisha ujumbe katika akaunti yake ya Twitter akisema mazungumzo sio suluhisho.

*DKT. MAGUFULI, MNANGAGWA WAWEKA HISTORIA MPYA*

Rais wa Zimbabwe, Emerson Mnangagwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli Rais wa Zimbabwe, Emerson Mnangagwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli wameweka historia mpya kwa kukubaliana kushirikiana kwenye maeneo makuu matatu yenye tija pande zote. *Kwanza*, *Kuimarisha uchumi* wa nchi hizi mbili kwa kukuza uwekezaji na biashara ambao umeanza kuonesha matunda makubwa. Mathalani, katika eneo la biashara kumeonyesha mafanikio makubwa kila mwaka. Mfano mwaka 2016 biashara kati ya Tanzania na Zimbabwe ilikuwa ni Tsh. Bilioni 18.3. Mwaka 2017 biashara ilikuwa Tsh. Bilioni 21.1. *Pili*; *kushirikiana* vyema kwenye masuala ya *utalii* kwa kutumia wingi wa vivutio vya utalii kama vile mbuga za wanyama, fukwe, maeneo ya kihistoria pamoja na Mlima Kilimanjaro. *Tatu*; Kushirikiana na kuimarisha eneo la *huduma za kijamii* zikiwemo afya, utamaduni, elimu na kukuza lugha ya kiswahili ambapo Tanzania ina Waalimu wa kutosha na hivyo...

MAPENZI: Kuna faida na ni muhimu Mpenzi wako kuwa rafiki yako pia

Kuna faida kubwa kwa wapenzi kuwa marafiki KUTOKANA na mila mbalimbali, baadhi ya watu wamekuwa wakiamini kwamba mwanamke ni daraja la pili. Daraja la kwanza na lenye kuthaminiwa ni mwanaume. Yaani mwanamke hana kauli kwa mwanaume. Anakuwa kama mtumwa fulani hivi.  Mwanaume akiongea, basi ni maelekezo kama vile rais wa nchi anavyotoa maelekezo kwa watu walio chini yake. Hakuna wa kupinga. Akisema sitaki kitu fulani kifanyike, basi ni mpaka atakapotoa maelekezo mengine. Vinginevyo, maelekezo ya awali yatabaki kusimama kama sheria.  Wapo baadhi ya wanawake wanaofurahia aina hii ya uhusiano kwa sababu ya mazoea. Kwamba wamekuzwa hivyo, mwanaume ni mwanaume. Huu ni mfumo ambao watu wengi wamekuwa wakiuishi. Kuna ambao wanakubaliana nao, wengine hawakubaliani nao.  Watu wengi sana wamekuwa wakiishi katika malumbano katika mahusiano yao kutokana na mfumo huu wa maisha. Mwanamke hataki kuishi kama mtumwa, mume anakomaa kuonesha uanaume wake. Hakuna anayekubali kushuka,...